PRESS RELEASE
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Naibu
Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini ndugu Zitto
Zuberi Kabwe ameanza ziara ya kikazi nchini Ujerumani ambapo atahudhuria
na kuhutubia Mkutano mkubwa wa masuala ya ushirikiano wa kiuchumi kati
ya Ujerumani na Africa. Mkutano huo “Economic Conference: Commitment to
Africa Initiative” utafanyika Jijini Berlin kuanzia tarehe 9 – 11
Desemba 2012 na umeandaliwa na Wizara ya Ushirikiano wa Kimaendeleo ya
Serikali ya Ujerumani.
Katika ufunguzi wa Mkutano huo ndugu Zitto
atatoa mada kuhusu mgongano wa maslahi kati ya Kampuni binafsi na Jamii
ambapo ataongelea suala zima la makampuni makubwa ya kimataifa
yanavyonyonya rasilimali za Afrika bila kuwajibika kulipa kodi na
kuendeleza jamii zinazozunguka shughuli zao.
Atazungumzia pia mitaji
kiduchu inayokuja Afrika na fedha nyingi inayotoroshwa Afrika kupitia
rushwa, ukwepaji kodi na wizi wa rasilimali. Afrika inapoteza zaidi ya
dola za kimarekani 583 bilioni kila mwaka kutokana na utoroshaji wa
fedha unaofanywa na makampuni ya kimataifa kwa kushirikiana na baadhi ya
viongozi wa Afrika. Hata hivyo Afrika inapokea takribani dola za
Kimarekani 80 bilioni tu kwa mwaka kutokana na Uwekezaji (FDI) na
Misaada (foreign Aid). Tanzania ni moja ya nchi inayopokea misaada mingi
kutoka nje na moja ya nchi ambayo rasilimali zake zinatoroshwa na
baadhi ya viongozi wake kutorosha fedha na kuzihifadhi kwenye mabenki ya
Ulaya kama Uswiss.
Mnamo tarehe 11 Desemba ndugu Zitto atakuwa
kwenye jukwaa moja na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani kuzungumzia
namna bora ya kushirikiana kati ya Ujerumani na nchi za Kiafrika.
Miongoni mwa mapendekezo ya Zitto ni kuondokana na mfumo wa sasa wa
ushirikiano wa misaada na badala yake kuwe na ushirikiano wa kujengeana
uwezo ili kila nchi iweze kuhimili maendeleo yake yenyewe.
Katika ziara hii Zitto atakutana na
Mawaziri Wakuu wa majimbo ya Nord Rhein Westphalen jimbo ambalo
limefanikiwa sana katika vita dhidi ya ukwepaji kodi unaotokana na raia
wa Ujerumani kuficha fedha kwenye mabenki ya Uswiss na wa jimbo la Lower
Saxony kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ukarabati wa Meli ya Liemba na
kujenga mahusiano kati ya Mkoa huu na Mkoa wa Kigoma pia kati ya mji wa
PapenBurg na Manispaa ya Kigoma.
Zitto anatarajiwa kutembelea baadhi ya nchi
nyingine za Ulaya na kukutana na watu mbalimbali katika kuimarisha
mtandao wa kimataifa dhidi ya utoroshaji wa fedha kutoka Afrika (illicit
money transfer). Pia atakutana na watu binafsi wenye ujuzi na weledi
katika masuala haya ya kupambana na watoroshaji wa fedha. Zitto
anataraji kurudi nchini mnamo tarehe 16 Desemba 2012. Kwa namna
itaakavyowezekana umma utapewa taarifa kuhusu ziara hii kupitia akaunti
ya twitter na facebook ya ndugu Zitto. Pia mada zote atakazowasilisha
zitawekwa kwenye blogu ya zittokabwe.com kila itakapowezekana.
Waziri Kivuli wa Fedha na Naibu Kiongozi wa
Upinzani Bungeni anawatakia Watanzania wote kila la kheri katika
Sikukuu ya Uhuru wa Tanzania Bara. Utu, Uzalendo, Uadilifu na
Uwajibikaji ni silaha muhimu sana za kujenga Taifa lenye heshima na
jamii ya watu wenye fursa za kuendeleza maisha yao kwa haki na amani.
Tutimize wajibu wetu katika kuijenga Tanzania tuitakayo kwa ajili yetu
na kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini
8 Desemba 2012, Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment