HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O.
MBILINYI (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA HABARI,
VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za
Bunge toleo la mwaka 2013)
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Dira ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
ni “kuwa na taifa lililohabarishwa vizuri, lina vijana wenye uwezo na malezi
bora, linathamini utamaduni wake na linakuwa mahiri katika michezo ifikapo mwaka
2025.” Aidha, ‘dhamira’ ya wizara hii ni ‘kuendeleza utambulisho wa taifa kwa
kuwezesha upatikanaji mzuri wa habari, kuwawezesha vijana kiuchumi na kukuza
utamaduni na michezo kwa umma kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.’
Mheshimiwa Spika,
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali
hii ya CCM imeshindwa kutekeleza dira na dhamira iliyotajwa katika maandiko ya
kisera ya Wizara. Badala yake, chini ya usimamizi wa Wizara hii, Tanzania imegeuka
kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya matendo ya watawala.
Tanzania imegeuka kuwa taifa linalofungia magazeti yanayofichua ufisadi, uchafu
na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa viongozi, watendaji na watumishi wa
Serikali hii ya CCM. Tanzania imegeuka, chini ya usimamizi wa Wizara na
Serikali hii ya CCM, kuwa taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa kwa kuwang’oa
kucha na meno, kuwatoboa macho, kuwamwagia tindikali na hata kuwaua. Tanzania
sio nchi inayoandaa vijana wake tena. Haiwapi tena elimu bora wala kuwapatia
maarifa, uwezo na malezi bora; ni nchi isiyowawezesha wala kuwathamini vijana wake;
ni nchi inayoruhusu vijana wake kunyonywa na kutoendelezwa; na ni taifa ambalo
limeachia utamaduni utambulisho wake kama taifa kupotea kabisa. Aidha, katika
fani ya michezo ya aina zote, Tanzania imeporomoka kutoka taifa lililokuwa
linaheshimika kimataifa katika miaka ya sabini na kuwa alichokiita rais mstaafu
Ali Hassan Mwinyi, ‘kichwa cha mwendawazimu’ ambacho kila kinyozi anajifunzia
kunyolea!
2. UHURU WA UHARIRI NA USALAMA WA WANAHABARI
Mheshimiwa Spika,
Kwa masikitiko makubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inalitaarifu Bunge lako tukufu kwamba sasa Tanzania imeingia rasmi katika
orodha ya fedheha (The List of Shame) ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni
taaluma ya hatari kwa wale wote wanaoitumia kama sehemu ya wajibu wao kwa taifa
na kama ajira yao. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari
Ulimwenguni (the Committee to Protect Journalists - CPJ) iliyotolewa mwaka huu
2013, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CPJ mwaka 1992, Tanzania imeingizwa
kwenye orodha ya nchi 20 ambazo ni hatari kwa waandishi wa habari kufanya kazi
zao kutokana na hatari ya kuuwawa kwa
mwaka 2012 (20 Deadliest Countries in 2012). Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ilishikilia
nafasi ya 7 ulimwenguni kati ya nchi 20 zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha ya
waandishi wa habari.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, tishio kubwa kwa
waandishi wa habari duniani ni kuuwawa kwa kutekwa na kuteswa na/au kutishiwa
maisha. Aidha, Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni washiriki
wakubwa wa mauaji ya waandishi wa habari. Kwa mujibu wa takwimu za CPJ, kati ya
waandishi waliouwawa mwaka 2012, karibu ya 20% waliuwawa ama na maafisa wa
serikali au na majeshi yake. Karibu idadi hiyo hiyo ya waandishi wa habari
waliuawa kwa sababu ya kufuatilia taarifa za kiuchunguzi na za hatari. Taarifa
hiyo inaonyesha kwamba hadi kufikia Aprili 2013, waandishi wa habari wapatao 30
tayari wamekwishauawa ulimwenguni wakati wakitimiza wajibu wao; wakati mwaka
2012 waandishi wa habari 103 waliuwawa ulimwenguni kote.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa
ya CPJ inaungwa mkono na ushahidi wa matukio mengi yanayodhihirisha kwamba maisha
ya waandishi wa habari wa Tanzania yako hatarini kutokana na vitendo na vitisho
kutoka kwa Serikali na watendaji wake ambao hawataki kusikia ukweli dhidi yao ukianikwa
hadharani. Kudhihirisha kauli hii tunaomba kumnukuu mwanahabari mahiri na mmoja
wa wahanga wa vita dhidi ya wanahabari na uhuru wa habari hapa nchini, Mzee
Ndimara Tegambwage:
“Mwaka 2006, waliojiita wananchi
wakazi wa jiji la Mwanza, walikusanywa na wenye uwezo kufanya maandamano
makubwa kwa walichoita ‘kupinga mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo’ na
kudai kwamba alikuwa Mkenya na ‘siyo raia wa Tanzania.’ Desemba 2009, mwandishi
Frederick Katulanda wa Mwanza, alivamiwa nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza
sauti na kudai kuwa ana nyaraka za akaunti za benki za Halmashauri ya Jiji la
Mwanza. Walikuwa na mapanga. Walikuwa wakichagizana kwa kusema, “Kata kichwa!
Kata kichwa!” Waliondoka na mafaili. Walimwachia kilema mguuni na makovu
mikononi.
“Mwezi Septemba,
2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, katika eneo la Nyambiti, Jimbo la
Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, mwandishi Frederick Katulanda alivamiwa
na kupigwa na watu wapatao 15 waliojiita “Green Guard” – wa “chama cha kijani.”
