Search This Blog

Saturday, July 13, 2013

Kwa heri wasomaji wangu mie nimeamua kujinyonga

Na Nyaronyo Mwita Kicheere
Mambo mengi yamefanyika nchi hii nikayapuuzia lakini hili la juzi limezidi kipimo nami siwezi kulivumilia kwa hiyo nitajinyonga tu ili kuondoa udhia.
Siko tayari kuendelea kutazama upuuzi huu, ushenzi huu, upumbavu huu, uhuni huu, uhayawani huu, umbumbumbu huu na unyang’au huu uliopindukia wa askari wetu kwenda Mtwara kupiga Wamakonde na kazi ya ulinzi wa ikulu yetu wakawaachia maaskari wa Marekani.
Nazungumzia kitendo cha askari wa Marekani kumsimamisha Waziri wetu wa Uwezekezaji, Bibi Mary Nagu, na kumkagua kabla haijaingia ikulu yetu ya Tanzania anakofanyia kazi rais wetu mpendwa kitendo ambacho kimenifanya niamue kujinyonga siku yoyote kuanzia leo.
Rais Baraka Obama
Nasema siwezi kukivumilia kitendo cha kihayawani kama hiki cha maaskari wa mabeberu wa Marekani kuja Tanzania kusimamia ulinzi wa Kilimanjaro Hotel alikolala rais wao Barack Obama na kufunga barabara ya Kivukoni kuzuia wakazi wa Kigamboni kwenda au kurudi kutoka mjini.
Yaani watu nchini mwetu tusiende mjini kununua nyama, tule mlenda na kisamvu eti kwa sababu Obama kalala Kilimanjaro Hoteli? Tunazuiwa kutembea barabarani nchini mwetu eti kwa sababu Wamarekani hawataki tupite karibu na alipo Rais wao?
Kitendo cha askari wa Marekani tena ambaye hana hata cheo cha ukoplo kumkagua waziri wetu, nchini mwetu, karibu na ikulu yetu, mbele ya maaskari wetu hakivumiliki na ndiyo maana nimeamua kujinyonga kwishilia mbali.
Nimeambiwa mawaziri wetu waliokaguliwa na maaskari wa Marekani nchini kwetu, wengine wakati wanakwenda ikulu yetu, kuhudhuria dhifa ya taifa iliyoandaliwa na Rais wetu, Jakaya Kikwete, kwa heshima ya mgeni wake, Rais wa Marekani Barack Obama, ni wengi na kwamba hakuna hata mmoja aliyekasirikia jambo hilo!
Wewe utavumilia kuwaona askari wenu wanapokea amri kutoka kwa wageni ndani ya nchi yenu? Eti askari private wa Marekani anatoa amri kwa askari wa Tanzania wenye vyeo mabegani? Sivumilii mimi kitendo hiki, bora nife kwa kamba ya katani.
Nimeshanunua kamba ya ukonge nimeificha mbali ili mke wangu Maritina na wanangu Nyagone, Mwita, Matinde, Robi, Tumaini na Bhoke wasije wakaiona na kuitilia mashaka wakaikata au kuichoma na kunizuia kujinyonga.
Miaka 50 baada ya uhuru mawaziri wetu wanashikwashikwa na Wamarekani wasiokuwa na vyeo begani wala ukoplo tu eti kwa sababu hawatuamini na wana mashaka na usalama wa Rais wao nchini, kwani ni lazima Obama aje kwetu Tanzania?
Askari wa Marekani wanawalazimisha Watanzania Waislamu kufungua mabegi yao na wanayanusisha na mbwa eti kuona kama kuna mabomu ndani yake! Laanakum yeyote aliyetoa amri mbwa wa Marekani kunusa nguo za dada zetu wawe makatoliki au Waislamu.
Kwani Wakenya ambao hawakutembelewa na Obama wamepungua nini? Kwa nini in the first place ziara za kipuuzi kama hizi ziandaliwe?
Kwani ni lazima tukubali kudhalilika mbele ya dunia nzima? Eti Obama ni rais wa dunia? So what? Kwani ni sisi tuliowatuma Wamarekani kuongopea dunia kuwa Saddam Hussein wa Iraq ana silaha za maangamizi na kumvamia mpaka leo wamejitengenezea maadui kila mahali?
Eti Wamarekani wana pesa, ni matajiri na wana nguvu za kijeshi! Kwa hiyo? Tudhalilike tu mbele ya walimwengu wote ili kumlinda Obama? Ni nani hasa aliyekubali mambo yooooote haya ya kihuni yafanyike na kutuondolea utu wetu ili kumfurahisha Obama?
Wallahi mie jua la kesho sitaliona. Mimi nitajinyonga tu nipishilie mbali wapuuzi waendeleze upuuzi wao. Siwezi kukubali upuuzi huu tunaofanyiwa Watanzania eti kwa sababu ya umaskini wetu, unyonge wetu, udhaifu wetu na upole wetu wa kipuuzi wa kufurahia ziara za kutupuuza.
Nasema haya huku nikijua fika kwamba kuna amri ya Waziri Mkuu wetu, Mizengo Pinda, inayowataka Polisi kutupiga kama tukikaidi jambo, nami nakaidi waziwazi jambo hili la serikali yetu kuwapeleka askari wetu Kusini kuwapiga Wamakonde, Wamwera, Wamakua na Wayao na kuwaacha skari wa Marekani wanawakagua wananchi Dar.
Bwana Mizengo Pinda usijihangaishe kutuma Polisi kuja kunipiga kwa kukaidi uhuni huu, upuuzi huu na uhayawani huu kwa sababu Polisi wako hawatanikuta badala yake watakuta kaburi langu. Tumechoka sisi raia kuliko mlivyochoka nyie serikali hadi ulinzi wa nchi mnawaachia wageni.
Nimekereka sana na sasa nasema nisilotaka kusema. Askari wa Marekani kanishika matako mimi eti ananikagua. Kweli mie mzee wa Kikurya nashikwa matako na haya majitu yaliyozoea kulambana madume kwa madume na majike kwa majike! Kweli ninayo heshima ya kuishi mie? Hapana najinyonga kesho.
Na hili silo pekee linalonifanya niamue kujinyonga. Yapo mengi ikiwa pamoja na hili lililoandikwa kwenye mtandao na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe, kwamba kampuni maarufu nchini ya mawakili ya Rex Attorneys eti ilithibitisha mkataba wa Dowans ili kampuni hiyo ipewe mkopo.
 
