Search This Blog

Sunday, December 23, 2012

Wahamiaji haramu wavamia Tembo

USALAMA wa Tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi uko mashakani kufuatia kuwepo kwa vitendo vya uwindaji wa wanyama hao unaofanywa na watu wanaoaminika kuwa ni wahamiaji haramu.
Wawindaji hao husafirisha pembe hizo za Tembo na kuzipeleka nchi jirani ya Rwanda kwa ajili ya kuziuza.
Mabaki ya Mizoga ya Tembo waliouawa hifadhini.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Constantine Kanyasu, umebaini kushamiri kwa wahamiaji haramu wanaojihusisha na ufugaji na wamekuwa wakiingia kinyemela nchini na kuendesha shughuli za ufugaji katika ardhi ya Tanzania na baadhi yao kuendesha vitendo vya uhalifu.
Baadhi ya wananchi katika vijiji vya Kasulo na Ngoma wilayani Ngara walisema wahamiaji hao wamekuwa wakifika na mifugo yao na kujifanya wafugaji lakini wamekuwa wakishughulika na uwindaji haramu ikiwa ni pamoja na uuwaji wa Tembo na kisha kuuza pembe nchini Rwanda.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kasulo, Ramadhani Luzuba alisema wahamiaji hao ambao wamekuwa wakiendesha shughuli za ufugaji, wamekuwa wakifanya uharamia huo kwa msaada wa maofisa wa Idara ya wanyamapori.
“Hawa wafugaji wa Rwanda wamekuwa wakipanga na askari wanyamapori, wanapotaka kuuwa Tembo ni lazima wawasiline na askari wa Pori, wanapokubaliana basi ni lazima utoe fedha na kila Tembo mmoja anayeuawa wauaji hulipia kiasi cha Sh1.5 milioni hadi Sh2 milioni,” alieleza mmoja wa wafugaji.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, wafugaji wengi wanaojihusisha na uwindaji wa Tembo wamekuwa wakiuza pembe za ndovu na kununua Ng’ombe ambao wamekuwa wakiwafuga porini, na kisha ng’ombe hao wanapofika zaidi ya 500 au 1000 wamekuwa wakiuzwa na kupeleka  fedha kwao.
Mauaji ya Tembo
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kasulo, wilayani Ngara, Yusuf Katura  alisema kwamba kwa takwimu walizonazo hadi sasa jumla ya Tembo 19 wameuawa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita na wafugaji hao.
Idadi hiyo inafanya idadi ya jumla ya Tembo 37 ambao watakuwa wameuawa na majangili katika Pori la Hifadhi ya Burigi iliyopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera.
“Tatizo kubwa ni hawa wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakiingia porini kwa kisingizio cha ufugaji, wengi ni raia kutoka nchi za Rwanda na Burudi. Hawa wafugaji wageni wanaua sana Tembo, na ikitokea wakati wa kuua Tembo akawapo mwana kijiji akawaona, basi kinachotokea aliyewaona uuawa na kama ni mwanamke hubakwa ama kupigwa,” alieleza Katura.
Taarifa za ndani kutoka katika Hifadhi ya Burigi, zilidai kwamba jumla ya Tembo kumi waliuawa mwezi Julai mwaka huu katika maeneo ya Kulushasha na ndani ya hifadhi hiyo na kuongeza kati ya Tembo hao, watatu waliuawa katika eneo la Kulushasha na saba ndani ya hifadhi ya Burigi ambapo kati ya mwezi Septemba na Agosti Tembo wengine waliuawa katika maeneo ya Bwawani, eneo la Gerezani.
“Wastani wa Tembo kuuwawa kwa siku ni kati ya mmoja hadi wawili, hawa ni wale ambao tunawaona huku kijijini kwetu, lakini kule ndani ya hifadhi wapo pia wanauawa,hiyo hesabu yake  hatuijui ila siku akifa Tembo huko utaona tu magari ya maliasili yakifika porini kwa wafugaji na kuwakamata, lakini baada ya muda wanaokamatwa huachiwa,” alieleza mwanakijiji cha Ngoma wilayani Ngara.
Waasi wa Burundi
Aidha imeelezwa kwamba sehemu kubwa ya wahamiaji ambao wamekuwa wakijihusisha na uwindaji wa Tembo ni askari  wa vikosi vya waasi nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba wamekuwa wakiendesha zoezi la uwindaji kwa ajili ya kusaka fedha za kulipa askari pamoja na kuwalisha waasi waliopo porini.
“Suala hili serikali inajua, limekwisha elezwa sana katika vikao vya ulinzi vya ujirani mwema, kwamba hawa wahamiaji haramu ambao wanafuga katika ardhi ya Tanzania wengi ni mawakala wa waasi wa kivita wa Burundi na wale wa Kongo, lakini tunaona Serikali imekuwa kimya ,” alieleza mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kasulo.
Kauli ya Serikali
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Constantine Kanyasu akithibitisha kuwapo kwa wahamiaji haramu alisema suala hili linafahamika na kwamba lina historia ndefu na kwamba limeanza takribani miaka 10 iliyopita.
“Inasemekana kuna mahusiano kati ya wahamiaji haramu na wafugaji lakini pia hata na majangili wanaohusika na uwindaji wa Tembo wetu. Kwa kipindi ambacho nimekuwa mkuu wa wilaya hapa tumeendesha vikao vya kamati ya ulinzi na usalama kujadili jambo hili, bado tunajipanga kwa ajili ya kulishughulikia zaidi,” alifafanua.
Uhamiaji wanena
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, George Goerge akizungumza kwa njia ya simu jana alisema kwamba kwa sasa hana taarifa za uhakika kuhusiana na wahamiaji hao haramu, hii ni kutokana na kuwa mgeni katika ofisi yake na kuomba alifanyie kazi.
“Mimi hapa nimepewa ni mgeni nina siku 21, tangu nimeingia mkoa huu wa Kagera, sina taarifa zaidi mpaka nifanyie kazi mambo haya,” alieleza
Kauli ya Waziri
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Lazaro Nyalandu alisema Serikali inafuatilia kwa makini suala la mauaji ya Tembo na kwamba idadi yake inafahamika na kila amapouawa mmoja wamekuwa wakitambua.
“Wizara yetu kwa sasa imejikita kusaka wauaji hawa, kwanza ikiwa ni pamoja na kufuatilia mitandao yao, nani anawafadhili na anayewapatia silaha, tunafahamu kila hatua ambayo Tembo wetu wanapouawa,” alifafanua.
Source:  http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/1650394/-/item/1/-/rh3qia/-/index.html

No comments:

Post a Comment