Search This Blog

Tuesday, July 16, 2013

Chadema: Tendwa alibariki kuanzishwa ‘Red Brigade’


Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimesema Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alibariki kuundwa kwa makundi ya vijana ndani ya chama hicho, yanayoitwa ‘Red Brigade’.
Hatua hiyo ya Chadema imekuja baada ya Tendwa kutishia kuifuta Chadema, iwapo wataendelea na mpango wao wa kuanzisha kambi za mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake nchini.
Katika taarifa yake, aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, na kusainiwa na Naibu Msajili, Rajab Juma kwa niaba yake, Tendwa alieleza kushangazwa na kusikitishwa na hatua hiyo ya Chadema kwa kuwa walishakatazwa mpango huo tangu mwaka 2004.
“Msajili anavikumbusha vyama vyote vya siasa hasa Chadema kuwa, kifungu cha 19 cha Sheria ya vyama vya siasa kinampa uwezo wa kufuta usajili wa chama chochote kinachokiuka masharti ya usajili au kifungu chochote cha sheria ya vyama vya siasa. Kifungu cha 20 cha sheria ya vyama vya siasa kinasema uamuzi wa msajili ni wa mwisho na hauwezi kukatiwa rufaa mahakamani,”
 alisema Msajili.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema: “Tendwa alikuwepo kwenye mkutano wa Chadema wa Agosti 13, 2006 uliopitisha katiba mpya ya chama hicho.
“Katika katiba mpya tuliweka kifungu kinachosema, Chadema itakuwa na chombo cha kulinda
uongozi na mali za chama kikiitwa Red Brigade...Tendwa katika mkutano aliipongeza Chadema kwa mabadiliko hayo ya katiba.
“Katiba ya Chadema ilisajiliwa katika ofisi yake kwa mujibu wa sheria mwaka 2006 na kusema Chadema imekidhi matakwa yote,”
Kuhusu madai ya Chadema kwamba CCM kina kambi ya namna hiyo, Tendwa alisema hayana msingi, badala yake amekitaka kuwasilisha ushahidi katika taasisi husika ikiwamo ofisi yake unaoonyesha kambi za mafunzo za vijana wa CCM, ili suala hilo liweze kushughulikiwa kisheria.
“Kwa kuwa hivi sasa sheria zinakataza suala hili, hazijabadilika na viongozi wa Chadema ni walewale waliositisha kutekeleza mpango huo mwaka 2004, haieleweki nia yao sasa ni nini.
Kama ni kupima matokeo iwapo watatekeleza mpango huo, utakuwa si uamuzi wa busara kwa uhai wa chama chao,’’ alisisitiza msajili.
Alisema kuwa mwaka huo 2004 hata Chama cha Wananchi(CUF)kupitia kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilfred Lwakatare kiliwahi kuomba ufafanuzi kwa msajili kuhusu nia yao ya kutaka kuanzisha mafunzo ya ukakamavu wa kujilinda kwa vijana wake kila wilaya, ambapo walikataliwa kwa kuwa ni kinyume cha sheria.Msajili pia alitumia fursa hiyo kuviasa vyama vyote vya siasa kutumia muda wao kufanya shughuli za siasa,ili kuchangia maendeleo ya nchi, badala ya kutumia uwezo wao na muda kubuni mambo yanayoleta mtafaruku na kuhatarisha amani na utulivu nchini.
Source:  http://www.mwananchi.co.tz/habari/Siasa/-/1597332/1916520/-/a5icxkz/-/index.html

No comments:

Post a Comment