Katika “kumshughulikia,” Katulanda anasema, walikuwa wakionyesha kuwa na ujuzi
mkubwa wa judo na karate huku wakidai kuwa anawaandika ‘vibaya’ Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
“Mwaka 2011 mwandishi
Richard Massatu alikutwa amekufa katika eneo la Igoma, jijini Mwanza. Vyombo
vya habari viliripoti kuwa macho yake yalikuwa yametobolewa na kuwekwa gundi
aina ya super glue; mguu wa kushoto na mbavu vilikuwa vimevunjika. Vyombo vya
habari viliripoti kuwa Massatu aliyekuwa mmiliki na mhariri mkuu wa gazeti la
Kasi Mpya (sauti ya umma), alionekana mara ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa
na maofisa wa polisi na usalama katika baa iitwayo Cross Park katika eneo la
Igoma.
“Tarehe 3 Januari,
maiti ya mwandishi Issa Ngumba iliokotwa katika pori la mlima Kajuruheta,
kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko katika mkoa wa Kigoma.Ngumba alikuwa
mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Tangu mwezi uliopita Machi, mwandishi wa
habari Erick Kabendera anayeishi Dar es Salaam, anaishi kwa wasiwasi. Wazazi
wake waishio Bukoba, wamehojiwa na ‘ofisa usalama’ kwa kile kilichoitwa
‘uhalali wa uraia wao.’
“Kuuwawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Luninga cha
ITV, John Lubungo ambaye alikuwa mfuatiliaji mahiri wa habari zinazohusu wafanyabiashara au biashara haramu ya dawa za
kulevya ambayo inadaiwa kufanywa na watu wakubwa nchini, wakiwemo vigogo
serikalini. Kuna orodha ndefu ya waandishi wa habari waliotishwa na
wanaoendelea kutishwa; waliopigwa na polisi na askari magereza (Ukonga, Dar es
Salaama) kwa tuhuma mbalimbali; waliotishiwa maisha kwa simu na hata kwa
kufuatiliwa na watu wasiowafahamu.”
Kwa sababu ya uadilifu na kutopenda kujikweza,
Mzee Tegambwage hakutaja shambulio la tindikali na mapanga dhidi yake na mwandishi
mwenzake Saed Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi, ambalo baadae lilifungiwa na
Serikali hii ya CCM.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake wakati wa mjadala wa bajeti ya
Wizara ya Katiba na Sheria ya tarehe 3 Mei mwaka huu, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ilielezea kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa tishio
kwa maisha ya waandishi wa habari na kwa uhuru wa habari katika nchi yetu.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirejeaRipoti ya Timu Maalum ya Uchunguzi Iliyoteuliwa
na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari Daudi
Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani
Iringa,
iliyotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT)
na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), taasisi mbili huru zinazojihusisha na
masuala ya habari Tanzania.
Kwa
mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao “... yanadhihirisha bila
wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi waliwavurumisha waandishi waliotoka Iringa
wakati wakikusanya habari za shughuli za CHADEMA katika kijiji cha Nyololo.
Zaidi ya hapo, Daudi Mwangosi mwenyewe aliuawa akiwa mikononi mwa polisi huku
wakisimamiwa moja kwa moja na Kamanda (wa Polisi wa Mkoa wa Iringa SACP
Michael) Kamuhanda.” Ripoti hiyo inaelezea jinsi Marehemu Mwangosi alivyouawa:
“Alipoangalia nyuma, Daudi Mwangosi aliona kikundi cha polisi wakimpiga
mwandishi mkuu wa gazeti la Nipashe wa
Iringa, Godfrey Mushi.... Wakati mwandishi Godfrey Mushi akiwa bado anapigwa na
polisi, marehemu Mwangosi aliwakimbilia akiwaomba waache kumdhuru zaidi Mushi
kwa kuwa alikuwa mwandishi tu. Polisi hawakumsikiliza. Badala yake wakamburuta
mwandishi huyo ambaye tayari alikuwa amepoteza fahamu na kumweka kwenye gari
lao na wakamgeukia Daudi Mwangosi mwenyewe, wakampiga kwa nguvu mpaka akapoteza
fahamu.”
Hata
amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga Mwampamba kuwataka askari polisi
waache kumpiga marehemu Mwangosi haikusikilizwa na askari hao. Ili kujiokoa,
marehemu Mwangosi alimkumbatia OCS Mwampamba na “baadaye kumwangukia miguuni
mwake kuepuka kipigo zaidi.” Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, “picha za mgando
zinaonyesha polisi mmoja akipiga bomu la machozi tumboni mwa marehemu Mwangosi
kwa karibu kabisa.” Bomu hilo liliusambaratisha mwili wa marehemu Mwangosi
aliyekufa papo hapo. Kwa sababu marehemu Mwangosi alikuwa chini ya miguu ya OCS
Mwampamba, “naye pia alijeruhiwa vibaya.”
Mheshimiwa Spika,
Sio
MCT/TEF pekee zilizofanya uchunguzi wa mauaji ya Marehemu Mwangosi. Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo ilitoa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa
Tukio Lililopelekea Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012
Kijijini Nyololo, iliyobaini kwamba Marehemu Mwangosi “... alizingirwa na
askari, aliteswa na hatimaye ... alipigwa bomu na kufa papo hapo.” Aidha, kwa
mujibu wa Taarifa hiyo, “... Tume imejiridhisha kuwa tukio la lililopelekea
kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.” Taarifa ya Tume inafafanua kuwa, “...
Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki ... ya kuishi, haki ya kutoteswa na
kupigwa, haki ya usawa mbele ya sheria na haki ya kukusanyika na kutoa maoni.”
