Search This Blog

Thursday, December 6, 2012

Dowans yaidai Tanesco jumla ya Sh122 bilioni

KIASI cha fidia ambacho Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) liliamriwa na Mahakama Kuu Dar es Salaam, kuilipa Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura, Dowans, limezidi kupaa, na sasa Dowans inaidai Tanesco zaidi ya Sh122 bilioni.

Kiasi hicho cha fidia kimepanda kutoka Sh 94 bilioni likiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh 28 bilioni kutokana na riba ya asilimia 7.5 kwa siku.
Tanesco iliamriwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuilipa Dowans fidia hiyo Septemba 28, 2011, kufuatia tuzo ilioyotolewa kwa Dowans na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara [ICC].

Novemba 15, 2010, ICC iliamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia ya Dola za Marekani 65,812,630.03, kutokana na kuvunja mkataba wa kibiashara baina yake kinyume cha sheria.
Kufuatia uamuzi huo wa ICC, Dowans kupitia kwa Wakili wake Kennedy Fungamtama iliwasilisha maombi Mahakama Kuu ya kusajili tuzo yake iliyotolewa na ICC, ili utekelezwaji wa malipo hayo uweze kuwa na nguvu ya kisheria.

Licha ya Tanesco kupinga tuzo hiyo kusajiliwa, Septemba 28, 2011, Mahakama Kuu katika hukumu iliyotolewa na Jaji Emiliani Mushi ilikubali maombi ya Dowans na kusajili tuzo na kuiamuru ilipe.

Kutokana na uamuzi wa mahakama hiyo kuisajili tuzo hiyo ya Dowans, iliamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia hiyo, pamoja na riba ya asilimia 7.5, hadi malipo ya mwisho yatakapokamilika.

Hata hivyo kwa mujibu wa Wakili wa Dowans, Fungamtama, fidia hiyo imezidi kupaa na kufikia kiasi cha zaidi ya Sh122 bilioni ikiwa ni deni (fidia) la msingi la Sh94 bilioni pamoja na riba hiyo ya asilimia 7.5 kwa siku.

Wakili Fungamtama aliyabainisha hayo katika hati yake ya kiapo, aliyoiwasilisha katika Mahakama ya Rufaa, kufuatia maombi namba 142 ya mwaka 2012, yaliyofunguliwa na Tanesco mahakamani hapo, likiiomba mahakama hiyo isimamishe ulipwaji wa fidia hiyo.

Kwa mujibu wa kiapo hicho cha Wakili Fungamtama, hadi Novemba 20, 2012, wakati akiwasilisha kiapo hicho, fidia hiyo ilikuwa imeshafikia Dola za Marekani 76, 318,457.43.
Fungamkono amebainisha katika hati yake hiyo ya kiapo kwamba kulingana na kiwango cha kubadilisha fedha cha siku hiyo ambacho kilikuwa ni Dola moja sawa na Sh1606, fidia hiyo ilikuwa imefikia Sh122,567,446,655.4

Wakati Tanesco wakiwalisha katika Mahakama ya Rufani maombi hayo ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu, Dowans pia kwa upande wake imewasilisha maombi mawili.

Katika maombi ya kwanza, namba 131 ya mwaka 2010, Dowans wanaiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara wa mwaka 2010.
Katika maombi ya pili maombi namba 53 ya mwaka 2011, Dowans inaiomba Mahakama ya Rufani itupilie mbali taarifa ya Tanesco ya kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, ulioisajili tuzo ya Dowans.

Dowans inaiomba Mahakama ya Rufani itupilie mbali taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa ikidai kuwa Tanesco imeshindwa kwa mujibu wa kifungu cha 90 (1) cha Kanuni za Mahakama ya Rufani ya Tanzania za mwaka 2009.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, rufaa ni lazima ikatwe ndani ya siku 60 tangu siku kuwasilishwa kwa taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/1637622/-/11padd9/-/index.html

No comments:

Post a Comment