Utata umeibuka kuhusiana na kifo cha Ofisa Usalama wa Taifa,
Peter Tyenyi, ambaye mwili wake umekutwa ndani ya kisima cha maji
kilichopo eneo la ofisi za idara zilizopo Kijitonyama, jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza kwa njia ya simu, msemaji wa familia
ambaye ni kaka wa marehemu, John Tyenyi alisema mwili wa Peter (53)
ulikutwa juzi ukiwa ndani ya kisima cha maji kilicho ndani ya eneo la
Ofisi za Usalama wa Taifa, Kijitonyama baada ya kutoweka tangu Jumatatu
ya Mei 27, alipoaga kwenda kazini.
“Peter alitoweka tangu Jumatatu alipoaga kwenda
kazini. Mimi nimepigiwa simu jana saa tano asubuhi nikiwa Mombasa nchini
Kenya kwamba amepatikana akiwa ndani ya shimo la maji,” alisema John.
Baadhi ya ndugu zake waliozungumza kwa sharti la
kutotajwa majina wakiwa msibani Kigamboni jijini Dar es Salaam, walisema
kuwa baada ya ndugu yao kutoweka mkewe Joyce Mwakilama aliwataarifu na
kuwasiliana na ofisi yake, lakini aliambiwa kuwa hata huko hayupo.
“Tuliwajulisha Usalama wa Taifa wakasema hata wao
hawajui. Lakini jana (juzi) wakatupigia simu kuwa amekutwa kwenye kisima
cha maji baada ya kutokea shida ya maji,” alisema mmoja wa wanafamilia
kwa sharti la kutotajwa jina na kuongeza:
“Walisema kuwa kisima hicho huwa kinalindwa, lakini tunashangaa ndugu yetu aliingiaje humo.”
Ndugu mwingine alisema: “Awali tuliambiwa kuwa
ndugu yetu yuko Muhimbili, tukaenda kuulizia tukamkosa. Baadaye
tukaambiwa yuko hospitali ya Lugalo, huko tukamkuta ameshaandaliwa kwa
mazishi. Tulipouliza tukaambiwa kibali cha kuzika kiko tayari na usafiri
wa ndege uko tayari tujiandae kusafirisha.”
Hata hivyo, msemaji wa familia John Tyeni alisema
kuwa ndugu hao walipinga kuusafirisha mwili huo, hadi ufanyiwe uchunguzi
(post mortem).
Mkurugenzi Usalama wa Taifa katikakati |
“Tulipokwenda hospitali tukakuta maofisa usalama
wamemchukua OCD wa Wilaya ya Kinondoni Wilbrod Mutangungwa na askari
wawili na kwenda kufanya post mortem. Yaani kulikuwa na ujanja ujanja
unafanyika. Sisi tukamchukua Ofisa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, RCO
Kimola na askari wawili na wapigapicha ndiyo tukafanya post mortem,”
alisema John.
Akizungumzia matokeo ya uchunguzi huo, John
alisema kuwa watapewa matokeo hayo baada ya kutoka kwenye mazishi
yatakayofanyika Musoma mjini mkoani Mara, baada ya kusafirishwa leo.
Hata hivyo alisema kuwa macho yake yalikuwa yametoka nje kwa sababu ya kujaa maji.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walidai kuwa mwili wake ulikutwa ukiwa umetumbuliwa macho huku nguo na viatu vikiwa bado mwilini.
Akizungumzia kifo hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Charles Kenyela alikiri kutokea tukio hilo na kusema kuwa bado uchunguzi
unaendelea.
“Ni kweli kuna ofisa usalama amefariki ndani ya
kisima, lakini bado tunachunguza. Kwa sababu itabidi tupate taarifa ya
daktari ndiyo tuunganishe na uchunguzi wetu,” alisema Kenyela.
SOURCE: http://www.mwananchi.co.tz/ habari/Kifo-cha-Ofisa-Usalama- chazua-utata/-/1597578/ 1868848/-/ahqc99/-/index.html
SOURCE: http://www.mwananchi.co.tz/
No comments:
Post a Comment