Search This Blog

Monday, December 10, 2012

Mandela alazwa hospitali


PRETORIA, Afrika Kusini
ALIYEKUWA Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ametumia usiku katika hospitali katika mji mkuu wa Pretoria.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, Mandela mwenye umri wa miaka 94 alilazwa hospitalini Jumamosi iliyopita kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.
Msemaji wa Rais Jacob Zuma, alisema atatoa taarifa zaidi kuhusu hali ya Mandela, baada ya madaktari wake kumaliza kumfanyia vipimo na kutoa taarifa yao ya kitaalamu.
Katika taarifa hiyo ya awali, Ofisi ya Rais Zuma ilisema Mandela alikuwa akiendelea vizuri na kwamba kulikuwa “hakuna sababu ya kuwa na mashaka”.
Mandela anahitaji matibabu “Mara kwa mara ambayo ni thabiti kutokana na umri wake,” iliongeza taarifa hiyo.
Hakuna taarifa kamili juu ya nini kilichosababisha kufikishwa hospitali na haikuwekwa wazi kuwa ni wakati gani Mandela ataruhusiwa kutoka hospitalini.
Associated Press liliripoti kuwa wanamaombi walikusanyika katika Kanisa Katoliki la Regina Mundi katika eneo la Soweto huko Johannesburg kwa ajili ya kumfanyia maombi Mandela.
Kanisa hilo lilikuwa kitovu cha mikusanyiko ya kiimani na kufanya maziko ya watu waliouawa katika maandamano ya kudai haki wakati wa kipindi cha ubaguzi wa rangi nchini humo.
Mandela alistaafu kutoka shughuli za umma mwaka 2004 na tangu wakati huo imekuwa nadra kuonekana hadharani katika mikusanyiko ya umma.
Aliwahi kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini kati ya 1994 na 1999, na alipata Tuzo ya Nobel mwaka 1993.
Hiyo ilikuwa baada ya kutumia zaidi ya miongo miwili jela chini ya utawala wa wazungu wachache wa ubaguzi wa rangi.
Kwa mara ya mwisho Mandela alilazwa katika hospitali mwezi Februari mwaka huu, kw aajili ya kumpatia matibabu kutokana na tatizo la tumbo lililokuwa likimkabili.
Januari 2011 alipatiwa pia matibabu makubwa kutokana na tatizo la maambukizi ya ugonjwa wa kifua.
Mandela amekuwa akitumai muda wake mwingi kupumzika katika kijiji cha Qunu, ambacho ndiko alikozaliwa.

No comments:

Post a Comment