WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mtoto wa Rais Jakaya
Kikwete, Ridhiwan wamezungumzia tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwao
kwamba wanamiliki rasilimali zenye thamani ya mabilioni ya shilingi.
Lowassa kwa upande wake amekuwa akidaiwa kuwa
tajiri anayemiliki kampuni kubwa za kibiashara na kumekuwa na taarifa
kwamba ana ukwasi ambao vyanzo vyake vinatia shaka na siyo rahisi
kuvitolea maelezo.
Ridhiwani Kikwete akiwa na Baba yake Jakaya Kikwete |
Wote wawili wamekuwa wakidaiwa kwamba baadhi ya mali zao wamekuwa wakiziendesha chini ya kivuli cha wafanyabiashara wengine wakubwa nchini ili kukwepa kuhojiwa walikotoa utajiri huo, taarifa ambazo hata hivyo imekuwa vigumu kuzithibitisha.
Hata hivyo jana kwa nyakati na mazingira tofauti,
Lowassa na Ridhiwan walijitokeza hadharani na kukanusha madai kwamba wao
ni matajiri wa kupindukia.
Lowassa kwa upande wake akiwa mjini Mbeya alisema
yeye siyo tajiri kama ambavyo imekuwa ikidaiwa lakini wakati huohuo
akasema “sijafilisika”.
“Wengi wanasema kuwa mimi ni tajiri siyo kweli,
lakini sijafilisika kutokana na kuchangia makanisa kwani nina marafiki
wengi ambao wananisaidia katika kuchangia makanisa nao pia
hawajafilisika,”alisema Lowassa.
Lowasa alitoa kauli hiyo alipokuwa akiendesha
harambee ya kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanachuo wanawake ambao ni
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Theofilo Kisanji cha mkoani Mbeya,
kinachomilikiwa na Kanisa la Moraviani Tanzania, Jimbo la Kusini
Magharibi.
Kiongozi huyo ambaye alichangia kaisi cha Sh25
milioni, alisema kila mtu ana wajibu wa kuchangia elimu na kwamba
mwanamke anapaswa kutazamwa kwa karibu zaidi kwani ndiye anayebeba
jukumu kubwa la kutunza familia.
Kwa upande wake Ridhiwan alisema: “Ikiwa mimi ni
tajiri wa kiasi kinachosemwa, basi mimi ninamzidi Bakhressa (Said Salim,
mfanyabiashara maarufu Afrika Mashariki), maana nimepewa kila hoteli
hapa mjini, kampuni za mafuta na kila biashara kubwa inayoanzishwa hapa
mjini ni ya Ridhiwan”.
Said Salim Bakhressa ni mfanyabiashara ambaye
anatajwa kuwa tajiri kuliko wote nchini na anashika nafasi ya pili
katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku akiwa miongoni mwa
wafanyabiashara 10 wanaonyemelea kuingia katika nafasi za juu za utajiri
Afrika.
Hata hivyo Ridhiwan ambaye hivi karibuni
alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC),
aliongeza: “Ninaweza kuwa nafanya biashara moja au mbili, lakini siwezi
kuwa mmiliki kiasi chote hicho cha mali.
Mtoto huyo wa Rais Kikwete alikuwa akijibu tuhuma
kwamba magari yake kumi ya kusafirisha mafuta yamekamatwa na kuzuiwa
katika mpaka wa Kenya na Tanzania, Namanga mkoani Arusha kutokana na
kukwepa kodi, taarifa ambayo aliikanusha.
Maelezo ya Ridhiwan
Maelezo ya Ridhiwan yamekua wakati kukiwa na taarifa kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inayashikilia malori mapya 10 ya kubebea mafuta yanayodaiwa kuwa ni yake, yanayodaiwa kuingizwa nchini.
Maelezo ya Ridhiwan yamekua wakati kukiwa na taarifa kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inayashikilia malori mapya 10 ya kubebea mafuta yanayodaiwa kuwa ni yake, yanayodaiwa kuingizwa nchini.
Hata hivyo Ridhiwan alikanusha kuhusika na
biashara ya mafuta akisema: “Ili kuwa na utajiri unaotajwa kwangu lazima
niwe nimekopa benki au nimeiba, sasa wale wanaonituhumu wasema nimekopa
benki gani na kama nimeiba basi wajitokeze watu kulalamika kuhusu wizi
nilioufanya”.