Mheshimiwa Spika,
Siku
moja baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Jeshi la Polisi lilianza kampeni kubwa
ya kujaribu kuficha ukweli juu ya kuhusika kwake, kwa kuhamishia lawama kwa
watu wengine wasiohusika na mauaji hayo. Kwa mfano, Kamanda Kamuhanda
alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba marehemu Mwangosi alifariki
“kutokana na kitu kizito kilichotupwa na waandamanaji.” Aidha, siku iliyofuata
Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja alidai kwamba baada ya
ghasia kudhibitiwa, marehemu Mwangosi alikimbilia walipokuwa polisi na “kitu
kama bomu kikarushwa na kundi la watu wanaokimbia hovyo na kumlipua Mwangosi.”
Njama
hizi za kuficha ukweli zimeumbuliwa na Ripoti ya MCT/TEF inayobainisha kwamba
marehemu Mwangosi “aliuawa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa RPC Michael
Kamuhanda.” Ripoti hiyo pia imeelezea kwa kirefu jinsi Jeshi la Polisi
lilivyotoa taarifa zinazokinzana juu ya kuhusika kwake na mauaji ya Mwangosi.
Hivyo, kwa mfano, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi
alidai tarehe 4 Septemba 2012 kwamba marehemu aliuawa na bomu la machozi ambalo
‘halikulipuliwa kitaalamu na polisi’, Kamanda Kamuhanda alitokea kwenye
televisheni siku iliyofuata “akitangaza habari za kuwatupia lawama wafuasi wa
CHADEMA kwa kutupa kitu kizito kilicholipuka na kumuua Mwangosi....”
Mheshimiwa Spika,
Hata Taarifa ya
Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi,
iliyoandaliwa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Nchimbi na kuongozwa na Jaji
Stephen Ihema imethibitisha kuhusika kwa Jeshi la Polisi na mauaji ya Marehemu
Mwangosi. Baada ya kuzunguka huku na huko ikijaribu kulisafisha Jeshi la Polisi
kutoka kwenye lawama ya kumuua Marehemu Mwangosi, Taarifa ya Kamati hiyo
inasema: “Hapakuwepo na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la
ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia.” Aidha, Kamati hiyo inakiri
kwamba “hapakuwepo umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa
ukamataji tayari askari polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.” Kwa
misingi hiyo, “… Kamati imeona kwamba … tukio la kuuawa Bw. Daudi Mwangosi na
kuumizwa baadhi ya askari polisi halikustahili kabisa.”
Mheshimiwa Spika,
Kuna uthibitisho mkubwa kwamba Serikali hii ya CCM
na Jeshi la Polisi wamekuwa wanawalenga kuwaua au kuwaumiza waandishi wa habari
wanaoandika zisizowapendeza viongozi wa Serikali au Jeshi la Polisi. Kwa mfano,
Ripoti ya MCT/TEF inaashiria kuwa sababu ya Marehemu Mwangosi kuuawa ni kwamba
yeye “... ndiye mwandishi pekee aliyemuuliza RPC (Kamuhanda) ‘maswali magumu’
kiasi cha kumkera kiongozi huyo wa jeshi la polisi.” Ripoti hiyo inafafanua kwamba
“baada ya mkutano huo na waandishi, ... baadhi ya polisi ... waliwaonya
wasiende Nyololo kwa ajili ya kukusanya habari za shughuli za kisiasa za
CHADEMA kutokana na uwezekano wa kutokea kwa hali hatarishi.” Aidha, “baada ya
mkutano wa waandishi wa habari wa asubuhi katika ofisi za RPC (Kamuhanda), ...
askari mmoja mpelelezi alimfuata Mwangosi na kumwambia: ‘Ina maana gani kwenda
Nyololo kuandika habari za Chadema ambazo zinaweza kuishia na kifo chako?’” Vile
vile, Ripoti ya MCT/TEF inabainisha, ni “... wazi kwamba Polisi walikuwa
wanawawinda waandishi wa Iringa ambao walikuwa wakiwajua.”
Mheshimiwa Spika,
Siku tatu baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi,
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika Jeshi la Polisi Robert
Manumba alitoa kauli kwa vyombo vya habari kuhusu matukio ya kuuawa kwa
waandishi wa habari ambapo alisema “….matukio ya aina hii yapo na yataendelea
kuwepo.” Katika kuthibitisha kwamba Serikali hii ya CCM ina sera isiyo rasmi ya
kulenga kuwadhuru waandishi wa habari wanaowaandika watawala vibaya na hata
kuwaua, kauli ya DCI Manumba imerudiwa tena na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magessa
Mulongo wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu jijini Arusha. Kwa mujibu wa
vyombo vya habari, Mkuu huyo wa Mkoa aliwatahadharisha waandishi kwa kuwaambia
kwamba “unapoingia katika mkakati wa kumdhalilisha kiongozi wa Serikali
unaiweka roho yako rehani…. Kuweni makini.”
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake kwenye mjadala wa Wizara ya
Katiba na Sheria, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyaita matamshi ya DCI
Manumba na Mkuu wa Mkoa Mulongo kuwa ni ‘matendo ya kigaidi’ kwa mujibu wa Sheria
ya Kuzuia Ugaidi, 2002, ambayo inafafanua ‘matendo ya kigaidi’ kuwa ni pamoja
na vitisho vinavyohusu mtu kusababishiwa maumivu au majeraha makubwa kimwili,
kuhatarisha maisha ya mtu na vinavyohusu usalama wa umma ambavyo vimelengwa au
ambavyo kwa hulka au muktadha wake vinaonekana vimelengwa kutishia umma au
sehemu ya umma.
Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama tafsiri
hiyo ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi ni sahihi au la. Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi
ya Upinzani inataka kujua ni kwa nini DCI Manumba na Mkuu wa Mkoa Mulongo bado hawajakamatwa
na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi hadi sasa? Kama tafsiri hiyo sio sahihi, basi
Serikali hii ya CCM itamke mbele ya Bunge lako tukufu kwamba ni sera yake rasmi
kwamba waandishi wa habari wanaoiandika Serikali au viongozi wake vibaya
‘wanaweka roho zao rehani’!
