Waziri wa Nishati na Madini |
Gazeti la The East African la Novemba 24 – 30, 2012 limetoa
taarifa kwamba jumla ya dola za kimarekani milioni 54 zimegundulika kuibwa na
watumishi waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la TANESCO
kupitia manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mtambo wa Umeme wa IPTL. Gazeti hili
limenukuu taarifa ya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Tanzania
(Controller and Auditor General). Taarifa hiyo inasema kuna kikundi (racket) ambacho
kazi yake kubwa ni kujifaidisha binafsi na mpango wa umeme wa dharura kupitia
manunuzi ya Mafuta mazito ya IPTL.
Itakumbukwa kwamba toka mwaka 2011 kumekuwa na shinikizo
lililotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Kamati ya Bunge
ya Nishati na Madini na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba zabuni za
ununuzi wa mafuta ya kuendesha mpango wa umeme wa dharura na mchakato mzima wa
manunuzi ya mafuta haya ufanyiwe uchunguzi wa kina (forensic audit).
Katika mkutano wa 3 wa Bunge la Kumi (April 2011) niliuliza
swali Bungeni kuhusu kashfa hii ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mtambo wa
IPTL na baadaye tarehe 16 Aprili 2011 nilimwomba Spika airuhusu Kamati ya
Nishati na Madini kufanya uchunguzi kuhusu kashfa hii. Kamati ya Nishati na
Madini chini ya aliyekuwa Mwenyekiti ndugu January Makamba ililitaka Bunge
kuazimia kufanyika kwa uchunguzi kuhusu suala hili kwenye Taarifa yake ya mwaka
2011 iliyowasilishwa Bungeni mwezi Aprili mwaka 2012. Waziri Kivuli wa Nishati
na Madini ndugu John Mnyika katika Hotuba yake ya Bajeti ya Wizara hiyo mwaka
2011 alipendekeza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kashfa hii pia. Juhudi zote
hizo hazikuzaa matunda.
Kipindi hicho kiwango kilichokuwa kinahojiwa kuibwa ni
shilingi bilioni 15 tu. Taarifa ya The East African kama walivyonukuu kutoka
kwenye taarifa ya CAG inaonyesha fedha zilizoibwa ni shilingi bilioni 86.
Zabuni za kununua mafuta ya kuendesha umeme wa dharura
zimekuwa zikitolewa bila kufuata utaratibu wa zabuni kwa mujibu wa Sheria ya
manunuzi. Hivi sasa kila mwezi Tanzania inatumia dola milioni 70 kununua mafuta
ya kuendesha mitambo ya umeme. Fedha hizi zinatoka Hazina na sehemu ndogo
kutoka TANESCO. Wakati fedha hizi bilioni 112 zinachomwa kila mwezi kununua
mafuta mazito na dizeli ya kuendesha mitambo ya umeme, Taarifa za kitaalamu
zinaonyesha kwamba Bwawa la Mtera hivi lina kina cha maji chini ya kiwango kinachotakiwa
na uzalishaji wa umeme ni asilimia 20 tu ya uwezo (installed capacity). Iwapo
TANESCO wataendelea kutumia zaidi maji yaliyopo Mtera, Mitambo itashindwa kazi
na Gridi nzima itasimama maana Mtera ndio nguzo kuu ya Gridi ya Taifa. Hali hii
ni hatari sana kwa uchumi na ulinzi na usalama wa Taifa. Kimsingi Gridi ya
Taifa ipo hatarini kutokana na kiwango cha Maji kilichopo Mtera hivi sasa na
kuendelea kupungua kwa kina hicho cha maji.
Wananchi wanapaswa kuelezwa kinaga ubaga nini kinaendelea
katika sekta ndogo ya umeme hapa nchini;
1.
Taarifa
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuhusu zabuni za manunuzi ya Mafuta ya
kuendesha mitambo ya umeme wa dharura iwekwe wazi na ‘racket’ inayosemekana
kuiba jumla ya shilingi bilioni 86 ionyeshwe na hatua za kisheria zichukuliwe
mara moja na bila kuchelewa.
2.
Waziri
wa Nishati na Maadini auleze umma hali yalisi ya sekta ya umeme nchini,
uzalishaji wa umeme upoje, hali ya maji katika bwawa mkakati la Mtera na nini
hatma ya mitambo ya IPTL, kesi zake na utekelezaji wa mapendekezo ya Bunge kuwa
kesi za kampuni hii zimalizwe nje ya mahakama. Pia Taifa lielezwe Mpango wa
Dharura wa umeme unakwisha lini maana muda uliotolewa na Bunge mwezi Agosti
mwaka 2011 tayari umekamilika. Waziri aeleze hatua agni amechukua baada ya
kukabidhiwa taarifa na CAG kuhusu maafisa waandamizi wa Wizara waliohusika na
wizi wa shilingi bilioni 86 za kununua mafuta ya IPTL.
3.
Waziri
wa Fedha na Uchumi aueleze umma ni kiwango gani cha fedha Hazina imetoa kununua
mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura kati ya Mwezi Novemba mwaka
2011 na Oktoba mwaka 2012 na kama taratibu zote za zabuni zilifuatwa na pale
ambapo hazikufuatwa ni hatua gani PPRA wamechukua dhidi ya waliokiuka sheria ya
manunuzi na kuleta hasara ya mabilioni ya fedha kwa Serikali.
No comments:
Post a Comment