Freeman Mbowe kushoto na Dr. Wilbrod Slaa



Humu duniani kuna mambo mengi sana yanayopingana. Yapo ya kushangaza, yapo ya kuchukiza, yapo yanayokera na kuchefua roho, yapo ya kufurahisha na kuburudisha na yapo mengine ya vioja na vituko. Haya ya vioja na vituko wakati mwingine ndiyo hayo hayo ya kuudhi, kushangaza na kuchukiza kama siyo ya kukera na kuchefua roho vile vile. Mwitikio wa serikali ya Rais Kikwete na Chama cha Mapinduzi kufuatia uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kutoa mafunzo ya kujilinda kwa chombo chake cha ulinzi na usalama wa chama – Brigedia Nyekundu – unaangukia kwenye hilo la mwisho.


Uamuzi wa CHADEMA umechelewa
Uamuzi wa CHADEMA kutoa mafunzo na kuchukua uamuzi wa kujihakikishia ulinzi wake yenyewe umechelewa sana. Uamuzi huu ulitakiwa uje kabla hata ya uchaguzi mkuu wa 2010 ambapo tulishuhudia vitendo mbalimbali ambavyo vilionesha wazi kuwa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama havikuwa tayari kuhakikisha usalama kwa CHADEMA kama vinavyofanya kwa Chama cha Mapinduzi.


Na tunaweza kusema umechelewa kwelikweli kwa sababu baada ya matukio ya Igunga kwenye uchaguzi mdogo kufuatia kujiuzulu kwa kashfa kwa Mbunge wa muda mrefu wa jimbo lile Rostam Aziz CHADEMA ilipaswa mara moja kujiangalia mfumo wake wa ulinzi na usalama wa viongozi wake na wanachama wake. Matukio mengine yaliyofuatia baadaye – ya Arusha, Mbeya, Tukuyu, Songea, Iringa na sehemu nyingine yalipaswa kuwa kichocheo tu cha kuharakisha kujichunguza huku na kuchukua hatua.


Ni Uamuzi unaoteteeka Kikatiba
Baadhi ya watu – hasa mashabiki wa CCM na wale wa Serikali –wameitikia kwa kusema kuwa uamuzi huu wa CDM unalingana na kuunda jeshi kitu ambacho Kikatiba hakiruhusiwi isipokuwa kwa serikali tu. Wanafanya hivi kwa kunukuu Ibara ya 146 ya Katiba ambayo inasema katika kifungu chake cha kwanza kuwa “Ni marufuku kwa mtu yoyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania jeshi la aina yoyote.”
Haiitaji uelewa mkubwa kutambua kuwa Ibara hiyo ya Katiba haikatazi kuundwa kwa makampuni ya ulinzi, vikundi vya ulinzi wa jadi, au hata vikundi vya ulinzi vya vyama vya siasa, makanisa, misikiti n.k. Kinachokatazwa ni kuundwa kwa jeshi (army) kwa maana ya chombo cha kivita. Kwa sababu tukikubali tafsiri finyu ya Ibara hiyo itabidi serikali itoe maelezo ya kutosha ya kwanini kuna makampuni mbalimbali ya ulinzi nchini ambayo yamesajiliwa na mengine yanabeba silaha za moto kabisa. Yapo makampuni makubwa kama KK Security, Knight Support, Bison Security, Dragon Security Services, Group 4 Security Ltd, Securex Tanzania, Aurora Security Tanzania, na Warrior Security –nikitaja machache – ambayo yote yanatoa huduma mbalimbali za ulinzi na usalama. Baadhi ya makampuni haya yameanzishwa na watu waliowahi kuwa wanajeshi na wengine wametumikia majeshi yetu katika ngazi mbalimbali.




Mkuu wa Kampuni ya Warrior Security akitembelea maafisa wake



Na tunaweza pia kuangalia kwa namna nyingine na kuona kwanini hoja ya serikali kupinga CHADEMA kujilinda haina mashiko, ya kipuuzi na yenye kuonesha kuchanganyikiwa kusiko na sababu tunaweza kuangalia eneo jingine ambalo tunaweza kulifananisha zaidi na CDHADEMA. Wengi wetu tumewahi kuhudhurudia hafla mbalimbali na burudani mbalimbali ambapo tunawakuta watu wanaoitwa “mabouncer” yaani walinzi wa milangoni. Iwe kwenye matamasha ya muziki, mikutano ya kidini au makusanyiko makubwa watu waliovaa tsheti za “Security” au “Staff” wanaonekana wakitoa ulinzi. Wote hawa wanafanya kile ambacho tunaweza kwa kabisa kukiita “kujilinda” yaani siyo tu wanalinda watu waliopo pale lakini pia wanalinda maslahi ya watu walioandaa tamasha au shughuli hiyo. Sasa je hawa nao wanavunja Katiba kwa kuamua “kujilinda”?