Kwa mujibu wa maelezo ya Zitto mtandaoni ni kwamba Novemba 2007 kampuni ya Dowans ilikwenda kukopa benki ya Stanbic dola za Marekani milioni 20 na kwamba benki hiyo ilipotaka ushauri wa kisheria kutoka kampuni ya REX Attorneys iliambiwa kuwa mkataba kati ya Tanesco na Dowans ni mzuri na uko sawasawa kabisa wapeni mkopo.
Kwamba July/August 2008 Tanesco waliiendea kampuni hiyo ya mawakili ya REX Attorneys kuomba ushauri wa kisheria kuhusu mkataba wa Dowans na Tanesco safari hii REX Arttorneys wakasema mkataba huo ni mbovu na haufai kabisa uuvunjeni kwa sababu hauna uhalali wowote. Tanesco wakaitika wakauvunja mkataba wake na Dowans.
 
Eti Dowans walipokwenda mahakamani kupinga kuvunjwa mkataba wao na Tanesco ukatolewa uamuzi wa kuiajiri kampuni maarufu ileile ya REX Attorneys kuiwakilisha Tanesco kwenye kesi ambapo ilishindwa kesi zote katika hatua zote!
 
Sasa mimi nitavumilia namna gani, eti niendelee kuishi huku naendelea kuona eti mtu kutoka REX Attorneys anateuliwa kuwa balozi wetu nje ya nchi? Kwa uendaji gani bora? Kwa manufaa ya nani? Na kwa kutaka kumridhisha nani? Mke wangu, wanangu na majirani kwa herini siwezi kuvumilia upuuzi huu.
 
Kama nilivumilia ya EPA, Deep Green, Meremeta, Twin Tower na Alex Stewart Assayers sipo tayari kuvumilia kushikwa matako na wageni wakati tuna polisi hata kama wana tuhuma za kurushia wapinzani mabomu na askari jeshi hata kama ni mabingwa wa kupiga raia basi angalhinda kesi walipwe dolaau wangeachwa ha[a dar wachache watukague siyo FBI, CIA na wahini wengine wa kigeni.
 
Kwa maelezo ya Zitto REX walilipwa dola za Marekani milioni 8 na Dowans walipwe dola za Marekani milioni 94! Bora nikafe kwa kamba ya mkonge kuliko kushuhudia haya tena katika wakati ambao vyombo vyetu vya dola vinapiga raia kwa amri ya Waziri Mkuu nasi wa dar tusiopigika tunashikwa matako na wageni wanaotukagua!
 
Mwisho mambo haya ya kihuni ya mabomu kulipuka mara kwa mara, askari kupiga raia Mtwara wakiacha askari wa kigeni wakikagua raia wetu, nchini kwetu, yanafanyika miaka 50 baada ya uhuru na baada ya majenerali Serakikya, Twalipo, Musuguri, Kyaro, Mboma na Waitara waondoke jeshini. Kwa nini? Wangekuwapo wangeruhusu tushikwe matako na Wamarekani wakitukagua? Kwa herini, najinyonga kesho, tukutane ahera.

No comments:

Post a Comment