Iwapo unaumwa, njia pekee ili upate kupona lazima upate matibabu.
Na kwa wale wa imani za kileo matibabu yao ni kwa njia ya uponywaji.
Lakini pia, wakati mwingine si mpaka uumwe. Unaweza kutumia dawa ili
kujikinga na maradhi kabla hata hayajakufika. Kinga ni bora kuliko
tiba, na pia ni vema kuswali kabla hujaswaliwa!
Naamu! CCM inayoongoza Serikali isiyokuwa na dini, nayo toka kale
inazo dawa na sindazo zake za kinga na matibabu. Miongoni mwa dawa na
sindano hizo ni UMOJA wa Kitaifa, UADILIFU wa Viongozi, CHEO kama
DHAMANA, na UONGOZI Bora wa Watu Kujiletea Maendeleo yao Wenyewe.
Vifuko vya dawa hizi, vingi vilijumuhiswa na kufanywa kifurushi kimoja
cha dawa iitwayo AZIMIO la Arusha.
Taifa chini ya CCM lilipougua ukabila na udini, viongozi wa CCM
walifanya utabibu haraka wakitumia dawa iitwayo UMOJA wa Kitaifa, rushwa
na ubadhilifu wa mali ya umma punde tu ulipoibuka, wale wote
waliobainika mara moja walidungwa sindano ya UADILIFU. Na mwenendo wa
Serikali katika kupambana na maadui (Ujinga, Umaskini, na Maradhi) wa
Taifa ilikuwa si kutembeza bakuli la kuomba misaada toka Ulaya na
Amerika bali kuwatumia VIONGOZI Bora kuwaunganisha wananchi katika
kuchangia vipawa, ujuzi, na mali katika kujiletea maendeleo yao kwa
kutumia rasilimali za nchi yao. Na hii ndiyo ilikuwa dhana kuu ya UJAMAA
na KUJITEGEMEA.
Lakini la ajabu, leo hii, CCM ndiyo kinara wa kuchua dawa ya
kubomoa UMOJA wa Kitaifa kwa kuendekeza Udini na Ukabila. Tumelishuhudia
hili wakati wa Uchaguzi Mkuu na limejirudia tena katika Chaguzi Ndogo
za Igunga na Arumeru. Tumeona jinsi CCM ya leo inavyoshangilia
wasio-WAADILIFU kuwadunga sindano za mauti Wanaopinga RUSHWA na
UBADHILIFU wa Mali za Umma. Na kubwa zaidi sote tu mashahidi, kwa CCM ya
leo Cheo si DHAMANA bali BIDHAA inayonunuliwa na Matajiri ili
wafanikishe mambo yao kupitia migongo ya Wapiga kura.
CCM imefanikiwa kwa muda kugeuza matumizi ya dawa zake bila
kudhurika. Habari njema ni kwamba, dawa zote sasa zimefikia ukomo wa
matumizi na zimegeuka sumu tena kali. Kwa sasa, UMOJA unaanzishwa na
Wananchi wenyewe kuikabili CCM. Wananchi hawakubali tena kugawanywa
katika makundi ya kidini wala kikabila ili CCM ipenye kuwatawala tena.
Wananchi wanawataka na wanawajua watu waadilifu. Na wanapojitokeza
wanaogawa RUSHWA, wananchi wanaipokea na kuila lakini haibatilishi
maamuzi yao yaliyo sahihi moyoni. Au wanaitumia hiyo pesa ya RUSHWA
kumchangia mtu muadilifu wampendaye ili afikie hatma ya kuwa kiongozi
wao. Hili limethibitika katika Uchaguzi Mkuu na limejirudia tena hivi
karibuni huko Arumeru Mashariki. Kiongozi ambaye Wananchi wanamhitaji ni
yule atakaye waongoza katika kutetea HAKI zao na kuwaunganisha
KUJILETEA maendeleo. Kitendo alichokifanya Kilema mmoja huko Mwanza, cha
kutoa Kuku wake wa Pasaka anadishwe katika Harambee ya kuchangia
madawati iliyoongozwa na Mbunge Wenje ili naye achangie watoto kupata
mazingira mazuri ya kusomea ni fundisho tosha kwa CCM na watoa RUSHWA.
Ili CCM ipone na dhahama ya sumu inayoendelea kuenea mwilini mwake,
lazima kwanza itapishwe na kukamuliwa sumu zote (Ubaguzi, Rushwa,
Ubadhilifu, Viongozi Uchwara/wafanyabiashara, n.k) na kisha ianze upya
matumizi ya dawa zake za awali (UMOJA, UADILIFU, UONGOZI BORA, CHEO kama
DHAMANA). Ni makosa ya makadirio ya kisiasa kwa CCM kufikiria jinsi
itakavyobaki madarakani hapo 2015. Hili jambo haliwezekani bila matumizi
makubwa yaliyopitiliza ya dola yatakaambatana na umwagaji wa damu isiyo
na hatia. Kadirio sahihi kwa CCM ni kufikiri nini itakuwa “Fall-Back
Position” hapo 2015 na nini kiandaliwe ili baada ya hapo warudi tena
madarakani ndani ya miaka mitano (5). Ni rahisi kwa CCM kurudi ndani ya
muda mfupi namna hii kwa sababu, pamoja na maandalizi yanayoendelea
kwenye vyama vya upinzani kushika dola, bado ni yatima wa mipango na
rasilimali watu makini wa kutekeleza na kukidhi matumaini ya Wananchi
ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitano (5). Vyama vya Upinzani
vimefanya na vinaendelea kufanya makosa makubwa sana kwa kuacha wananchi
kuweka matumaini makubwa kupitiliza juu ya nini watakifanya wakiingia
madarakani. Wamewaaminisha wanancnhi kwamba kile walichoshindwa CCM kwa
miaka 54 (hapo 2015) wao watakifanikisha ndani ya miaka mitano! Kwa kosa
hili, wategemee kuchukiwa haraka sana na kupingwa na wananchi hao hao
watakaokuwa wamewapa ushindi. Ebu nisitoke ndani ya mada maana hii
tayari ni mada nyingine kabisa.
Nakutakia tafakuri njema.
Source: http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/252439-zilizokuwa-dawa-za-ccm-ndizo-sumu-zinazoiua-ccm.html
No comments:
Post a Comment