HATIMAYE Serikali imekiri kuwa rada inayotumika kwa ajili ya kulinda usalama wa anga nchini, imechoka. Kutokana na hali hiyo, usalama wa anga la Tanzania upo shakani, kutokana na ubovu wa rada hiyo ambayo ni muhimu kwa ajili ya usalama wa anga.


Taarifa hizo za majonzi kwa Serikali, zilielezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba alipotembelea Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), jijini Dar es Salaam jana.

Dk. Tizeba, alisisitiza umuhimu wa Serikali kununua rada nyingine haraka iwezekanavyo, ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na ubovu huo.

Dk. Tizeba alikiri kuwa amepata maelezo juu ya utendaji kazi wa rada hiyo, yanayotia wasiwasi kuhusu usalama wa anga hasa kwa usafiri wa ndege.

Kutokana na hali hiyo, ameitaka mamlaka husika kuwasilisha maombi mapema ofisini kwake, ili jambo hilo liweze kuingizwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014.

“Ni kweli rada yetu imechoka….kwa hili tusiweke mzaha kuna umuhimu wa kununua rada nyingine haraka iwezekanavyo, tukiendelea na mtindo wa kulilea tatizo hili siku moja litatuaibisha jamani,” alisema Tizeba.

Mapema Agosti, mwaka huu rada hiyo ilishindwa kufanya kazi baada ya kuharibika kifaa (Power Supply Unit) ambacho kiliigharimu Serikali Sh milioni 40.

Rada hiyo, ilinunuliwa kutoka Kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa Sh bilioni 40 na hivyo kuibua mjadala mkubwa, baada ya kubainika bei hiyo, ni kubwa kinyume na bei halisi.

Rada hiyo, ilinunuliwa kwa ushauri wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo, Andrew Chenge ambaye sasa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM).

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TCAA, Fadhili Manongi alisema mamlaka yake inafanyakazi katika wakati mgumu, kutokana na rada hiyo kusuasua.

Hata hivyo, Manongi alisema kulingana na ukubwa wa anga la Tanzania rada moja haitoshi na kusema Tanzania inapaswa kuwa na rada zisizopungua tano, ili kuongeza ufanisi wa usalama wa anga.

“Anga la Tanzania ni kubwa ikilinganishwa na maanga ya nchi nyingine za Afrika Mashariki, wenzetu Kenya wanatumia rada tano.

“Wanatumia rada tano kwa hivi sasa, licha ya anga yao kuwa ndogo kuliko ya kwetu, iweje sisi tuendelee kutumia rada moja tena iliyochoka na ukiangalia bei ya rada kwa sasa imeshuka kwa kiasi kikubwa,” alisema Manongi.

Alisema mamlaka yake inalazimika pia kufanya kazi katika anga ya Rwanda na Burundi na inatarajia kutumia Sh milioni 102, kwa ajili ya kutengeneza kituo kipya eneo la Kasulu, ili kuongeza ufanisi.

Taarifa hiyo ilimshitua naibu waziri, ambaye alihoji kama huduma za TCAA nchini Rwanda na Burundi zinalipiwa.

“Inakuwaje mnahudumia mataifa hayo, mnafaidika nini…kama hawawalipi inabidi wachangie gharama za kituo cha Kasulu…sababu mambo ya kubeba majukumu ya taifa lingine ni ya kizamani na tukiendelea hivi wanatudharau,” alisema Dk. Tizeba.

Mkurugenzi wa TCAA alikiri mamlaka yake hailipwi chochote na nchi hizo na wanafanya hivyo kwa kufuata agizo la Mamlaka ya Kimataifa ya Usalama wa Anga, (ICAO).

“Kwa kuwa nchi hizi zina eneo dogo la anga, kwa kuanzia umbali wa mita 24,500, inabidi tuwahudumie na hii inatokana na agizo la Mamlaka ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO),” alisema Manongi.

Chanzo: Mtanzania | Nov 30, 2012