Ujinga ni hali mbaya sana ya kiakili; lakini pia ni hali njema sana ya akili ya mwanadamu. Ujinga - ni hali ya kutokujua kitu ambacho mtu aweza akajulishwa, akakipokea na ule ujinga kumtoka. Ujinga basi ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanadamu kwani ni katika kuwa wajinga ndio tunatoka na kujifunza vile tusivyovijua. Kwa vile akili ya mwanadamu ina ukomo wake basi kila mwanadamu kwa asili yake kabisa ana ujinga wa aina fulani. Hakuna mwanadamu asiye mjinga. Kila mtu ana ujinga wa aina fulani hivi.

Kuna ujinga wa mambo ya kawaida ambayo ni muhimu kwa mtu kuyajua ili aweze kuishi na kumudu mazingira yake vizuri. Ujinga huu uondolewa na wazazi au walezi katika maisha yetu kwani tunapozaliwa tunakuwa na kile kinachoitwa tabular rasa - ubao mtupu. Ni katika hali hii ya kuzaliwa mwanadamu anajifunza kwa mang'amuzi, kuona, na kutumia vionjo mbalimbali (perception) kuweza kujua mambo mbalimbali. Mwanzoni akijifunza vitu kwa kutumia vionjo zaidi lakini kwa kadiri anavyokua akitumia akili na hisia zake zaidi. Na mtu anapozidi kukomaa akili yake inazidi kujifunza zaidi na ni kutokana na ujuzi huo anaweza kutawala vionjo, hisia na maisha yake. Ujinga hivyo huweza kumtoka mtu.

Lakini mwanadamu ana kikomo cha mambo anayoweza kujua kwa njia ya vionjo na hisia. Kuna mambo mengine ambayo hawezi kuyajua isipokuwa kama amepata mahali pa kufundishwa au kupewa ujuzi. Hivyo tangu zama na zama watu wamechukua muda kujifunza - ama kwa njia rasmi (vyuo, na shule rasmi) au kwa njia zisizo rasmi (mazoezi ya vitendo, chini ya mwalimu mmoja n.k). Na wale ambao wanajifunza rasmi au wamepata ujuzi zaidi ya ule ambao wangeupata kwa maisha yao nao wakawa na wanafunzi wao na kuendelea kupitisha ujuzi zaidi.

Lakini katika kupata ujuzi na kujua zaidi akili ya mwanadamu inapata uwezo zaidi wa kuhoji, kuthubutu na kufikiria. Na hivyo mwanafunzi anapojifunza zaidi na anakutana na maswali zaidi anatumia kutafuta majibu na katika kufanya hivyo anaongeza elimu katika ujuzi. Ndio maana basi katika elimu moja utakuta watu wanakuwa na ujuzi tofauti na nafasi mbalimbali za kuongeza ujuzi. Mtu anayejua kuhesabu tu anaweza kuongeza na kujua zaidi ya hisabati, na akachanganya na Fizikia, au Kemia na akaongeza ujuzi zaidi na zaidi. Yote haya ni katika kuonesha kuwa mwanadamu haachi kuwa mjinga na wakati huo huo haachi kutaja kujua zaidi. Lakini akiacha kujua zaidi mwanadamu yuko kwenye matatizo. Hivyo ni lazima awe anazidi kujijuza kila kukicha ama kwa elimu rasmi au kwa kujiendeleza mwenyewe. Ujinga haupaswi kupewa kiti ukakaa!

Upande mwingine kuna hekima. Hekima ni uwezo wa mwanadamu kutumia mjumuisho wa ujuzi, hisia, na uwezo wake wote kufanya maamuzi ambayo yatakuwa mazuri na kuyakwepa yasiyo mazuri. Ni ule uwezo wa kupima matokeo ya mambo. Hekima bahati mbaya sana haina chuo au darasa. Hekima huwezi kumfunza mtu darasani; mtu anaweza kuwa na elimu ya darasani lakini asiwe na hekima ya kutumia elimu hiyo. Wakati mwingine watu wanapata shida kwa sababu mtu aliyesoma sana anadhaniwa kuwa basi ana hekima zaidi na mtu ambaye anaweza asiwe na elimu sana ya chuo akaonekana hana hekima na kudharauliwa.