Na ukiangalia baadhi ya makampuni haya yamejipanga na yanafanya kama kama majeshi. Wanavaa sare na wengine wana nyenzo zinazokaribiana kabisa na zile za vyombo vya kijeshi; lakini hatujasikia serikali ikisema kuwa “vimeanzisha majeshi kinyume na Katiba”! Picha za hapa chini zinadokeza uwepo wa vikundi vya kujilinda (makampuni) ambavyo havijaanzishwa na serikali na hoja inaweza kujengwa kuwa vinakiuka Katiba.



Nafasi ya Polisi katika Kujilinda
Sasa, sote tunatambua kuwa uwepo wa makampuni mbalimbali ya ulinzi au vikundi mbalimbali vya kujilinda haina maana kuwa polisi hawawezi kuhusika au hawatakiwi kuwepo; na haina maana kabisa kuwa watu wanaofanya shughuli ya kujilinda wamejipa majukumu ya polisi. Ukweli rahisi kuona ni kuwa polisi kama chombo cha umma kina watumishi wachache, ambao hawawezi kuwepo mahali pote wakati wote kuhakikisha ulinzi na usalama. Hivyo katika kile ambacho kinatambulikana kama “ulinzi shirikishi” watu na makundi ya watu yanapofanya shughuli mbalimbali za kujilinda wanasaidia polisi kuhakikisha usalama na badala ya kuwakataza watu hao kufanya hivyo jeshi la polisi linatakiwa kuwapongeza na kuhakikisha kuwapatia msaada wakati unapohitajika.


Mazingira ya Sasa yanalazimisha CDM kujilinda
Kama nilivyodokeza hapo juu CHADEMA imechelewa kuchukua uamuzi wa kuanza kujilinda hasa katika mazingira ambayo vyombo vya dola viko dhidi yake. Katiba inampa kila Mtanzania haki ya “kulinda, kuhifadhi, na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa”. Matukio ya mashambulizi dhidi ya CHADEMA na viongozi wake yanatishia umoja wa taifa na hivyo wana CHADEMA kama Watanzania wengine wanaitwa kulinda na kuhifadhi umoja huu kwa kuhakikisha kuwa matukio kama haya hayajirudii tena kwenye mikutano yao. Jukumu hili la kulinda halihitaji kibali cha Rais, Jaji Mkuu, Mwanasheria au Kiongozi wa juu wa CCM; ni jukumu ambalo kila Mtanzania analo na anapaswa kujitambua kuwa analo.
Mauaji ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mikutano ya CHADEMA karibu yote hadi hivi sasa yamehusishwa na polisi – watu waliopaswa kutoa ulinzi. Na ushahidi wote unaonesha kuwa Jeshi la Polisi halijabadili mtazamo wake wa utendaji na linaendelea kuangalia CHADEMA kama chama cha waleta vurugu na hivyo limejiandaa mara zote kuingilia kati kuleta usalama. Na uamuzi wa Rais Kikwete kuwapongeza na kuwapandisha vyeo baadhi ya maofisa ambao wanatajwa kuhusika na mitazamo hii hasi ndani ya jeshi la polisi ni uthibitisho dhahiri kuwa CHADEMA hawawezi – na watakuwa wapumbavu – kutegemea ulinzi wa polisi. Maana kama polisi wanapotoa ulinzi ndio yanatokea mauaji itakuwaje kama hawatoi!?


CDM Iandae mpango mzuri wa kujilinda
Kwa vile CHADEMA wamesema wanataka kutoa mafunzo ya ukakamavu kwa vijana ili kusaidia kujilinda kwa kupitia makambi nchini pote hatari ya hili ni kuwa kama CCM na makambi yake. Tayari wananchi wanajua kile kinachozalishwa kutoka makambi ya CCM, CHADEMA haipaswi kuiga hilo. Kwa vile lengo la CHADEMA ni kuhakikisha kuwa inajilinda na kulinda wanachama, mali na viongozi wake basi mpango wake wa kujilinda hauwezi na haupaswi kuwa kama wa CCM au unaoshabihiana na ule wa CCM kwa namna yoyote ile; hatutaki CHADEMA ifanane na CCM maana ikifanana na CCM haitakuwa tofauti na CCM na watu wanachotaka ni tofauti na hasa kama ni tofauti nzuri na bora.



Hivyo, CHADEMA wasiwe kama wana –beep – tu na kutishia bali wajipange vizuri na wawaeleze wanachama na Watanzania mpango huu na utekelezaji wake; hakuna kambi za siri au mafunzo ambayo yataweza kutafsiriwa kama kujiandaa kulipa kisasi.