Mheshimiwa Spika,
Kauli ambazo zimetolewa na Serikali hii ya CCM ndani
ya Bunge lako tukufu zinathibitisha kuhusika kwa Serikali katika, kama sio kupanga
basi angalau kubariki, mauaji yanayofanywa na vyombo vya usalama vya Serikali kwa
waandishi. Na moja ya kauli za Serikali ambazo zimeifadhaisha na kuisikitisha
sana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni ile iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa
Serikali na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, Mh. William
Lukuvi pale alipomsifu Kamanda Kamuhanda wakati wa mjadala wa Wizara ya Mambo
ya Ndani: “Katika kitabu hiki cha Kambi
ya Upinzani, wamekutaja sana (Kamuhanda), hawawezi kukupongeza. Huko Iringa
Kamanda unafanya kazi nzuri sana, usitetereke na makamanda wako wa huko
Iringa.”
Ikumbukwe, Mheshimiwa
Spika, kwamba mtu anayesifiwa kwa ‘kufanya kazi nzuri sana kule Iringa’ ni
yule yule ambaye aliyelaumiwa na Tume ya Haki za Binadamu – ambayo Makamishna
wake wote ni wateule wa Rais kwa mujibu wa Katiba – kuwa alikiuka sheria za
nchi yetu na misingi ya utawala bora kufuatia tukio la mauaji ya Marehemu
Mwangosi! Mtu anayeshauriwa na Waziri Lukuvi kwamba ‘asitetereke’ ni yule yule
ambaye MCT/TEF imemhusisha na usimamizi wa moja kwa moja wa mauaji ya Mwangosi.
Needless to say, mtu huyu bado yuko
huru na hajachukuliwa hatua yoyote licha ya mshangao mkubwa kitaifa na
kimataifa!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kauli ya Mheshimiwa Lukuvi
kuhusu kuhusika kwa Kamanda Kamuhanda na Jeshi la Polisi katika mauaji ya
Marehemu Mwangosi ndio msimamo rasmi wa Serikali hii ya CCM. Aidha, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kuliambia Bunge lako tukufu ni
nini msimamo wake rasmi juu ya Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Ripoti ya
MCT/TEF kuhusu kuhusika kwa Jeshi la Polisi na Kamanda Kamuhanda katika mauaji
ya Marehemu Mwangosi. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kimya cha
Serikali hii ya CCM juu ya maswali haya muhimu ni ushahidi dhahiri kuwa mauaji
haya ni sehemu ya mkakati ulioasisiwa na Serikali hii ya CCM wa kuwanyamazisha
waandishi wa habari kwa nia moja tu: kufifisha uhuru wa kupata na kutoa habari
muhimu zinazohusika kashfa za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka serikalini.
Mheshimiwa Spika,
Miezi sita baada ya Jeshi la Polisi kumuua Daudi
Mwangosi, mwandishi mwingine mwandamizi na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, alitekwa nyara na kuteswa vibaya nje ya nyumba
yake baada ya nyendo zake kufuatiliwa na polisi na watu wengine wanaodhaniwa
kuwa watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS). Badala ya
kuchukua hatua za dhati kuwachunguza na kuwakamata wale wote waliohusika na
tukio hilo la kigaidi, Jeshi la Polisi likishirikiana na Idara ya Usalama wa
Taifa, maafisa waandamizi katika Ofisi ya Rais Ikulu na viongozi waandamizi wa
CCM chini ya Naibu Katibu Mkuu wake Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na baadhi ya
waandishi habari maslahi, walianzisha kampeni kubwa ya kuipakazia CHADEMA na Mkurugenzi
wake wa Ulinzi na Usalama Wilfred Lwakatare kwa madai ya kuhusika na ugaidi
kutokana na ushahidi wa kutunga!
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile njama dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare zimegonga
mwamba baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuyatupilia mbali mashtaka ya ugaidi
dhidi yake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa
taarifa rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya waliohusika na jaribio la
kumuua Bw. Kibanda. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya kuhusika kwa
Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Ikulu na CCM katika kutengeneza
ushahidi wa uongo dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare ili kuwapumbaza Watanzania
wasihoji shambulio la kigaidi dhidi ya Bw. Kibanda.
Kutoa taarifa ya uongo kwa lengo la kuanzisha
mashtaka ya jinai mahakamani au kutengeneza ushahidi wa uongo kwa lengo la
kuipotosha mahakama ni makosa ya jinai yenye adhabu ya kifungo cha miaka saba
kwa mujibu wa Sheria ya Adhabu ya
Tanzania. Ni muhimu kwa ukweli wa jambo hili kujulikana sio tu kwa ajili ya
kuwawajibisha kijinai wahusika, bali pia kwa lengo la kulinda demokrasia na
utawala wa sheria katika nchi yetu. Kama alivyosema Chris Conybeare, Katibu
Mkuu wa Chama cha Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC) katika ujumbe wake kwa Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara juu ya
mauaji ya Marehemu Mwangosi: “Waandishi wa habari wanapouawa demokrasia pia
inakufa.”
3. MAELEZO NA UHURU WA HABARI
Mheshimiwa Spika,
Idara ya Habari (MAELEZO)
ilikasimiwa majukumu na mali za lililokuwa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA)
na Sheria ya Kufuta Shirika la Habari la Tanzania, Na. 7 ya mwaka 2000. Wakati
SHIHATA ilikuwa na ukiritimba wa kukusanya habari pamoja na mamlaka ya kusajili
waandishi wa habari, ukiritimba huo na mamlaka ya usajili wa waandishi wa
habari yalifutwa kabisa kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au
Vyama Vingi vya Siasa Tanzania, 1991 (‘Tume ya Nyalali’), iliyobaini kwamba
Sheria ya SHIHATA ilikuwa inakiuka misingi ya uhuru wa mawazo na uhuru wa
habari.