Tangu tukio la Arusha nimewasikia wengi wakizungumza; na wengine wamezungumza Bungeni hadi nashindwa kueleaw kama ni ujinga (kutokujua) au ni kukosa hekima. Maana kama ni ujinga watu hawa tunaweza kuwasaidia - kwa kuwajulisha. Lakini kama ni kukosa hekima - sidhani kama kuna msaada. Hekima haiji ukubwani au uzeeni. Kama mtu anaenda Bungeni au ameanza kazi na hana hekima sidhani kama anaweza kupata hekima ukubwani. Lakini kama mtu ameshajifungua kutafuta hekima basi mtu huyo kwa kadiri anavyoishi ndivyo anavyozidi kuongeza hekima na akifika ukubwani au hata uzeeni hekima inapata kuvishwa taji.

Yote haya nimeyasema ili kuuliza maswali yafuatayo:

1. Wale wanaosema tukio la kulipuliwa kwa bomu wakati wa Ibada ya Misa ambapo Askofu Mkuu Lebulu na Mwakilishi wa Papa Askofu Mkuu Padilla walikuwa wanaadhimisha halikuwa tukio lenye mlengo wa kidini wanapata ujuzi huu wapi?

2. Na wengine ambao wanasema moja kwa moja kuwa tukio hili limefanywa na Waislamu au na Wakristu na hivyo wao wa kulaumiwa hili wanalipata wapi? Je tukio la udini ni lazima lifanywe na watu wa dini nyingine peke yao?

3: Kwanini tunapozungumzia suala la "udini" tunaonekana kuzungumzia ni udini baina ya Wakristu na Waislamu? Kwamba Msikiti ukiungua basi waliofanya ni "Wakristu" na Kanisa likiungua basi waliofanya ni "Waislamu". Kwani udini ni lazima ufanywe na watu wa dini tofauti?

4. Kama ikionekana wahusika wa tukio hili wana majina ya Kikristu je ina maana hapo hakuna udini? Kwani Wakristu wote wanaamini wanayoamini Wakatoliki? Wakati Ireland ya Kaskazini na Waingereza wako katika kugombana si waliokuwa wanalipuana wote walikuwani "Wakristu"? Kwani baadhi ya milipuko huko Afghanistan, Pakistan na Iraq si imefanywa na Waislamu dhidi ya Waislamu wenzao? Je jambo ovu likifanywa kwa misingi ya kidini na likifanywa na watu wenye imani ile ile linaacha kuwa lakidini?

5. Je kwa viongozi wa serikali kuharakisha kutoa majina ya Kikristu na kuacha ya wale raia wa UAE wanajaribu kufanya tukio hili lisiwe la kidini? Je ni ajabu wahalifu wa dini mbalimbali kushirikiana katika kufanya uhalifu? Je, kama ni kweli waliofanya tukio hilo ni wa dini mbalimbali je linaacha kuwa la kidini (angalia namba 4); siyo kwamba kwa kufanya hivyo serikali yenyewe inathibitisha kuwa wanatambua tukio hilo ni la kidini na wanajaribu kupunguza makali yake?

Kwanini naamini tukio hilo la kighaidi ni la kidini

Maoni yangu na kwa kuangalia tukio zima na yale ambayo yamesemwa hadharani hadi hivi sasa tukio hili ni la kidini. Kukana hili ni sawa sawa na kukana mwanga wa jua kwa vile mtu yuko kivulini. Shambulio la bomu linapotokea mahali popote ambapo watu wako kwenye ibada; na likifanywa likiwa na uhakika wa kusababisha madhara kwa watu wengi bila ya shaka litakuwa na masuala ya kidini ndani yake.

Swali kubwa ambalo linabakia - ambalo uchunguzi utatusaidia kutuondoa ujinga - ni kuwa dini hapa imeingia vipi? Na hili likijulikana mwitikio wa watu wa dini ile ile au dini zile zile uweje? Je kama ikijulikana kuwa tukio hilo limefanywa na Wakatoliki au Wakristu wenyewe je Wakatoliki au Wakristu waone kuwa halina makali yanayostahili au waone ni la kikundi kidogo? Je kama itagundulika kuwa limefanywa na Waislamu ina maana Waislamu waone kama wanasingiziwa wote? au ni la wale wahusika tu?

Je kama itaonekana kweli kuna suala la dini katika tukio hili - na ninaamini lipo - inajalisha nini kujua ni watu wa dini gani wamefanya hivyo?

Katika kutafuta majibu maswali haya tutakuwa tunatoa ujinga; katika kuyafanyia kazi majibu hayo ndio tutaulizana kama tuna hekima au la. Fikiria.