Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limemkamata mbunge wa Mtwara
Mjini (CCM), Hasnain Murji likimtuhumu kuchochea vurugu za kupinga mradi
wa bomba la gesi kutoka mkoani humo kwenda jijini Dar es Salaam.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Msemaji
wa Jeshi la polisi nchini, Advera Senso zinaeleza kuwa Murji alikamatwa
jana jioni nyumbani kwake maeneo ya Shangani mjini Mtwara.
Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM) Hasnain Murji |
Kukamatwa kwa mbunge huyo kunakuja ikiwa zimepita
siku tano tangu viongozi wanne wa vyama vya upinzani mkoani Mtwara,
kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Juni 4, mwaka huu
wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kula njama, kufanya uchochezi na
kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa hao ni Katani Ahmed Katani (33) na
Saidi Kulaga (45) wa CUF, Hassan Uledi (35) wa NCCR Mageuzi na Hamza
Licheta (51) wa TLP, wote wakazi wa Mtwara. Taarifa zaidi zilieleza kuwa
baada ya polisi kumkamata mbunge huyo, walifanya upekuzi katika nyumba
yake kwa saa kadhaa na baada ya kujiridhisha walikwenda kupekua na ofisi
yake.
“Amekamatwa kwenye saa 11:00 jioni, hata hati ya
kukamatwa kwake imeeleza kuwa anatuhumiwa kuchochea vurugu za kupinga
gesi inayopatikana mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam,” alisema Katibu
wa Mbunge huyo, Meckland Millanzi.
Katika ufafanuzi wake Senso alisema kukamatwa kwa
mbunge huyo ni jambo la kawaida na kwamba hivi sasa unaandaliwa
utaratibu ili faili lake lipelekwe kwa Mwanasheria wa Serikali.
“Acheni polisi ifanye kazi yake kama kutakuwa na
la ziada tutawaeleza ila kwa sasa tunaandaa utaratibu wa suala hili
kwenda kwa mwanasheria wa Serikali,” alisema Senso. Murji amekamatwa
ikiwa zimepita siku 16 tangu kutokea vurugu kubwa mkoani Mtwara
zilizodumu kwa siku mbili, ambapo polisi walipambana na makundi ya
vijana wanaopinga mradi wa bomba la gesi kujengwa.
Vurugu hizo zilizosababisha baadhi ya watu
kupoteza maisha huku wengine wakiachwa majeruhi na mali nyingi
kuharibiwa, ziliibuka baada ya hotuba ya bajeti ya wizara ya nishati na
madini kusomwa bungeni .
Mvutano kuhusu mradi wa bomba la gesi ulianza
Novemba 16, mwaka jana baada ya Serikali kutuma kamati inayoratibu maoni
ya sera ya gesi “The Natural Gas Policy of Tanzania -2013” ambayo
ilifika mkoani Mtwara kukusanya maoni ya wananchi.
Katika mikutano yake mjini Mtwara, wananchi wengi
hawakukubaliana na wazo la kusafirishwa gesi nje ya Mtwara kwa njia ya
bomba. Hali hiyo ndiyo iliyowasukuma viongozi wa vyama kuhamasisha
wananchi kuhusu suala hilo.
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Mbunge-CCM-mbaroni-vurugu-za-gesi-Mtwara/-/1597296/1876684/-/r4t0bbz/-/index.html
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Mbunge-CCM-mbaroni-vurugu-za-gesi-Mtwara/-/1597296/1876684/-/r4t0bbz/-/index.html
No comments:
Post a Comment