Habari za uhakika kutoka ya Mahakama ya Rufaa inayosikiliza kesi hiyo, zilisema kuwa uamuzi huo utatolewa jijini Dar es Salaam ambapo shauri hilo linasikilizwa na majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande, Natalie Kimaro na Salum Massati.
Awali kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama, Maximilan Malewo, uamuzi wa pingamizi hizo ulipangwa kutolewa Novemba 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ingawa wakati Jaji Mkuu Chande akiahirisha shauri hilo jijini Arusha baada ya kusikiliza hoja za pingamizi kutoka kwa mawakili wa wajibu rufaa na majibu toka kwa mawakili wa mleta rufaa, alisema uamuzi huo ungetolewa Oktoba wakati wa vikao vya mahakama hiyo.
Oktoba 2 mwaka huu, rufaa hiyo iliposikiliza kwa mara ya kwanza mjini Arusha, mabishano makali ya kisheria baina ya mawakili wa pande zote yalitawala katika kesi hiyo ambayo Lema anapinga kuvuliwa na Jaji Gabriel Rwakibarila.
Mabishano hayo yalizuka baada ya upande wa wajibu rufaa kuwasilisha mahakamani hapo hoja zao za pingamizi za awali nne wakidai kuwa rufaa hiyo ni batili kwani imefunguliwa na tuzo ya Mahakama Kuu ambayo ina upungufu wa kisheria kwani haikugongwa muhuri wa mahakama.
Mawakili wa wajibu rufaa, Medest Akida na Alute Mughwai, waliwasilisha pingamizi hilo mbele ya majaji watatu wa mahakama ya rufaa wakiongozwa na Jaji Mkuu, Othman Chande, Natalia Kimaro na Salum Massati ambapo upande wa waleta rufaa uliwakilishwa na mawakili, Method Kimomogoro na Tundu Lissu huku Mwanasheria Mkuu akiwakilishwa na mwanasheria wa serikali, Timon Vitalis.
Wakili Mughwai akiieleza mahakama kuwa tuzo iliyotolewa mahakamani haikubaliani na hukumu ya mahakama kwani imezingatia vifungu vya sheria tofauti ambapo kwenye hukumu ilitaja kifungu cha sheria za uchaguzi namba 113 kipengele cha namba moja mpaka saba wakati kwenye kukazia hukumu ilitaja kifungu namba 114 kipengele namba moja mpaka saba.
Aliieleza mahakama kuwa hati hiyo ya kukazia hukumu haikuandikwa kama inavyopaswa kisheria kwani ina upungufu wa baadhi ya maneno yanayoonesha imetolewa na nani, wapi na lini jambo alilodai kuwa imekiuka kanuni za masijala za Mahakama Kuu, hivyo kutaka rufaa hiyo itupwe na mahakama itoe fursa kwa upande wa waleta rufaa kujipanga upya kuleta upya rufaa yao mahakamani.
Katika pingamizi la nne, Mughwai alidai kuwa hati hiyo ya kukazia hukumu haikuwa na muhuri wa Mahakama Kuu jambo alilodai kuwa inaifanya ikose sifa kisheria kwani muhuri ndiyo uhalali wa nyaraka ya mahakama, vinginevyo inakuwa ni karatasi tu.
Akijibu pingamizi hizo za awali wakili Kimomogoro aliieleza mahakama kuwa baada ya Jaji Rwakibarila kutoa hukumu, jalada lilihamishiwa Dar es Salaam, hivyo hakukuwa na muda wa kupitia hukumu na hati ya kukazia hukumu hiyo kwani walikuwa wanaletewa nyaraka hizo kutoka huko.
“Waheshimiwa majaji wa Mahakama ya Rufaa, wakili mwenzetu, Mughwai, ametueleza hapa aliomba mara mbili tofauti apewe tuzo hiyo ikiwa imesahihishwa lakini hakupatiwa majibu, katika mazingira hayo alitegemea sisi tungeipata vipi?” alihoji wakili huyo huku akielezea kushangazwa na hatua ya mawakili wa wajibu rufaa kutowapa nakala ya barua hizo.
Akinukuu maamuzi mbalimbali ya mahakama hiyo kuhusiana na masuala ya hati ya kukazia hukumu pamoja na kanuni mpya za uendeshaji mashauri ya Mahakama ya Rufaa ya mwaka 2009, Wakili Kimomogoro alisema kuwa si kila hati ya kukazia hukumu yenye upungufu inaifanya iwe batili.
Alisema kuwa hati hiyo ya kukazia hukumu imekidhi vigezo vyote muhimu ikiwemo kuonyesha namba ya kesi, majina na hadhi ya wadau, mambo yaliyokuwa yakidaiwa, imeainisha kilichoamuliwa na mahakama pamoja na gharama.
Aliendelea kuieleza mahakama kuwa hata jaji aliridhika nayo ndiyo maana aliamua kuisaini jambo alilosema kuwa endapo jaji aliridhika kimakosa wao kama mawakili hawawezi kumfuata na kumwambia hapa umeridhika vibaya hebu ridhika vizuri ili tukakate rufaa bali wanachofanya wao ni kuendelea na hatua inayofuata ambayo ni kukata rufaa kama walivyofanya.
Hata hivyo, Kimomogoro alisema kuwa suala la tuzo hiyo kutogongwa muhuri si suala la jaji bali ni suala la utawala kwani anayegonga muhuri mara baada ya jaji kusaini ni msajili wa mahakama.
Alisema kuwa endapo mahakama hiyo itakubaliana na hoja ya pingamizi ya wajibu rufaa kuwa hati hiyo ya kukazia hukumu ni batili basi na mteja wake, Lema atakuwa ni mbunge halali wa Arusha Mjini.
Alisema kuwa makosa yaliyofanyika ni ya kawaida ambayo hayaathiri kiini cha tuzo hiyo kwa kile alichoieleza mahakama kuwa tuzo haiwezi kuwa batili kutokana na mchoro au mamlaka iliyoitoa, bali kinachoangaliwa ni maamuzi yaliyo ndani ya tuzo hiyo.
Aliomba mapingamizi hayo yatupwe kwa gharama za wajibu rufaa kwani kasoro zilizojitokeza zinaweza kurekebishwa wakati shauri hilo likiendelea au kila upande ubebe gharama zake kwenye usikilizwaji wa mapingamizi hayo kutokana na kuwa upande wa wajibu rufaa nao walishaandaa rufaa panda.
Kwa upande wake wakili wa serikali aliieleza mahakama hiyo kuwa anaunga mkono hoja za waleta rufaa huku akiweka wazi kuwa hati ya kukazia hukumu hutolewa kwenye mashauri ya madai ambapo alisema kuwa kazi ya kuweka muhuri si ya jaji bali ni ya masijala ya mahakama kuu.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote Jaji Mkuu, Chande, alisema kuwa pande zote zitajulishwa siku ya kutoa uamuzi ambapo aliahirisha kikao hicho kilichoanza tokea Septemba 3, mwaka huu, ambapo tayari mahakama hiyo ilishatoa msimamo kuwa endapo hoja za pingamizi zitasikilizwa basi rufaa itasikilizwa jijini Dar es Salaam katika kikao kinachotarajiwa kukaa mwezi huu.
No comments:
Post a Comment