Search This Blog

Wednesday, August 7, 2013

Moto uwanja wa ndege wa Kenya wadhibitiwa

Moto mkubwa katika uwanja mkuu wa ndege jijini Nairobi ambao umeharibu eneo muhimu la kurukia na kutulia ndege na kuilazimisha serikali ya Kenya kuzizuia ndege zote kutua, sasa umedhibitiwa, huku uchunguzi ukiendelea.
Waziri wa Usafiri na Miundombinu, Michael Kamau, anaongoza upelelezi huo. Rais Uhuru Kenyatta na mawaziri kadhaa wamekuwapo kwenye uwanja huo wa ndege tangu mapema asubuhi ya leo (Jumatano, 7 Agosti) , mara tu baada ya taarifa za moto kusambaa.
Moshi mzito na cheche za moto zimeonekana mapema asubuhi kwenye anga la uwanja huo wa ndege, zikitokea kwenye sehemu za kuwasili na kusafiri abiria wa ndege za kimataifa.
Hakuna taarifa za watu waliouawa ama kujeruhiwa hadi sasa, na abiria waliokuwa kwenye ndege ambazo zilikuwa tayari zimeshatua wakati moto huo ulipozuka, walifanikiwa kuondolewa salama.
Maafisa wa serikali wanasema sehemu ya paa la Kitengo Namba 1 cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta lilianguka kutokana na moto huo, na kuwapa tabu sana wafanyakazi wa kikosi cha uokozi kupambana na moto huo ulioanza mapema asubuhi.
Abiria wako salama
Mionzi ya moto ikionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi. Mionzi ya moto ikionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi.
Ndege zote zilizokuwa zituwe kwenye uwanja huo, sasa zimeelekezwa kutua kwenye viwanja vya ndege vya Mombasa na Eldoret, huku mamlaka nchini Kenya zikiwashauri abiria kuwasiliana na mashirika yao ya ndege kutokana na hofu ya kupanguka kwa ratiba za safari zao.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Kenya, Titus Naikuni, amewahakikishia wasafiri kwamba ajali hii ya moto haijaondosha usalama wao.
"Abiria wetu wote wanaoingia na kutoka Kenya wako salama. Kutakuwa na athari kidogo kwenye operesheni zetu na mara tutakapojua kiwango hasa cha madhara kwenye operesheni hizo, tutamueleza kila mtu kile tunachokusudia kukifanya," alisema Naikuni.
Uwanja huo wa ndege jijini Nairobi ni kituo cha watalii wanaotembelea taifa hilo la Afrika ya Mashariki na pia unatumia kama kituo cha kubadilishia ndege za kimataifa kwa wasafiri wanaoelekea maeneo mengine ya Afrika.
Ulikuwa moto mkubwa sana
Mionzi ya moto ikionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi. Mionzi ya moto ikionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imesema moto huo ulikuwa "mkubwa sana" na kwamba chanzo chake bado hakijafahamika. Shirika la habari la Ujerumani, dpa, limemnukuu msemaji wa polisi nchini Kenya, David Kimaiyo, akitaka kuwepo kwa utulivu.
"Ninatoa wito kwa wananchi wote kuwa watulivu katika wakati ambapo serikali inachunguza sababu ya moto huu. Tayari upepelezi umeanza," ameandika Kimaiyo kupitia akaunti ya Twitter ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Moto huu umetokea katika siku ambayo Kenya inakumbuka mwaka wa 15 tangu mashambulizi ya mabomu kwenye ubalozi wa Marekani jijini Nairobi.
Mashambulizi kama hayo yalifanyika pia siku na muda huo huo kwenye ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, Tanzania, ambapo matukio hayo mawili yaligharimu maisha ya watu 220.
Hadi sasa hakujawa na taarifa zozote za kuihusisha ajali hii ya moto na mashambulizi ya kigaidi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/Reuters

No comments:

Post a Comment