Kwa sababu hiyo, majukumu
mapya ya Idara ya Habari, kama yalivyofafanuliwa katika kifungu cha 4(2) cha
Sheria ya Kufuta SHIHATA, ni pamoja na kutoa, kuendeleza na kuhamasisha
uanzishwaji na uendeshaji wa za kukusanyia na kusambaza habari; kukusanya na
kusambaza habari na kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu usambazaji
habari na utendaji wa mashirika ya habari. Idara ina ofisi katika baadhi ya
mikoa ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika,
Tofauti na SHIHATA, Idara ya Habari haina na
haijawahi kupewa jukumu la kisheria la kuwa msimamizi wa vyombo vya habari na
wanahabari nchini. Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa SHIHATA, Idara hii imekuwa inawauzia
waandishi wa habari vitambulisho (press cards) ambavyo vimekuwa vinatumika kama
vitambulisho cha kazi kwa waandishi wa habari hapa nchini. Vitambulisho hivyo
vimekuwa vinauzwa kwa shilingi za Tanzania elfu ishirini, lakini Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba bei ya vitambulisho hivyo imepanda mwaka
huu hadi kufikia shilingi elfu thelathini. Aidha, vitambulisho hivyo hutolewa kila
mwaka katika Ofisi za MAELEZO Dar es Salaam na hivyo kusababisha gharama na usumbufu
mkubwa kwa waandishi wa habari walioko mikoani.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo hivi vya Idara ya Habari ni kinyume cha
Sheria ya Kufuta SHIHATA. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu Idara ya Habari
imetoa wapi mamlaka ya kusajili waandishi wa habari kwa kuwalazimisha kununua
vitambulisho vya uandishi habari. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inataka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kuna masharti
yoyote ya kisheria yanayolazimu waandishi wa habari wasajiliwe na MAELEZO kwa kupatiwa
vitambulisho vya kazi na Idara hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Idara ya Habari imejitwalia mamlaka
ya kusajili waandishi wa habari kwa kuwalazimisha kununua vitambulisho vya
taaluma yao, lakini pia imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa kupanuka kwa
demokrasia na uhuru wa habari katika nchi yetu. Historia yake inaanzia miaka ya
mwanzo ya utawala wa kikoloni wa Kiingereza wakati walipotunga Sheria ya
Magazeti ya 1928. Chini ya Sheria hiyo, wakoloni walidhibiti ukuaji wa vyombo
vya habari vya wenyeji wa Kiafrika kwa kuviwekea masharti ya kusajiliwa baada
ya kutoa dhamana ya fedha taslimu.
Marekebisho ya Sheria hiyo yaliyofanywa mwaka 1952
yaliweka masharti magumu zaidi ya usajili wa magazeti pamoja na kuongeza
kiwango cha dhamana kutoka pauni za Kiingereza 160 hadi pauni 520. Kwa mujibu
wa Martin Sturmer katika kitabu chake The
Media History of Tanzania, wakati magazeti ya Wamisionari na yale
yaliyokuwa yanaunga mkono sera za utawala wa kikoloni katika Tanganyika
hayakudaiwa kulipa dhamana, magazeti yaliyokuwa na mrengo wa upinzani wa sera
za dola ya kikoloni yalilazimika kulipa dhamana hiyo.
Baadae mwaka 1955 dola ya kikoloni iliongeza
udhibiti zaidi wa vyombo vya habari kwa kuingiza katika Sheria ya Adhabu
vifungu vipya vilivyokataza uchapishaji wa jambo au taarifa yoyote lenye uwezo
wa kuleta chuki dhidi ya serikali ya kikoloni au watendaji wake. Kama
anavyosema Sturmer, kutokea hapo sheria hiyo ya uchochezi ndio imekuwa
kizingiti kikubwa kwa uhuru wa magazeti katika Tanzania. Haiwezi kuwa ajabu
kwamba wahanga wa kwanza wa sheria hiyo ya uchochezi walikuwa mabwana Kheri
Rashidi Baghdelleh na Robert Moses Makange waliokuwa wahariri wa gazeti la Mwafrika; na mhariri wa gazeti la Sauti ya TANU aliyejulikana kama Julius
Kambarage Nyerere!
Mheshimiwa Spika,
Kitu cha ajabu ni kwamba sheria iliyotungwa na
wakoloni wa Kiingereza kwa lengo la kuwadhibiti wenyeji wa Kiafrika wasidai
uhuru au kuanika uchafu na uonevu wa dola ya kikoloni haikufutwa mara baada ya
uhuru. Badala yake, sera za habari za dola ya uhuru sio tu zilipokea na
kuzidisha masharti ya kisheria dhidi ya uhuru wa habari kwa kutunga Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976
iliyoongeza makali ya sheria ya uchochezi, bali pia zilitaifisha magazeti na
vyombo vingine vya habari binafsi vilivyokuwepo wakati wa uhuru.
Hivyo, kwa mfano, Shirika la Utangazaji la
Tanganyika (TBC) lilitaifishwa kwa Sheria ya Bunge ya tarehe 16 Machi 1965 na
kubatizwa jina jipya la Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Aidha, tarehe 5
Februari, 1970, gazeti binafsi la The
Standard lilitaifishwa na Serikali. Na ilipofika tarehe 26 Aprili, 1972, The Daily News, gazeti jipya la Serikali
lilianzishwa kwa kuunganisha The Standard na gazeti la The Nationalist
lililokuwa linamilikiwa na TANU. Hivyo basi, kama anavyosema Sturmer katika historia
yake ya vyombo vya habari Tanzania, “kufikia mwaka 1976 Serikali ya Nyerere
ilishafanikisha lengo lake kuu la sera ya habari – kuwa na udhibiti juu ya
vyombo vyote vikuu vya habari....”
