Search This Blog

Sunday, July 14, 2013

Sheikh wa wilaya Arusha amwagiwa Tindikali

Wakati vumbi la matukio ya kigaidi ya milipuko ya bomu kanisani na kwenye mkutano wa kampeni za Chadema halijatulia, tukio lingine linalohusishwa na ugaidi limetokea wilayani Arumeru kwa Sheikh wa wilaya hiyo, Said Juma Makamba aliyejeruhiwa kwa kumwagiwa usoni kimiminika kinachoaminika kuwa tindikali.
Sheikh Makamba anayekaimu nafasi hiyo alikutwa na hayo kati ya Saa 4:00 hadi 5:00 usiku wa kuamkia juzi akitoka kusali Tarawei na alilazwa wodi namba nne katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa matibabu.
IGP Said Mwema
Jicho la kushoto la Sheikh huyo limeathirika, huku akiwa amebabuka na kuvimba usoni, kifuani, mkono wa kushoto na mgongoni.
Akizungumza kwa taabu kitandani kwake alikolazwa, Sheikh Makamba ambaye pia ni Imamu wa Msikiti wa Sekei wilayani Arumeru alisema alimwagiwa tindikali muda mfupi baada ya kurejea nyumbani kwake akitoka kuswali.
“Nilipotoka Msikitini, nilisindikizwa hadi nyumbani na vijana wawili nilioongozana nao kutoka msikitini ambao walihakikisha nimeingia ndani salama. Lakini kabla ya kulala nilitoka nje kwa ajili ya kujisaidia kwenye choo cha nje ndipo nilimwona mtu amesimama pembeni ya nyumba nikiwa najitahidi kumwangalia ili nimtambue, ghafla alinimwagia kitu cha majimaji usoni,” alisema Sheikh Makamba.
Ingawa hataki kuingia kwa undani kuhusu anaowatuhumu na sababu za kumwagiwa tindikali, Sheikh Makamba alisema anadhani jambo hilo linatoakana na ugomvi wa madaraka msikitini hapo.
Katibu wa Bakwata Wilaya ya Arumeru, Sheikh Yahaya Husein Mwangela aliwaomba polisi kuchunguza tukio hilo ili kuondoa hofu miongoni mwa viongozi wa Bakwata.
Hili ni tukio la pili kwa viongozi wa Bakwata Arusha kumwagiwa tindikali baada ya Oktoba mwaka jana, Katibu wa Baraza hilo Mkoa wa Arusha, Abdukarim Njonjo kulipuliwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu. Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa hadi jana kulikuwa hakuna mtu aliyekamatwa.
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Sheikh-wa-wilaya-arushiwa-tindikali/-/1597296/1914272/-/xxpuox/-/index.html

No comments:

Post a Comment