Mpayukaji wa Msemahovyo
KWA mujibu wa taarifa iliyosomwa na profesa, daktari, shehe,
gwiji, alhaji, kanali, father Njaa Kaya Kiwewe ni kwamba walevi kwenye kaya hii
wamezaliana na kuongezeka sana. Hili ni jambo la kujivunia.
Ni ushahidi kuwa sera ambazo baadhi ya fyatu huziita usanii
na uchakachuaji zimefanikiwa. Kila mtu anamchakachua mwenzake na kuzalisha
vitegemezi iwe halali au haramu. Unakumbuka yale matokeo ya kipimo cha vinasaba
cha DNA?
Kwa wasiojua maana ya DNA ni Deoxyribo-Nucleic Acid. Kipimo
hiki kilionesha kuwa katika ndoa na ndoana watoto wanaozaliwa asilimia zaidi ya
40 ni wa kuchakachua.
Mama anamchakachua baba na baba anachakachua nje sawa na
watawala wanavyochakachua sera. Usishangae siku moja ukiambiwa kuwa kaya yenu
ni kaya ya uchakachuaji.
Chakachua ngoma ya zama zile. Leo si ngoma bali mfumo ambapo
kila kitu kinachakachukuliwa kuanzia kura, elimu, afya hata familia! Mwe!
Msipojifunza na kujirudi mwesha mie simo bahati nzuri.
Kutokana na kuwa na shahada ya juu yaani PhD in Demography
and Chakuazation, leo nataka nifanye uchambuzi wa kina (deep and critical
analysis) juu ya ni kwanini walevi wamezaana na kuongezeka sana. Kuna sababu za
kisayansi ambazo nimezibaini ambazo zimesababisha kuongezeka kwa walevi.
Mosi, mgawo wa umeme. Utafiti uliofanywa na mtaalamu bingwa
na baba ya uchakachuaji unaoshuhudia aitwaye Profesa Alhaj Ally Hossein Mwinyi
ni kwamba watu wanazaliana sana kwenye giza kuliko kwenye mwanga.
Hii inatokana na ukweli kuwa wakati wa mgawo wa umeme watu
hukosa mambo muhimu ya kufanya au fursa ya kujishughulisha kama vile kusoma,
kuangalia taarifa za habari hata kuonekana.
Hivyo, wahusika hujikuta wakiwa na msongo wa mawazo na sononi
kiasi cha kujiburudisha kwa kula tunda lile. Hata kama huwa wahusika hawana nia
au hamu ya kula tunda, mazingira ya kiza huwalazimisha kufanya hivyo.
Umenielewa? Najua wengine watauliza tunda gani. Ni tunda lililo katikati ya
miiba. Kama ni nanasi au ‘whatever please ask me not.’
Sitaki uniulize miswali mingi hadi nikujibu kipuuzi kama Dk
Dugong bin Manatee Ben Willy Makapa aliyewahi kuwatolea watu uvivu kuwa wana
uvivu wa kufikiri asijue naye alikuwa nao hadi akaingizwa majaribuni na
Delillah wake akajimegea Kiwila. Anyways, tuyaache hayo si mwake humu leo
ingawa ujumbe umetua, msg sent au siyo?
Mbali na kuongeza idadi ya walevi, mgawo wa umeme hukuza
uchumi wa kaya kwa kuagiza na kuingiza jenereta nyingi ambazo huuzwa kwa bei
mbaya. Pia jenereta hizi husaidia kutunza mazingira kwa kutoa mimoshi
inayosaidia majani kuota na kusafisha anga. Najua kuna watakaoniona kama chizi.
Kama mgao wa umeme hauzalishi majenereta ambayo ni salama kwa mazingira chizi
ni nani kati yangu na wale wanaosababisha mazingira ya kuwepo madudu haya?
Kutokana na kukua uchumi hasa kwa kutoa ajira kwa
wafanyabiashara wengi wa Kihindi, taifa letu limeweza kuwekeza kwenye huduma
bora za afya ndani na nje. Kwa sasa tuna kile Wazungu huita cutting edge tech
kwenye mahospitali yetu maarufu kama vile Apollo. Hivyo, kuzaana si tatizo.