Mheshimiwa Spika,
Utaratibu huu wa udhibiti juu ya vyombo vya habari
kwa kutumia Sheria ya Magazeti
ulishambuliwa na Tume ya Nyalali kwa kukiuka matakwa ya ibara ya 18 ya Katiba
inayotoa uhuru wa mawazo na uhuru wa habari. Kwa maneno ya Tume hiyo, Serikali
inakiuka uhuru wa mawazo na wa habari “... kwa kujihusisha na kuchuja habari
zinazotolewa kwa wananchi.” Tume ilipendekeza marekebisho makubwa katika Sheria
ya Magazeti “... ili kuruhusu uhuru mkubwa zaidi wa habari na wa mawazo na
kulegeza uchujaji wa habari.” Mapendekezo haya ya Tume ya Nyalali
hayajatekelezwa hadi leo hii, zaidi ya miaka ishirini na mbili tangu Tume hiyo
iwasilishe Taarifa yake kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Tanzania imebakia mateka wa sera za habari
za kikoloni na za utawala wa kiimla wa chama kimoja, jirani zetu wa Kenya na
marafiki zetu wa Zimbabwe wamepiga hatua kubwa katika kupanua uhuru wa habari.
Hivyo, kwa mfano, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe iliyopitishwa kwa kura ya
maoni ya wananchi wa nchi hiyo mwezi Februari mwaka huu inatoa uhuru wa mawazo
ambao unajumuisha uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza mawazo na habari
nyingine; uhuru wa mawazo ya kisanii na wa utafiti wa kisayansi na uhuru wa
taaluma.
Aidha, Katiba hiyo inatoa uhuru wa habari ambao ni
pamoja na ulinzi wa vyanzo vya habari vya waandishi wa habari; na uhuru wa
uanzishaji wa vyombo vya utangazaji ambavyo havitakiwi kuwa chini ya udhibiti
wa serikali au maslahi ya kisiasa au kibishara. Vile vile, Katiba Mpya ya
Zimbabwe inavilazimu vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali kuwa huru
kuamua mambo gani ya kutangaza; kutokupendelea na kutoa fursa sawa kwa ajili ya
kutangaza maoni tofauti na mawazo yanayokinzana.
Mheshimiwa Spika,
Katiba Mpya ya Zimbabwe inatoa pia uhuru wa
taarifa (access to information). Hivyo, kwa mfano, kila raia au mkazi wa kudumu
wa Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na makampuni na vyombo vya habari, ana haki ya
kupatiwa taarifa yoyote inayodhikiliwa na Serikali au na taasisi au shirika
lolote la serikali katika ngazi zote, kama taarifa hiyo inahitajika kwa ajili
ya maslahi ya uwajibikaji kwa umma. Zaidi ya hayo, kila mtu, ikiwa ni pamoja na
vyombo vya habari vya Zimbabwe, ana haki ya kupatiwa taarifa inayoshikiliwa na
mtu yeyote, pamoja na Serikali, kama taarifa hiyo inahitajika kwa ajili ya
kufurahia au kulinda haki yake. Kama ilivyo kwa Zimbabwe, Katiba Mpya ya Kenya
nayo pia imetoa uhuru mpana wa habari kwa wananchi wa Kenya.
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ni
fedheha kwamba nchi yetu iliyokuwa ya kwanza kupata uhuru katika ukanda wa
Afrika Mashariki, Kati na Kusini inaelekea kuwa ya mwisho katika masuala ya
uhuru wa habari kwa watu wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali hii ya CCM kulieleza Bunge lako tukufu ni lini italeta muswada wa
sheria kwa lengo la kufuta urithi huu wa fedheha wa sheria za kikoloni ili
Tanzania iendane na karne mpya ya uhuru wa habari na wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika,
Kwa sasa vyombo vya
habari vya Serikali yaani, Radio na Television za Taifa ndio vinatoa matangazo
kwa wananchi kuhusu kile kinachoendelea Bungeni. Kwa bahati mbaya ni kwamba
Radio ya Taifa ambayo inasikilizwa na watanzania wengi wa hali ya chini na kati
katika maeneo mengi ya mijini na vijijini wanashindwa kusikiliza mijadala
inayoendelea Bungeni, kwani matangazo yanakatishwa pindi kipindi cha maswali na
majibu kinapomalizika. Matangazo ya mjadala wa Bunge yanaendelea kurushwa
kwenye Television ya Taifa hadi Bunge linapoahirisha shughuli zake kwa siku.
Mheshimiwa Spika,
Huku ni kutowatendea
haki watanzania wengi kwa kuwapa fursa kusikiliza nini wawakilishi wao wanachokiongea
katika mijadala mbalimbali Bungeni. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona sasa ni muda
mwafaka kwa sekta binafsi nazo kufanyakazi hiyo ambayo inaonyesha imevielemea
vyombo hivyo vya serikali na kuondoa ukiritimba uliopo wa kurusha matangazo ya
Bunge.
3.2 Matangazo ya serikali kwenye
vyombo vya habari
Mheshimiwa Spika,
Suala la matangazo ya serikali katika vyombo vya
habari si kwamba limekuwa likitumika kuminya uhuru wa habari katika baadhi ya
vyombo vya habari hususan vinavyoonekana kuwa vinafanya utafiti katika habari
zake kwa masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na hivyo kuweka
hadharani mapungufu na uchafu wa Viongozi waliopewa dhamana na wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Suala hilo la matangazo badala ya kuviimarisha
vyombo vya habari ili viweze kusimama na kufanyakazi bila ya kuingiliwa, sasa
linatumika kama njia ya kufifisha uhuru wa kutafuta na kutoa habari na
kuvifanya vyombo vya habari kuachana na uhandishi wa uchunguzi na hivyo kukiuka
haki za walaji za kupata taarifa kwa mujibu wa Ibara ya katiba ya 18 (d).
Mheshimiwa Spika,
Sasa kumezuka mtindo mwingine wa kuhamishia
raslimali za Serikali kwenye chama kwa ajili ya kuiokoa CCM na wanasiasa
wengine. Tutatoa mfano hai wa hivi karibuni kabisa. Kwa wafuatiliaji wa habari katika vyombo vya
habari, bila shaka watakumbuka kuwa siku ya Mei Mosi, Gazeti la CCM linaloitwa
Uhuru, lilikuwa na kurasa 79, ikiwa ni ongezeko la karibu mara tatu ya gazeti
hilo linavyotoka kwa siku za kawaida kama halina matangazo.
Kinachoweza kuwa kimewasikitisha wafuatiliaji
makini wa masuala ya habari ni kwamba matangazo hayo hayakuwa ya watu au
kampuni binafsi yalikuwa ni matangazo ya serikali na taasisi zake, kwa maana ya
kwamba yaligharimu mamilioni ya shilingi za walipa kodi wa Tanzania, ambayo
kimsingi yalipotumika ‘hovyo’ kama tutakavyoonesha kwa hoja hapa;
Mheshimiwa Spika,
Tatizo hapa si tu kwamba gazeti hili ni la CCM,
bali pia kuna masuala ya msingi kadhaa ambayo kwa kweli mtu yeyote makini,
anayejua biashara ya matangazo, hasa kutangaza kupitia vyombo vya habari,
anapaswa kuzingatia mara zote kabla hajaamua kutumbukiza mamilioni kwa ajili ya
kujitangaza;
Kwanza, kama chombo hicho ni gazeti, basi
linapaswa kuwa na wasomaji wengi na pia mzunguko mkubwa sokoni kwa maana ya
kuwafikia watu wengi kutokana na kusambaa maeneo mengi ndani (na nje ikibidi)
ya nchi. Mfuatiliaji yeyote makini wa vyombo vya habari anajua wazi kuwa gazeti
hilo la CCM, halina sifa hizo.
Kama serikali na taasisi zilizotumia gazeti hilo
la CCM kama njia ya kujitangaza zingekuwa makini na matumizi halali ya fedha za
Watanzania, lazima zingezingatia kanuni za kawaida kabisa; yaani kuhakikisha
wanapata wasomaji na soko kubwa katika bidhaa na huduma zao wanazotangaza,
hivyo wangepaswa kutangaza katika magazeti yanayosomwa na yenye mzunguko
mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Kinachoonekana hapa ni kwamba, baada ya njia
nyingine za kifisadi za kupata fedha kuisaidia CCM kushtukiwa, sasa zimebuniwa
mbinu nyingine za kifisadi za kusaka fedha kwa ajili ya chama hicho, mojawapo
ikiwa ni hii ya utoaji wa matangazo kwa vyombo vya habari vya CCM, visivyokuwa
na sifa stahili. Haya ni matumizi mabaya ya matangazo yenyewe na fedha za umma!
Ni namna ile ile ya kutoa zabuni kwa Kampuni ya
CCM, ifanye upanuzi wa eneo la bandari kwenye eneo la CCM, bila makampuni yenye
uwezo kushindanishwa ili kupata moja iliyo makini na yenye vigezo vya kufanya
kazi husika.
3.3 TCRA NA UANGALIZI WA VYOMBO VYA HABARI VYA KIELEKTRONIKI
Mheshimiwa Spika, TCRA ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia vyombo vya elkroniki kama Radio
na Televisdion, lakini imeshindwa kabisa kusimamia vyombo hivyo walivyovipatia
leseni ya kufanyakazi, kwani baadhi ya
vituo ukisikiliza vinafanya uchochezi wa kisiasa, kidini, ukabila wa
wazi lakini vimeachwa hadi
matatizo ya udini yaliposhika kasi ndio
Serikali ikaanza kukimbia kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika, Hivi sasa intaneti haitawaliwi na sheria
yoyote nchini, baadhi ya vipindi vya redio na televisheni havizingatii maadili
ya Kitanzania, maeneo mengi ya vijijini hayana huduma ya televisheni. Kambi
Rasmi ya Upinzani inasema kuwa huu ni udhaifu wa wazi kwa mamlaka hiyo iliyopewa jukumu la kusimamia.
Hivyo basi tunaitaka Serikali itoe kauli kuhusiana na udhibiti wa TCRA katika
suala hilo.
ka 2013)
3.4 SHIRIKA LA UTANGAZAJI TANZANIA (TBC)
3.4.1 TBC na matukio muhimu ya Kitaifa
Mheshimiwa Spika,Ikiwa imepita takribani miaka mitano
tangu Mhe. Raisi alipozindua rasmi Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mwezi
mei 2008. Kwa kuwa, pamoja na uchakavu na ukosefu wa vifaa TBC imeweza kupanua
masafa yake ya utangazaji karibu nchi nzima ,na kwa kuwa hili ni shirika la
umma, ni matumaini makubwa kwa watanzania kuwa TBC ingekua mstari wa mbele
katika kuripoti na kutangaza matukio muhimu yanayoendelea katika nchi yetu.
Mheshimiwa
Spika, Kwa masikitiko makubwa TBC imekua nyuma katika kuripoti matukio
muhimu na badala yake imekua ikiweka vipindi visivyoendana na matukio
yanayolikabili taifa. Hii ni dharau kwa watanzania wengi hasa ukizingatia kuwa
hili ni shirika la umma na si la mtu binafsi hivyo wajibu wake mkubwa ni kumpa
taarifa mtanzania kwa wakati hata pale inaposhindwa kutoa taarifa ama kuwepo
eneo la tukio basi lazima programu zake ziendane na hali halisi.
