Mabaki ya Mzoga wa tembo aliouawa hifadhi ya Buligi |
Mwaka
mzima uliopita, 2012, ulijaa habari za kukamatwa kwa shehena za meno ya
Tembo kutoka Tanzania huko HongKong zikielekea China. Mwezi Disemba
shehena yenye tani 1.3 ya meno ya Tembo iliyofichwa kwenye magunia ya
Alizeti ilikamatwa na Maafisa wa Forodha wa HongKong. Shehena hii
ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni moja na nusu. Wiki
mbili kabla ya hapo takribani tani nne za meno ya Tembo zilikamatwa huko
huko HongKong. Kwa matukio haya mawili, hawa ni sawa na Tembo 900
waliouwawa.
Mwezi
huo huo wa Desemba, 2012 Polisi mkoani Arusha walikamata nyara nyingi
za Serikali katika eneo la Kisongo. Nyara hizi ni pamoja na ngozi za
Simba na wanyama wengine, pembe za ndovu na wanyama wengine na vichwa
vya wanyama. Nyara hizi zilikuwa tayari kwa kuuzwa nje ya Nchi. Mkoani
Katavi walikamatwa majangili kadhaa na kuachiwa huru kwa amri kutoka juu
kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa wanyama pori.
Ujangili
umeshamiri sana na kwa kasi ya kutisha. Takwimu za Serikali zinaonyesha
kuwa mwaka 2010 jumla ya Tembo 10,000 waliuwawa hapa Tanzania peke
yake. Hii ni sawa na Tembo 37 kila siku. Hali imekuwa mbaya zaidi mwaka
2012 ambapo jumla ya Tembo 23,000 waliuwawa sawa na wastani wa Tembo 63
kila siku. Kwa hesabu ya haraka, kutokana na kasi hii ya ujangili,
ifikapo mwaka 2017/2018 Tanzania haitakuwa na Tembo hata mmoja. Hivi
sasa Tanzania ina Tembo kati ya 150,000 na 170,000. Maafisa wengine wa
Wanyama pori wanasema Tembo wanafika 250,000 na nusu ya Tembo hao wapo
pori la Selous kusini mwa Tanzania. Sote tuna wajibu wa kulinda urithi
huu tulioachiwa na MwenyeziMungu.
Kasi
ya ujangili imechangiwa na mambo mengi sana lakini kubwa ni kukua kwa
uchumi wa China na nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa Asia. Kwa hiyo
takribani nchi zote za Afrika zenye Tembo zinaathirika na Biashara hii
ya Pembe za Ndovu. Tanzania, Kongo-Kinshasa na Msumbiji zipo kwenye
hatari zaidi ya Tembo wake wote kumalizika kutokana na nguvu kubwa
waliyonayo wafanyabiashara haramu wa Pembe za Ndovu. Kenya na Nigeria
inasemekana jumla ya Tembo 25,000 waliuwawa mwaka 2011 peke yake.
Inasemekana kuwa kuongezeka kwa wafanyabiashara wengi kutoka China na
hivyo wafanyakazi kwenye makampuni ya Kichina kuzagaa Afrika kunachangia
kwa kiasi kikubwa sana Ujangili na biashara hii haramu.
Pembe za ndovu zilizokamatwa katika operesheni dhidi ya biashara ya magendo huko Hong Kong zikioneshwa kwenye mkutano wa vyombo vya habari |
Mtandao
wa Ujangili ni mpana na wenye nguvu sana za pesa, kisiasa na kimamlaka.
Mtandao huu huanzia chini kabisa kwenye Mapori na Hifadhi ambapo wauaji
ni watu masikini wa vijijini na wengine hutumia magobole tu. Hawa
hulipwa kwa kuua tu. Wakataji nao huingia hapo na kukata meno na kuandaa
usafiri ambao hufanywa wakati mwingine na magari ya Serikali. Hivi
karibuni gari za polisi, muhimbili na hata magari ya viongozi wa dini
yamekamatwa na meno ya Tembo huko mkoani Iringa. Baada ya kusafirishwa
na kufikishwa maeneo ya mijini hufungwa na kusafirishwa kupitia bandari
ya Dar es Salaam. Katika mtandao huu kuna watu wa Vijijini, masikini
ambao hutumia ujangili kama sehemu ya kupata kipato. Pia kuna watu wa
kati kama maafisa wa Polisi, maafisa wa wanyama pori, madereva wa magari
ya Serikali wenye tamaa tu kuongeza kipato. Juu kabisa kuna
wafanyabiashara wakubwa na inasemekana pia wanasiasa ambao hulinda
biashara hii.
Nina karibia kumaliza kitabu cha kurasa 301 kiitwacho “Killing for Profit: Exposing the illegal Rhino Horn Trade” ambacho kimeandikwa na Mwandishi wa habari Julian Rademeyer wa Afrika Kusini.
Kitabu hiki ni cha uchunguzi ambapo mwandishi amechunguza mtandao mzima
wa biashara haramu ya meno ya Faru. Mwandishi anasema, kule nchi za
Kusini Mashariki mwa Asia kama Vietnam, meno ya Tembo na Meno ya Faru
yana bei kubwa kuliko dhahabu na madawa ya kulevya. Anasema Biashara hii
imejaa tamaa za mali na rushwa ya kiwango cha juu. Mwandishi anaonyesha
kwa ushahidi namna biashara hii ilivyotumika kuendeleza vita Msumbiji
na Angola kwa nguvu ya Serikali ya Makaburu. Hata baada ya ukaburu
kuisha anaonyesha namna ambavyo wanasiasa watawala wanaendeleza biashara
hii na kupata fedha za kampeni.
Katika
kitabu hiki Mwandishi anathibitisha kuwa Meno ya Tembo na Meno ya Faru
huko Asia hutumika kama mapambo kwa kutengeneza bangili zenye bei aghali
na kwa matajiri na mapambo mengine kwenye mikufu, herein nk. Hata hivyo
anasema meno haya hutumika kama dawa na hasa dawa za kuongeza nguvu za
kiume kwa wanaume na hivyo kusababisha bei yake kuwa kubwa sana. Jinsi
uchumi wa Mataifa hayo unavyokuwa na kuongeza watu wa tabaka la kati,
ndivyo mahitaji wa Meno ya Tembo na Faru yanaongezeka. Mwandishi
anaonyesha kwamba mwaka 1960 kulikuwa na Faru 100,000 katika nchi za
Zimbabwe na Afrika Kusini. Hivi sasa kuna Faru 2400 tu. Nadhani ni
muhimu kupata pia takwimu za Tanzania kuonyesha hali upande wetu ipoje.
Watafiti waliofanya tafiti kwenye eneo hili watujuze.
Jambo
moja lipo wazi hapa Tanzania ni kwamba maeneo ya Hifadhi za Taifa
takwimu za Ujangili ni chache kuliko maeneo ya mapori ya Akiba kama
Selous. Hii inatokana na ukweli kwamba maeneo ya mapori ya Akiba uwezo
wan chi kulinda wanyama ni mdogo sana maana hakuna askari wa kutosha na
waliopo maslahi yao ni madogo sana. Hivyo moja ya pendekezo la dhati
kabisa ni kuimarisha ulinzi kwenye mapori ya Akiba. Pori kama Selous
ambalo ni urithi wa Dunia ni vema liundiwe mamlaka yake (Selous Games
Authority) kama ilivyo Mamlaka ya Ngorongoro. Mapori mengine yawekwe
chini ya wakala wa Serikali na yawezeshwe kutokana na mapato ya uwindaji
wa Kitalii. Lazima kutoa motisha ya kutosha kwa Askari wa wanyama pori
na pia kutoa adhabu kali sana kwa askari atakayejihusisha na ujangili.
Hata
hivyo, wataalamu wa wanyamapori wanasema ‘kuua majangili hakuleti
mafanikio yeyote. Kuna watu wengi sana masikini wapo tayari kuingia kuua
Tembo ili wapate pesa kidogo. Hata ukiua mamia yao, hawatamalizika.
Suluhisho pekee ni kuua soko la biashara hii haramu’. Soko hili litakufa
kwa kuusambaratisha mtandao wa ujangili kwa kuanzia na wafanyabiashara
wakubwa. Hii ndio opresheni. Operesheni linda Tembo. Sasa ianze.
Tafuta
namba ya simu ya Mbunge wako au mbunge yeyote mwandikie “nataka ulinde
Tembo wetu #OperesheniLindaTembo kwa kuihoji na kuiwajibisha Serikali”.
Mabadiliko ni Mimi, Ni wewe, Ni sisi. Tumia simu yako kutaka viongozi
wako wawajibike. Ni wajibu wetu kikatiba kulinda urithi wetu.
No comments:
Post a Comment