Mtoto huyo wa Rais Kikwete, alisema kumekuwa na
kile alichokiita uzushi wa ajabu na kwamba hajui wanaozusha mambo hayo
wana malengo gani. “Wameanza kusema kwamba nauza dawa za kulevya jambo
ambalo siyo kweli, mie sifanyi biashara za aina hiyo, kama kuna jambo
jingine tuunguze lakini hilo ni uzushi tu,”alisisitiza.
Habari zilizopatikana jana, zilidai malori hayo
mapya yanashikiliwa na TRA kituo cha mpakani cha Namanga kwa madai ya
kuwapo “utata” wa malipo ya ushuru wa forodha.
Taarifa za kuzuiwa kwa malori hayo zilianza
kuzagaa nchini wiki mbili zilizopita kupitia mitandao ya kijamii ukiwamo
mtandao maarufu wa Jamii Forums (JF).
Kulingana na taarifa hizo, watu walioshuhudia
magari hayo walidai yalikuwa zaidi ya 70 yakitokea Kenya kutengenezwa
bodi huku wengine wakidai yalikuwa ni mapya.
Baadaye taarifa hiyo ilibadilika na kusema kwamba
magari hayo yalikuwa 20 na kwamba ni malori 10 tu ndiyo yaliyolipiwa
ushuru na kuingia nchini, lakini malori mengine 10 yalikuwa yakiendelea
kushikiliwa kutokana na ukwepaji wa kodi.
“Ni kweli hayo magari ni ya huyo bwana mkubwa na
yalikuwa 20, lakini 10 yalilipwa ushuru halali”alidai ofisa mmoja wa TRA
kituo cha Namanga.
Ridhiwan alisema kuthibitisha kwamba tuhuma hizo
ni za uwongo haiwezekani mtu anayetajwa kuwa tajiri kama yeye ashindwe
kulipia ushuru wa malori kumi. “Uwongo mwingine huo, kama kweli
ningekuwa nina utajiri wote huo, nishindwe kulipia ushuru wa malori kumi
tu! Ndo maana nasema ni uwongo tena wa kutunga,”alisema.
Kaimu Meneja wa TRA Arusha, Theresia Mponeja
alipulizwa na gazeti hili wiki iliyopita alikanusha kuzuiwa kwa malori
hayo na kwamba hakuna taarifa hizo.
Lowassa na elimu
Katika hafla ya jana mjini Mbeya, Lowassa
aliendelea kuipigia chapuo elimu akisema: “Ni vizuri vijana wetu
wakazingatia elimu kwani bila elimu watashindwa kuhimili ushindani wa
ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
“Msipozingatia elimu mtabakia kuwa wachota maji na wakata kuni
daima. Ni vizuri vijana wetu mkafahamu kwamba bila ya elimu hamtaweza
kufika kokote,”alisema kiongozi huyo.
Aliwaasa wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii ili
kuweza kuboresha maisha yao na kuisaidia jamii, huku akitaka wajiepushe
vishawishi ambavyo vimekuwa kikwazo katika masomo yao. “Hata vitabu
vitakatifu vya Mungu elimu imepewa umuhimu mkubwa, Biblia inasema mshike
sana elimu na usimwache aende zake kwani huko ndiko uliko uzima wenu,
kwa wenzetu Waislamu Quran inasema itafuteni elimu kwa bidii hata
Uchina, maana ni kwamba itafute elimu hiyo hata kama utaipata mbali
kiasi gani,’’ alisisitiza Lowassa.
Akitoa taarifa ya chuo hicho, Kiongozi wa Kanisa
la Moravian Tanzania, Askofu Alinikisa Cheyo alisema ujenzi wa hosteli
hiyo ulianza 2011 na unatarajiwa kuwa na vyumba 87 vitakavyotoa fursa
kwa wanachuo 348.
Alisema katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo,
kanisa liliomba mkopo kutoka mamlaka ya elimu Tanzania na kukubali
kupewa Sh500 milioni na kwamba awamu hiyo iliyoanza Julai 2011,
iligharimu Sh580 milioni.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin
Meela aliyemwakilisha mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema
Serikali inaunga mkono juhudi za sekta binafsi hususan madhehebu ya
kidini katika kuchangia elimu.
Alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu, madhehu ya
dini yanaongoza kwa kuwa vyuo vikuu vingi. Chuo kikuu hicho cha Theofilo
Kisanji kilianzishwa 2004, ingawaje kulikuwa na chuo cha Theolojia
tangu miaka ya 1960.
Source: http://www.mwananchi.co.tz/ habari/Siasa/-/1597332/ 1629230/-/item/2/-/9eae0lz/-/ index.html
Source: http://www.mwananchi.co.tz/
No comments:
Post a Comment