Huduma za afya zipo kwa wote wenye mshiko na viza ya kwenda India kutibiwa.
Faida nyingine ya mgawo licha ya kuzaliana ni kutoa fursa za
kuweza kuleta makampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ambayo mwisho wa siku
huzalisha dharura ya wizi na kutengeneza pesa nyingi hivyo kuacha baadhi ya
wanene kwenye kaya wakiwa mabilionea. Mara hii mmesahau Richmonduli na Dowans!
Ukosefu wa ajira hivyo kazi inakuwa hiyo hiyo. Usiniulize
hiyo hiyo ipi tafadhali. Ufisadi, watu wanachuma wasipopanda kiasi cha kujiona
matajiri hivyo kuzaliana bila kuogopa chochote wasijue neema yao ni ya muda.
Wakuu wetu kujizalia sana kiasi cha kutufanya tuwaigize. Hebu
waulize wao wana watoto wangapi na mali kiasi gani? Kila mmoja siri yake. Je,
unategemea nini hapa?
Maisha bora kwa wote. Baada ya walevi kungoja maisha bora kwa
wote wasiyaone wameamua kuongezeka ili wale watakaokufa kwa matatizo angalau
waache mbegu nyuma.
Sababu nyingine ya kuongezeka kwa walevi ni matangazo
yanayochochea ngono. Kwa sasa matangazo machafu ndiyo fasheni.
Magazeti ya uchafu yafichwayo kwenye jina la udaku, runinga
zenyewe wendawazimu wanaoitwa watangazaji na matangazo ya kusambaza ukimwi kwa
kisingizio cha kuupinga ndiyo usiseme.
Hili likiunganishwa na sheria kutowashughulikia wanaovunja
maadili ya taifa linafanya hali kuwa mbaya. Hapa hutujagusa wanaowatia mimba
watoto wa shule. Hivi kama dingi anasema wanaopata mimba wakiwa mashuleni ni
matokeo ya kiherehere chao unategemea nini?
Kubariki jinai. Kama halali imegeuzwa haramu na haramu halali
unategemea nini? Kila mtu anaendekeza libeneke akijua kuna siku ataukata kwa
vile kuukata hakuna kizuizi kisheria. Hivyo watu wanajenga kwenye ndoto zao
wakisahau kuwa kuna kubaunzi kwa ndoto na mipango yenyewe.
Ingawa kuzaliana na kuzalishana na kuongezana kwa walevi ni
jambo bora, halikosi kasoro. Baada ya walevi kuona wanaongezeka huku masahibu
yao nayo yakizaliana, wameanza kugombea utajiri. Hamkusikia wale wa kule
Zaainzibaa na Ntwara wakigombea nishati? Hamkuwasikia mawaziri wehu nao
wakichochea kadhia hizi kwa kutoa majibu ya kubabaisha?
Nawakumbuka waishiwa kama vile Billy Mgimwa na Sossy Muongo
wakisia urongo na upupu kuwa walevi wasiwe na wasi wasi kwa vile watawekezwa!
Hakuna aliyenichefua kama Murongo aliyesema eti wamachinga kule Ntwara hawana
sababu ya kudai kufaidi wese kwa vile nao wamekuwa wakifaidi nishati ya
Kihainsi!
Kwani walikuwa wakipewa bure? Mbona kila mlevi anajua magumu
ya kulanguliwa huduma mbovu kuanzia simu, umeme hadi hewa?
Kwa ufupi ni kwamba kama utawala na staili ya kutawala
vitaendelea kuwa hivi hivi, walevi wataongezeka hadi wageuke bomu linalotika.
Wataacha kuwa neema waishie kuwa balaa. Hata hivyo, inatupasa kushangilia
ufanisi huu wa kuzaliana sawa na mabalaa yetu. Nadhani ombaomba wetu wenye suti
wanachekelea kwa vile wamepata sababu ya kwenda kuzurura wakidai wanaomba
njuluku kwa ajili ya walevi huku njuluku zenyewe zikiishia kule Ususio au
Uswisi.
Acha niwahi home kwenda kuzalisha nami! Who cares if at all
what we’ve is but megalomania in the name of polity? Usiniulize tafsiri
No comments:
Post a Comment