Na M. M. Mwanakijiji
WATAWALA huweza kutawala wapendavyo mpaka pale wananchi wanapoamua kuuliza maswali. Utawala wa kiimla unaweza kujisimika kwa muda mrefu madarakani kwa kadiri ya kwamba maswali na kupinga (dissent) kusivyo ruhusiwa. Kwa muda mrefu Ulaya ilikuwa katika wimbi la kutumia imani kuelezea mambo yote mpaka pale walipotokea watu walioanza kuuliza maswali na kutafuta majibu wao wenyewe wakasababisha kile zama za Enlightenment.
Zama hizo za kujifunza zaidi na kufahamu zaid zilisababisha watu kufanya tafiti kwa kutumia njia za sayansi, kuuliza maswali kwenye imani za dini, na kutoa mapendekezo kwa kutumia akili (reason) badaa ya imani au ushirikina. Lakini yote yalianza kwa watu kuamua kuuliza maswali na kutafuta majibu na kubadilishana mawazo. Matokeo ya kubadilishana huku kifikra kulikuwa ni Azimio la Ufaransa Juu ya Haki za Raia na za Binadamu, Azimio la Uhuru la Marekani n.k.
Watawaliwa wasiouliza maswali watawala hutawaliwa bila kuulizwa na watawala! Lakini hoja siyo kuuliza tu bali pia kukataa majibu (dissent). Mojawapo na naweza kusema alama kuu ya demokrasia ni kupinga (dissent). Mtawala anapotoa jibu lisiloingia akilini au lisilo na ukweli raia au mwananchi anajikuta na jukumu la ama kukataa au kukubali. Anaweza akakataa kimoyo moyo bila mtawala kujua lakini kama mtawala hajui amekataliwa kukataliwa huko kuna maana gani kama raia yule yule anafanya kile ambacho moyoni amekikataa? Kumbe kukataa ni lazima kujulikane kwa watawala!
Mfano mzuri ambao unaweza kufaa hapa kwa kiasi chake ni jibu la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe kuhusu suala la usafirishaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar. Baada ya majibu yaliyotolewa na watawala ambayo mengine yalikuwa ni kejeli na dhihaka kwa wananchi Zitto aliamua kuwaambia kuwa majibu yao hayana mashiko. Tunaweza kusema Zitto aliamua kuonesha dissent. Kina cha kupinga huko japo si kirefu sana lakini kimsingi ameonesha kukataa majibu ya watawala! Lakini jibu lake kwa kiasi ni jibu la kisomi lenye kutaka kushawishi hoja za kisomi. Hili ni zuri kwa technocrats lakini si jibu zuri kuelezea kinachoendelea. Binafsi ningependa angefanya zaidi kama alivyofanya kwenye tamko lake la kwanza baada ya maandamano (haikuripotiwa sana na vyombo vya habari wakati ule).
Zitto katika lile tamko alisema hivi (Kitu ambacho na mimi nimekuwa nikipigia sana debe CDM wasimamie lakini wanasitasita kama chama) "Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona. Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa."
Lakini kuna mfano mwingine mzuri wa kulionesha hili. Ukiniuliza mimi ni kitu gani ni janga kubwa katika Tanzania na linasababisha kuendelea kwa Umaskini nitajibu pasi ya shaka ni elimu mbovu. Kwa muda mrefu tumeshuhudia elimu yetu ikivurugika licha ya kuongezeka kwa shule na vyuo mbalimbali. Bado ubora wa elimu yetu unatuletea matatizo zaidi na zaidi. Inapofika taifa linakuwa na Waziri asiyejua Muungano wa Tanzania ulitokana na nini basi tuna tatizo kubwa sana. Bahati mbaya hatujaona dissent ya kutosha katika hili. Walimu wetu wanakubali majibu ya serikali, wazazi wanakubali, wanasiasa wanakubali na siku zinakwenda miaka inapita wanasubiri matokeo mengine. Imefika mahali sasa ili angalau kuonesha elimu inaboresheka watawala wanajaribu kubadili vigezo vya kupasi!
Lakini jingine ambalo ningependa msomaji wangu ulifirikirie ni hili: Kwanini unalazimika kuwa na line zaidi ya moja ya simu kwa matumizi binafsi? Kwanini kwa mfano utakuta karibu kila Mtanzania mwenye simu ya mkono ana namba angalau mbili za makampuni tofauti? Mtu utamkuta ana Zantel na Voda, Airtel au Sasatel. Kwanini watu wanalazimika kuwa na line zaidi ya moja ambazo anazilipia na mtu huyo labda yuko kwenye mji mmoja zaidi si kwamba anasafiri sana kwenda mahali nje ya Tanzania? Jibu linalotolewa mara nyingi ni kuwa "ni bei rahisi kupiga simu ndani ya mtandao mmoja kwani ukipiga nje ya mtandao ni gharama ya juu"? Na wapo watu wanakubali jibu hili kana kwamba limeandikwa kwenye ubao wa moto.
Je yawezekana yote haya ambayo tunayalalamikia kila siku ni kutokana na kushindwa kwa sera za CCM? sijasema kushindwa kutekelezeka bali sera zenyewe zimeshindwa?
Nani ataonesha kupinga?
Nitafute Facebook: http://www.facebook.com/mwanakijiji
No comments:
Post a Comment