Na Zitto Zuberi Kabwe:
Maandamano ya amani
yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua hoja mbali mbali
kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye
mitandao ya kijamii hasa twitter na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita
waandamanaji wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na
wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.
Lakini kuna tatizo kubwa
zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali pia katika sekta
nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza
kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM. Sera hizi ndizo ambazo
zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa
muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama
tawala basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.
Wanaona katika nishati,
wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu
kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi
wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao
na zinaonekana kuendelea kushindwa.
Mtwara
na Lindi wanataka nini?
Watu wa Mtwara wanataka gesi
isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni
umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara
hawasemi kwamba Gesi yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme
uzalishwe Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa
nchi nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini.
Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la hasha.
Sio dhambi hata kidogo kwa
watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa
amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni yao. Kwanini tuwasute na
kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai
viwanda ili wapate ajira? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa
masikini kabisa nchini? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa
ukombozi wa kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau
‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau
kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya
Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe Fedha za Mkonge na
Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho? Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili
kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya Tumbaku.
Lakini tujiulize, watu wa
Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi
fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea –
Mtwara iling’olewa na Serikali huru ya Tanzania?
Tujiulize zaidi, hivi watu
wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa
umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi
katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri
ya Wilaya ya Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya
yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa
Mtwara wana Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao
kwenye Gesi asilia.
Mtwara
na Lindi wanakosea wapi?
Madai yao halali na mimi
binafsi na chama changu tunayaunga mkono. Lakini kuna mahala lazima waelimishwe.
Watu wa Mtwara pia wanapaswa
kuelewa kuwa juhudi zao zisiwatenganishe na Watanzania wengine kwani bado
utajiri wa Taifa unafadisha kikundi cha Watanzania wachache sana. Watu wa
Mtwara wanahitaji kuungana na watu wa Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga
na watu wa Kagera kudai utajiri wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya
kunufaisha kundi dogo la watu. Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na
Watanzania wengine kuzuia uporaji wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi
kijacho. Watu wa Mtwara wasijitenge wakawa peke yao na Gesi yao. Nguvu ya
mnyonge ni umoja.
Serikali isiyosikia
Serikali ina hoja kuhusu kujenga Bomba la Gesi kwa ajili ya kuzalisha
umeme kwa gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya Watanzania. Kwa
kuwa hii asilimia 14 ndio wenye sauti basi watu wa Mtwara wataonekana hawana
hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara mbilimbili kuhusu mradi huu wa
Bomba? Tunaambiwa na Wataalamu kwamba kuna uwezekano mkubwa mwakani gesi asilia
ya kiasi cha futi za ujazo trillioni 20 itakuwa imegunduliwa katika Kitalu
namba 7( block 7) ambacho kipo mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Temeke.
Iwapo gesi nyingi hivi itakuwa hapa Dar karibu kabisa na mitambo ya kuzalisha
umeme, mradi huu wa Bomba unaojengwa kwa trillioni za shilingi utakuwa na maana
tena? Huu mkopo utakuwa na tija?
Serikali imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba Dar dhidi ya
gharama za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na kuusafirisha umeme
kwenda maeneo mengine ya Tanzania? Serikali imeangalia faida ya kujenga gridi
nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na bwawa la Mtera? Leo
bwawa la Mtera lisipozalisha hata megawati moja hata Dar es Salaam izalishe
megawati alfu kumi umeme hautakuwapo maana uti wa mgongo wa gridi ni Mtera! Kwa
nini tusiwe na gridi nyingine yenye uti wa mgongo Lindi au Mtwara?
Tuwasikilize
watu wa Mtwara
Watanzania sio mabwege tena.
Kuwaita watu wa Mtwara ni wahaini, wapuuzi au watu hatari haisaidii kujenga
Taifa moja lenye watu huru. Serikali na wadau wote wa sekta ya Gesi likiwemo
Bunge washirikiane na watu wa Mtwara kuhusu miradi ya gesi asilia. Tuwe na
Azimio la Mtwara, tamko la kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa Gesi
bila kuathiri umoja wa Taifa letu.
Ujio
wa Sera, Maono na Uongozi Mbadala
Sasa hivi wananchi wa Mtwara
kama wananchi wa sehemu nyingine wanahitaji maono mbadala, uongozi mbadala,
sera mbadala na mwelekeo mbadala wa kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao,
utazingatia raslimali zilizopo na utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika
kutengeneza mfumo wa kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima.
Ni kwa sababu hiyo naamini
chama changu ni jibu sahihi kwa matamanio na kiu ya wananchi wa Mtwara na
sehemu nyingine nchini. Ikumbukwe kuwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2010
tulielewa haja ya kuangalia mikoa hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa
mwelekeo wa kipekee katika sera. Bado
tuna makusudio hayo tunapoelekea 2015 na tukishika Dola wananchi wa Mtwara na
sehemu nyingine zote zilizoachwa pembezoni mwa mafanikio wajue kuwa wamepata
rafiki na mshirika wa karibu wa kushirikiana nao kuleta maendeleo.
Siyo katika suala la gesi tu
bali katika nishati, maji, elimu, miundombinu, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii.
Mtwara kama ilivyo mikoa mingine ina raslimali za kutosha kuweza kuwainua
wananchi wake kimaisha, na zaidi ya yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi. Hili
ambalo ni kweli kwa Mtwara ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara,
Katavi, Lindi n.k.
No comments:
Post a Comment