Jeshi la Polisi na Serikali Wajiulize Wametufikisha Vipi Hapa?
Badala ya kuipiga mikwara CHADEMA na kuwatishia viongozi wake uongozi wa jeshi la polisi na Ikulu inapaswa wawe na ujasiri wa kusimama mbele ya vioo na kujiuliza maswali ambayo majibu yake yagonge visogo vyao. Maswali hayo baadhi yake ni haya:
a. Kwanini CHADEMA imefikia mahali pa kutaka kujilinda?
b. Vyombo vya usalama vimepungukiwa nini kiasi kwamba chama kikuu cha upinzani nchini haiviamini?
c. Je, uongozi wa vyombo vya usalama una mahusiano gani ya kikazi na viongozi wa CHADEMA?
d. Je, ni kwanini matukio yaliyotokea na kugusa CHADEMA hayachunguzwi kwa kasi ile ile kama matukio mengine – mfano mauaji ya Padre Mushi kule Zanzibar yamepewa uzito wa uchunguzi (Hadi Rais kaingilia kati) kuliko mauaji ya mtoto mdogo Arusha?
e. Je vyombo vya usalama vinaweza kuchukua hatua gani kurudisha imani ya CHADEMA na wanachama wake kuwa vinafanya kazi kwa weledi na siyo kama sasa ambavyo vimebatizwa majina ya CCM kama PoliCCM (badala ya Polisi), na TICCM (Badala ya TISS) n.k?
f. Rais Kikwete ajiulize kwanini wale aliowakabidhi dhamana ya kusimamia usalama nchini wameifikisha nchi hapa – kuwalaumu CHADEMA kwa kujilinda ni kukosa umakini na kuwa na usahaulifu unaobagua (selective amnesia).


Cheo cha Kamisaa wa Polisi Kirejeshwe
Lakini kubwa zaidi naamini wakati umefika kwa Jeshi la Polisi kufikiria kurejesha cheo cha Kamisaa wa Polisi (Police Commissar) ambaye atashughulikia masuala ya vyama vya siasa kwenye mkoa au wilaya ya kipolisi. Afisa huyo wa ngazi za juu (Mkoani asiwe chini ya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi na Wilayani si chini ya Mrakibu Msaidizi wa Polisi) ndiye atakuwa ni ni kiungo kati ya vyama vya siasa na jeshi la polisi katika eneo lake na ndio atawajibika kusimamia masuala ya ulinzi na usalama katika eneo lake hili na kwa kwa kushirikiana na Mkuu wa Polisi wa eneo atawajibika kwa yote yanayotokea au kupaswa kutokea kuhusiana na ulinzi na usalama wa mambo ya kisiasa mkoani.


Mwisho
Haki ya kujilinda ni miongoni mwa haki za msingi kabisa za binadamu ambazo zinatokana na mtu kuwa binadamu na haziwezi kuondolewa au kufutwa na chombo chochote. Ni haki ambayo mwanadamu anayo kwa kuzaliwa kwake. Haki hii kwa kadiri tunavyokua tunaiacha kwenye vyombo mbalimbali lakini mwisho wa siku bado ni haki yetu ya msingi kama binadamu. Mwanadamu anaposhambuliwa ana haki ya kujikinga kukinga maisha yake na mali yake; na kama ni familia yake inashambuliwa ana haki ya kulinda familia yake. Huwezi kumwambia mtu kuwa akipigwa ainame na kukubali kipigo bila kujilinda.


Haki hii ni tofauti na haki ya kujitetea au kulipiza kisasi – japo ni haki zinazoendana pamoja katika ile haki ya msingi ya kutokudhulumiwa. Haki ya kujilinda ni haki ambayo mtu si lazima alipe kisasi lakini ni haki ya kuzuia kutendewa vibaya. Hii ndiyo sababu watu wamejenga kuta kwenye nyumba zao, wameweka vyombo vya ulinzi na kuajiri walinzi. Wote hawa wanatumia haki yao ya kujilinda bila kulazimika kulipa kisasi. CHADEMA kama chama cha siasa ambacho tayari kimeshadhurika mara kadhaa sasa na kwa niaba ya wanachama wake kimeamua kutoa mafunzo ya ukakamavu na kujilinda; wanatumia haki hii ya msingi.


Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama na wale wote wanaobeza wanahitaji kutafakari upya kama wao wangekuwa upande wa pili kama wasingetafuta mbinu ya kujilinda. Kama wale watu waliowekwa kutoa ulinzi ndio hao hao wanaoharibu ulinzi utakuwa ni ujinga wa hali ya juu kuwategemea. Bila mabadiliko ya msingi ya mfumo na utendaji wa jeshi la polisi katika mazingira ya vyama vingi vya siasa ni vigumu kwa chama cha upinzani kama CHADEMA kuweka maisha yake na maisha ya viongozi wake mikononi mwa chombo hicho. Ni wajibu na ni haki kwa wao kufikiri namna ya kujilinda na kulinda maslahi yake. Hili halihitaji baraka kutoka CCM, Ikulu, au Polisi.
Na kama nilivyosema, ni jambo ambalo limechelewa.


Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com