Search This Blog

Sunday, November 25, 2012

Waliotumia ARV feki kuiburuta Serikali mahakamani

MIEZI mitatu baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kukamata dawa bandia za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa Ukimwi (ARVs), sasa walioathiriwa na dawa hizo wanajipanga kuifikisha mahakamani Serikali ili kudai fidia.

Wakizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili, baadhi ya viongozi wa vyama vya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wamedai kuwa Serikali inahusika katika suala hilo, hivyo haiwezi kujichunguza yenyewe na ndiyo maana imeshindwa kuwafikisha mahakamani wahusika hadi sasa.

Shehena ya dawa hizo aina ya TT-VIR 30 yenye toleo namba OC.01.85 zilizotengenezwa na Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Ltd (PTI), iligundulika ikiwa katika hospitali mbalimbali nchini zikiendelea kutolewa kwa wagonjwa.

Hali hiyo ilifanya Serikali ichukue hatua ya kuzuia usambazwaji wa dawa hizo huku ikiwasimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti na Ubora na Ofisa Udhibiti Ubora wa Bohari hiyo ili kupisha uchunguzi kwa madai ya kuruhusu kusambazwa kwa dawa hizo.

Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Shidepha), Joseph Katto alisema wanajipanga na wakati wowote watakutana na wataalamu huru wa masuala ya afya, wanasheria na wadau wengine kujadili na kuchukua hatua za kulifikisha suala hilo mahakamani.

"Tuna kawaida ya kukutana na wataalamu huru wa masuala ya afya kila linapotokea jambo lisilo la kawaida katika sekta ya afya, hilo ndilo ambalo tunatarajia kulifanya wakati wowote kuanzia sasa," anasema.

Alisema waliotumia dawa hizo walikumbwa na athari nyingi, ikiwa ni pamoja na kuvimba matumbo, ngozi kuharibika na wengine kukumbwa na hali ya kusikia kichefuchefu.

Ofisa Uhusiano wa wizara hiyo, Nsachriss Mwamaja alisema kuwa suala hilo linashughulikiwa na vyombo tofauti,  likiwa tayari kila kitu kitawekwa wazi na kwamba, ikibainika kuna tatizo hatua za kisheria zitafuatwa.


"Suala hili linashughulikiwa na mamlaka nyingi, nafikiri ni vizuri kuvuta subira," alisema Mwamaja.

Katto alifafanua zaidi kwamba, athari za dawa hizo zinaendelea kujitokeza kwa baadhi ya watu wanaoishi na virusi hivyo.

Alisema kuwa dawa hizo zilikamatwa na kuondolewa katika zahanati, vituo vya afya na katika hospitali lakini kwa walaji ziliachwa bila hatua zozote kuchukuliwa wala kutolewa maelekezo yoyote jambo ambalo ni kinyume cha haki za binadamu.

"Watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ambao wamekumbwa na athari za dawa hizo wapo njiapanda na hawajui wafanye nini.  Kibaya zaidi hakuna mbadala wa dawa hizo feki ambazo Serikali ilikuwa inatoa ruzuku kwa watengenezaji," Katto alisema.

Mwenyekiti huyo alisema anashangazwa na kigugumizi cha Serikali katika kuwafikisha mahakamani wahusika huku wanashuhudia ikiwafukuza  na kuwasimamisha kazi baadhi ya watuhumiwa bila hatima ya waathirika wa dawa hiyo kufahamika kwa wahusika.

Katto alisema anashangaa na wala hajui ni nini majukumu ya Bodi ya Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kwani Tanzania hivi sasa limekuwa jalala la dawa feki ambazo zinatengenezwa na kusambazwa hadi kwa walaji.

Mwenyekiti wa Shirikisho na Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Tanopha), Julius Kaaya alisema kuwa anashangaa Serikali kwa miezi mitano inamlipa fedha mtu ambaye anawapa dawa feki za kurefusha maisha bila kugundua lolote hadi ilipobainika hivi karibuni.

"Mimi nasema kuwa, Serikali inahusika katika sakata hili, hivyo haitaweza kumsimamisha mtu yeyote mahakamani, labda kiwepo chombo huru," alisema Kaaya.

Alisema kuwa Wizara ya Afya kuna watu hawawezi kuishi bila Ukimwi kuwapo na hao ndio ambao wameitumbukiza Serikali katika biashara hiyo ya dawa feki za kurefusha maisha ambazo tayari zimewaathiri maelfu ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

"Kama Serikali haihusiki basi iwapandishe kizimbani wanaohusika kwani ni kipindi kirefu sasa tangu kiwanda kifungwe na baadhi ya watendaji kusimamishwa ajira," alisema.

Kaaya alilalamika kuwa dawa hizo zimewasababishia  athari kubwa waliozitumia, lakini hadi sasa hakuna mamlaka yoyote iliyochukua hatua.

"Tupo mbioni kukutana na hakuna cha zaidi isipokuwa kuipeleka Serikali mahakamani kwa kuruhusu dawa hizo kuingia sokoni," alisema Kaaya.

Waziri wa Afya

Mara baada ya kukamatwa kwa dawa hizo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema Serikali itawachukulia hatua wahusika wote na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi  yao.

Naibu Waziri huyo alikiri dawa hizo kuingia katika mzunguko na kuwatoa hofu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kuwa dawa zilizopo sasa katika mzunguko (baada ya kukamatwa zile za awali) ni salama.
Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment