Taarifa
za kuuawa kwa askari polisi wawili zimezidi kuchukua sura mpya wilayani
Karagwe baada ya wananchi kuanza kutoboa unaodaiwa kuwa ukweli wa tukio
hilo ambao wanadai umefichwa kwa makusudi na badala yake kuwatolea
lawama wananchi.
Ukweli unaoelezwa ni huu: Mtu mmoja (Raymond) wa kijiji cha Rugu (iko wilayani karagwe) alikuwa na
meno ya tembo; aliamua kwenda maeneo ya Benaco (iko wilayani Ngara) kutafuta
wanunuzi wa Meno ya Tembo na huko aliwapata watu wawili (Abubakari na Geofrey).
Baada ya makubaliano ya kulipwa shs 12 milioni wale wanunuzi
walimweleza kuwa kwa kuwa watakwenda usiku na njiani kuna pori la Kimisi
watakwenda na mtu wao mwenye bunduki ambaye huwa anawalinda mara kwa mara.
Walipofika Rugu wakauona mzigo, wakaupima na kukuta kilo walizokubaliana ndivyo
zilivyo.
Mzigo ulipakiwa kwenye gari lao; jamaa hao wakataka kuondoka
bila kulipa. Mwenye mali alipouliza mbona hawampi hela yake alijibiwa kuwa
'sisi ni polisi na haya meno ya tembo ni nyara za serilkali, ukileta fujo
tutakukamata!'
Kwa kuwa walikuwa na bunduki jamaa aliogopa lakini
alijitahidi kupambana na kuvunja kioo cha mbele cha gari hilo. Gari
lilipoondoka na mzigo jamaa akapiga simu kwa watu walio kwenye stesheni ndogo
ambayo ilikuwa lazima gari hilo lipitie akiwaeleza kuwa wamevamiwa na majambazi
lakini wamepambana nao na kupasua kioo cha gari, hivyo wajitahidi kulizuia
lisipite.
Raia hao walipanga mawe makubwa barabarani na mara gari hilo
likaja - kioo kimepasuliwa na halina namba. Gari liliposimama raia wakaanza
kuwahoji wanakotoka na wanakokwenda na walifuata nini.
Ikabidi kichapo kitembee kidogo. Jamaa kuona kichapo kinazidi
ikabidi waseme kuwa wao no polisi na kuna mhalifu walikuwa wamnamfuatilia.
Lakini raia wakaona hao polisi mbona hawawahamu?
Raia waliamua kupiga simu kwa OCS wa kituo cha karibu
(Chanyamisa) akawajibu kuwa hana taarifa zozote na watu hao; wakapiga simu
kituo cha Omukaliro, OCS akawajibu kuwa hana taarifa;. Walipiga simu polisi
wilayani lakini jibu likiuwa ni hilohilo!
Hao Polisi -majambazi kuona hivyo yule aliyekuwa na bunduki
akafyatua risasi hewani raia hawakuogopa wakataka wamkamate, akapiga risasi
nyingine ikampiga kijana mmoja kwenye mkono!. Hapo ndipo raia waliona kuwa
kumbe hawa tukiwalegezea watatuua. Kichapo kikaendelea lakini aliyekuwa na
bunduki alikimbia baada ya kufyatua risasi nyingine. Hao wawili waliobaki
walipigwa hadi kufa!
Raia waliamua kulitia gari moto, wakati likiendelea kuuungua
walifungua kwenye boot na kukuta meno ya tembo baadhi yakiwa yameanza kuungua
kidogo.
Huo ndio unaelezwa kama ukweli baada ya TBC kutangaza wakimkariri
msemaji wa jeshi la Polisi kuwa hao polisi walikuwa wanataka kumkamata mhalifu
na raia wakawaua ili wasimkamate, raia wamechukizwa sana uongo huo.
Ukweli huu umetobolewa na wananchi katika kipindi cha Radio Jana
majira ya saa 3 hadi saa 4:30 Usiku na kituo cha Radio ya kijamii (Radio Fadeco)
iliyoendesha kipindi kwa kuruhusu wananchi kupiga simu kueleza nani alaumiwe
kwa mauaji ya hao polisi?
No comments:
Post a Comment