Wapiganaji saba na wengine 14 walijeruhiwa Jumamosi iliyopita.
Askari wa JWT ambao ni Majeruhi Dafur |
Gazeti hili limepata majina ya askari hao
waliofariki kutoka vyanzo tofauti lakini limeshindwa kuwataja leo kwa
kuwa JWTZ kupitia kwa msemaji wake, Kanali Kapambala Mgawe limesisitiza
kuwa haliwezi kutangaza majina hayo hadi litakapowasiliana na jamaa za
askari waliofariki.
Tukio lilivyotokea
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, askari
polisi huyo anayefanya kazi katika Mji wa Nyala uliopo Darfur, alisema
mauaji hayo yalitokea wakati askari hao walipokuwa wakifuatilia magari
yao yaliyokuwa yameporwa na kundi mojawapo la waasi.
Usalama katika Mji wa Nyala ambao ndiyo mkubwa
zaidi katika eneo la Darfur, umekuwa mdogo katika siku za hivi karibuni.
“Wale wanajeshi walikuwa doria ya kawaida, ila kama wiki moja iliyopita
waasi walivamia tena doria ya wanajeshi wetu na kupora magari manne
bila kuua mtu.
“Siku ya mauaji hayo wanajeshi wetu wakiwa tena
katika doria waliyaona yale magari yaliyoporwa kwa mbali yamepaki,
waliyafuatilia, walipokaribia kumbe ulikuwa mtego, wakashambuliwa,”
alisema askari huyo na kuongeza: “Mauaji hayo yametokea takriban
kilometa 70 kutoka katika kambi niliyopo mimi, lakini wote tupo eneo la
kusini na hiyo kambi ya Korabeche inaongozwa na jeshi letu.”
Tofauti na chanzo chetu cha habari huko Darfur,
Kanali Mgawe alisema wanajeshi hao walishambuliwa walipokuwa kwenye
msafara wa kusindikiza walinzi wa amani.
Makundi yanayopambana
Askari huyo aliyeko Darfur alisema: “Makundi
yanayopambana huku yapo mengi ila makubwa yapo kama matano. Kuna moja
linaitwa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan (SPLA), ambalo limegawanyika
katika makundi mawili pia kuna mengine kama JEM, Janjaweed na
mengineyo.”
Akizungumzia mshtuko walioupata baada ya mauaji
hayo, askari huyo alisema wafanyakazi wote wanaohusika na ulinzi wa
amani wamepatwa na ganzi... “Huku kwa kweli hali imekuwa chungu, tangu
askari hao wauawe hali haitabiriki kabisa, tupo nje hapa (hospitali
walimohifadhiwa), tunasubiri uhakika.”
“Hawa jamaa (waasi), wamesheheni silaha na wana
vifaa vya kisasa kiasi kwamba hata ndugu zetu walizidiwa kutokana na
wenzao kuwa na silaha nzito, nikija Tanzania nitakuonyesha picha za
mapambano yao,” alisema.
Akizungumzia kazi ambazo polisi wanazifanya huko, alisema
hawaruhusiwi kushika silaha, bali kuwashirikisha wananchi katika masuala
ya amani.
“Sisi majukumu yetu ni kuungana na jamii na
kuwafundisha masuala mbalimbali, hivyo sisi tunawasiliana moja kwa moja
na wananchi waliopoteza makazi kisha tunaandaa taarifa. Haturuhusiwi
kushika silaha, wanajeshi wao wanatulinda na kusimamia usalama na
kutusindikiza wakati wa doria,” alisema.
“Huku hali ya usalama haitabiriki. Mpaka sokoni tunakwenda chini ya ulinzi.”
Kauli ya JWTZ
Akizungumza kwa simu jana, Kanali Mgawe alikanusha
uvumi wa majina yaliyosambaa mitandaoni huku akisema kwa utaratibu
uliopo, jeshi haliwezi kutangaza majina hayo hadi ndugu
watakapotaarifiwa. “Hayo majina yanayotajwa kwenye mitandao ni ya uongo.
Kwa sasa mimi sijaletewa majina na utaratibu uliopo ni hadi ‘next of
kin’ (ndugu) wao wajulishwe kwanza,” alidai Kanali Mgawe.
Hata hivyo, alisema Tanzania imewasilisha maombi
ya kubadilisha kanuni za kulinda amani ikitaka kuruhusiwa kujihami kwa
silaha za moto pale wanajeshi wake wanaposhambuliwa kwa kutumia kanuni
namba saba ya Sheria za Majeshi ya Kulinda Amani.
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/1916496/-/13b9r33/-/index.html
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/1916496/-/13b9r33/-/index.html
No comments:
Post a Comment