Search This Blog

Friday, January 4, 2013

Mtei amtaka Zitto Kabwe asigombee urais 2015

MWASISI wa Chadema, Edwin Mtei amemtaka Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe kumwachia Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa fursa ya kuwania tena urais mwaka 2015 kwa madai kuwa ndiye chaguo la watu kwa sasa.
Kauli hiyo ya Mtei inakuja siku kadhaa  baada ya kuunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwamba Dk Slaa awanie tena  urais katika uchaguzi ujao huku yeye akijiondoa katika orodha ya viongozi watakaowania nafasi hiyo kupitia Chadema.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu Mh Zitto Kabwe(kushoto)akiwa katika picha ya pamoja na Mwasisi wa Chadema Mzee Edwin Mtei .
Akihojiwa na gazeti hili, Mtei alisema Zitto anapaswa kumwachia Dk Slaa apeperushe bendera ya chama hicho katika uchaguzi ujao kwa kuwa ndiye chaguo la wengi.
“Zitto atagombea baada ya Dk Slaa na kwa sasa amwachie katibu mkuu atupeperushie bendera ya chama katika uchaguzi ujao kwani ndiye chaguo la wengi,” alisema Mtei.
Mtei alisema yeye anasimamia msimamo wa Mbowe  na kamati kuu ya chama hicho kuhusu kumpendekeza Dk Slaa kuwania nafasi hiyo.
Alisema kila mmoja ndani ya chama amekuwa na hisia na mawazo tofauti lakini msimamo wake kwa sasa ni kumtaka Dk Slaa awanie nafasi hiyo ya urais na si Zitto. “Kila mmoja na hisia na maoni yake, Dk Slaa ana yake, Freeman na yake hata mimi nina hisia zangu na Slaa ndiye pendekezo langu nataka atupeperushie bendera,” alisema Mtei.
Hata hivyo, Mtei alisema Zitto ana haki ya kuonyesha demokrasia yake ndani ya chama kwa kutangaza kuwania uraisi mwaka 2015 na ndiyo maana halisi ya chama chao.
“Kuonyesha hisia si dhambi, kila mtu ana hisia zake hata yeye (Zitto) ana sababu za kuonyesha hisia zake,” alisema Mtei.
Hata hivyo, alionya kuwa kila mmoja mwenye hisia za kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao anapaswa kusubiri mchakato wa mchujo wa majina utakaofanyika ndani ya chama muda mwafaka ukiwadia.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Siasa/-/1597332/1656632/-/bpadr5z/-/index.html

No comments:

Post a Comment