Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingiza (NEMC) linakusudia
kubomoa hoteli ya Royal Sunset Beach mali ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
salaam Willson Kabwe kutokana na kujenga ndani ya eneo la mita 60 kutoka Ziwa
Victoria kinyume na sheria ya usimamizi wa Mazingira kifungu cha 57 pia kumtoza
faini ya Sh10 milioni.
Mbali na hatua hiyo pia NEMC inaweza kuwatia mbaroni watu
wawili ambao ni Wakurugenzi wa Taasisi zisizo za Kiserikali (NGO) kutokana na
kudaiwa kughushi mihuri, nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa vyeti
bandia vya Tathimini ya Mazingira (EIA) kwa makampuni ya mane ya Jijini Mwanza
na kujipatia fedha kinyume cha sheria.
Mwanasheria wa NEMC Heche Suguta akieleza |
Akizungumza na Waandishi wa habari jana Mwanasheria wa NEMC,
Manchare Heche Suguta alisema watu hao wamekamatwa baada ya kuwekewa mtego na
kutokana na kubainika kuwa walitoa vyeti vya Tathimini ya Mazingira kwa
makampuni ya Bibiti Oil (T) ltd, Nyanza Road Works Ltd, Wang Hill Hotel pamoja
na Brichand Oil Ltd kwa kutozwa kati kiasi cha Dola za Kimarekani 10,000.
Suguta alisema kwamba Vyeti hivyo ambavyo ni Bandia
vilivyotolewa na Mwanza Environment and Conservation of Nature (MEC) pamoja na
Mwanza Region Environment Conservation zote za jijini Mwanza na kubainisha kuwa
wahusika wake wametiwa mbaroni baada ya kuwekewa mtego na maofisa wa NEMC kama
wateja waliokuwa wakihitaji cheti na kukubaliana nao kutoa cheti kwa Sh5
milioni.
“Kawaida vyeti hivi
hutolewa na kusainiwa na waziri na wala siyo NGO, lakini wao wamekuwa
wakijifanya ni maafisa wetu na kukagua viwanda ama Hetali zilizojengwa ndani ya
maeneo ya Mito, Vyanzo vya maji na ndani ya eneo la Mita 60 kutoka ziwani na
hivyo kujipatia fedha kwa udanganyifu,” alieleza na kuongeza kuwa NGO hizo
mbili zimefungiwa kuendelea na shughuli zake..
Alisema ofisi yake kwa sasa ambao imeunda Kitengo cha Polisi
wa Mazingira kinachosimamiwa na Afisa wa wanaoshughulika na Mazingira kutoka
Jeshi la Polisi, ameanza msako na kwamba watawakamata wale wote wenye vyeti
Bandia vya Usimamizi wa Mazingira ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale
wote waliojenga kinyume cha sheria kwa kuwavunjia nyumba zao.
Alisema vyeti hivyo hutolewa na Waziri anayehusika na
Mazingira na kusainiwa naye lakini hivyo vilikuwa vikitengenezwa na NGO hizo na
kutolewa kwa Makampuni hayo jambo ambalo alisema ni kosa na kuwataka wale wote
wenye vyeti bandia kuvisalimisha katika ofisi zao ikiwa ni pamoja na wale
wanaohitaji pia.
Aidha katika zoezi la kuwachukulia hatua waliojenga nyumba
katika maeneo ya fuko za Ziwa Victoria, NEMC tayari inakusudia kubomoa Hoteli
ya Royal Sunset Beach inayomilikiwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza
na sasa Jiji la Dar es salaam.
“Tayari tumeshamwangia Barua Julai 10, tukimtaka kubomoa
mwenyewe eneo la Hoteli yake ambalo lipo ndani ya MIta 60 ikiwa ni pamoja na
kulipa Faini ya Sh10 milioni kwa kutiririsha maji ndani ya ziwa Victoria,”
alieleza na kubainisha kwamba iwapo atashindwa kubomoa NEMC itabomoa yenyewe na
kumtoza gharama zake.
Akizungumza na Gazeti hili kwa njia ya Simu, Mkurugenzi wa
Jiji la Dar es salaam Wilison Kabwe alieleza kwamba amejenga kwa mujibu wa Sheria na kubainisha
kwamba inaruhusu kujenga vitu ambavyo ‘water related activity’ pamoja na
Majengo ya Muda badala ya kudumu.
“Sheria ina niruhusu kujenga majengo ya muda, miundombinu
yote pale Hotalini siyo ya kudumu ni ya muda. Ninavyo vibali vingine
vinavyoniruhusu kujenga,” alieleza Kabwe.
Hata hivyo mwanasheria wa NEMC alisema sheria ipo wazi na
kubainisha kwamba Hoteli hiyo imejenga Majengo ya Kudumu na kwamba
walichomwagiza katika barua yao ni kumtaka avunge eneo la Mita 60 kutoka ndani
ya Ziwa Victoria.
No comments:
Post a Comment