JENGO la ghorofa 19 lililojengwa karibu na Ikulu ya Dar es
Salaam linadaiwa kuhatarisha maisha ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, UWAZI
limefuatilia kwa umakini.
WALINZI WA OBAMA WADAIWA KUWA CHANZO
Kuna habari kwamba, ujio wa
Rais wa Marekani, Barack Obama nchini Tanzania Julai Mosi, mwaka huu
ndiyo ulioibua mambo mengi juu ya kuwepo kwa jengo hilo kwani maafisa wake wa
usalama walikataza watu kupanda hadi ghorofa ya 19 kwa maelezo kuwa wamegundua
ni hatari kwa maisha ya viongozi, hasa Rais Obama aliyekuwa ikulu na Jakaya Kikwete.
Kikosi cha Majasusi wa Marekani (FBI) waliotangulia nchini
miezi minne kabla ya ujio wa Obama ndiyo walioishtua serikali kwa kuwaambia
watu wa usalama kuwa urefu wa jengo hilo ni hatari kwa ikulu kwa vile maadui
wanaweza kulitumia.
FBI WALITEGA MITAMBO YAO JUU YA JENGO
Uchunguzi unaonesha kwamba, kwa vile FBI waliamini usalama
wa ikulu ni mdogo kutokana na jengo hilo hivyo walilazimika kuweka mitambo yao
juu yake na kuendelea kuwepo hapo kwa saa ishirini na nne kipindi chote cha
ziara ya Obama.
FBI WALIONDOA MAGARI CHINI YA JENGO
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya ikulu vililitonya Uwazi
kuwa, mbali na FBI kuweka mitambo yao ya kiusalama, pia walilazimika kuondoa
magari yote yaliyokuwa yamepaki chini ya jengo hilo na kuitahadharisha serikali
ya Tanzania kuwa makini na ghorofa hilo. Habari zaidi zinasema FBI hao walipendekeza
jengo hilo livunjwe ama liwe la serikali na waishi wana usalama wanaolinda
viongozi wa kitaifa.
“Baada ya FBI kutoa taarifa hizo ikulu ndipo ‘mchawi’
alipoanza kutafutwa hadi kufikia hatua ya kukamatwa walioruhusu ujenzi huo,”
kilisema chanzo.
Waandishi wetu wamegundua kuwa pamoja na tahadhari
iliyotolewa na FBI juu ya jengo hilo, lakini bado shughuli za kila siku
zinaendelea sambamba na watu kuishi.
WALIOTOLEWA ‘KAFARA’ NI HAWA
Hivi karibuni Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na Msanifu
Mwandamizi wa Majengo, Richard Maliyaga walipandishwa kizimbani wakikabiliwa na
mashitaka ya kutumia madaraka vibaya kwa kuruhusu ujenzi wa ghorofa hilo karibu
na ikulu.
Washitakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu na kusomewa mashitaka na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo.
Washitakiwa walikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana baada
ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini watatu wafanyakazi wa serikali
waliosaini hati ya shilingi milioni 50.
Souce: Global Publishers
http://paparaziblog.blogspot.com/2013/08/maisha-ya-rais-kikwete-yako-hatarini.html?spref=fb
No comments:
Post a Comment