Mheshimiwa Spika, Kwa masikitiko makubwa wakati wa
ajali ya meli ya MV Skagkit iliyotokea mwaka jana, 2012, wakati kuna taarifa za
awali za ajali, TBC ilikua ikiweka na kupiga muziki wa taarabu bila ya
kuzingatia uzito wa ajali ile, hata siku iliyofuata kwa ajili ya shughuli za
uokoaji TBC iliendelea kuweka programu ambazo hazikuendana na uzito wa tukio
lile licha ya kuwa mamia ya watanzania walipoteza maisha na huku tafrani
ikizuka kwa baadhi ya watanzania ambao ndugu zao walikua katika tukio lile.
Mheshimiwa Spika,Katika kuonesha kuwa TBC haijifunzi
kutokana na makosa, ama labda imekosa uongozi wenye weledi na umakini tangu
kuisha kwa ajira ya mkurugenzi wao makini Tido Muhando, mwezi wa April 2013
ambako kulikua na mlipuko wa bomu Arusha,tukio ambalo lilikuwa kubwa kwenye
historia ya nchi yetu kwani ni mara ya kwanza tukio kama hilo kutokea, TBC
iliendelea na urushaji wa matangazo na vipindi tofauti huku televisheni na
vituo vingine vya binafsi vilikuwa vinajulisha taifa kuhusiana na tukio hilo.
Mheshimiwa Spika, Tukiwa katika mijadala ya muhimu ya
mustakabali wa taifa letu, ambapo tunajadili na kupitisha bajeti kwa ajili ya
watanzania, TBC hukata matangazo ya vipindi vya Bunge wakati uwasilishaji wa
hoja muhimu ukiendelea. Wakati wa hotuba ya Mambo ya ndani, wakati msemaji mkuu
wa kambi ya upinzani anakaribia kuanza kusoma maoni ya Kambi ya Upinzani , TBC
walikata matangazo na kuweka sherehe za Mwenge.
Mheshimiwa Spika,Pamoja na hayo yote, TBC bado
inaendelea na kauli mbiu yake ya 'Ukweli
na Uhakika' kauli ambayo haiendani
na uhasilia wa uratibu wa vipindi vyake vya
matangazo na uwasilishaji wa taarifa kwa umma. Mara nyingi kwenye
mijadala na hoja nzito ambazo Serikali inakua ina hali mbaya, matangazo ya
bunge hukatwa kwa kisingizio kuwa mitambo au matatizo ya kiufundi yametokea,
mbona matangazo au hitilafu za ufundi hazitokei katika sherehe za Mwenge?Ama
hitilafu kwenye kuonesha ujio wa rais wa China ? TBC inatumika na imeendelea
kutumiwa na Serikali ya CCM katika kuminya haki ya mtanzania ya kupata habari
si kwa sababu ya ufinyu wa bajeti peke yake bali kuwaridhisha watawala. Lazima
TBC ibadilike na kujua kuwa ina dhamana katika kupeleka habari na taarifa
sahihi kwa umma kwa wakati na si kwa kuendeshwa kama roboti.
4.0 MASUALA YA VIJANA
4.1 UUNDAJI WA
BARAZA LA VIJANA LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, suala la mchakato wa uundwaji wa Baraza la Taifa la Vijana, sasa umekuwa
si tu wimbo bali zimwi la muda mrefu linaloiandama serikali ya CCM na
imeshindwa kabisa kuepukana nalo.Sera ya zamani ya
maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa
katika Sera mpya ya mwaka 2007; hata hivyo Serikali imekuwa ikiwepa kuhakikisha
kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa pamoja na kuwa suala hilo
linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba
katika ilani za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vyama mbalimbali viliahidi
kuhakikisha kwamba Baraza la Vijana la Taifa linaundwa.
Mathalani,
CHADEMA katika Ilani yake 2010-2015 kipengele
6.4.1 (viii) ilitamka “Kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa hapa nchini, na
kwa kuwa uhai wa muda mrefu wa taifa letu upo mikononi mwa vijana, Serikali ya
CHADEMA itawezesha vijana kuunda Baraza la Vijana (BAVITA) ambalo limekwamishwa
na Serikali ya CCM kwa muda mrefu”.
CCM
nayo kupitia ilani yake ya katika kipengele 80 (k) “Kuhamasisha ushiriki wa
vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na kukamilisha
uanzishaji wa Baraza la Vijana”.Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inatarajia
kwamba wabunge wa pande zote katika suala hili la kuanzishwa kwa Baraza la
Vijana la Taifa kuungana kuwa kitu kimoja kuisimamia Serikali itekeleze Sera na
ahadi badala ya kuitetea kwa udhaifu iliyouonyesha.
Mheshimiwa Spika; Katika Hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo juu ya mapitio ya utekekelezaji kwa
mwaka 2010/2011 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2011/2012 tulihoji
ni lini hasa Serikali ingewezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa. Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani ilirudia tena kuhoji suala hili wakati wa mjadala wa
mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi
kwa mwaka 2012/2013. Hata hivyo, kwa nyakati zote hizo Serikali katika
majumuisho imekuwa irudia tena ambayo imekuwa ikitolewa kwa miaka zaidi ya
miaka 17 ya kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa baraza la Vijana la Taifa; bila utekelezaji kamili
na wa haraka.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inayo taarifa kwamba kufuatia hali hiyo mwezi Januari
2013 mbunge wa Ubungo, Mheshimiwa John
Mnyika aliwasilisha kwa Katibu wa Bunge
muswada binafsi wa sheria kuwezesha kuundwa kwa Baraza la Taifa la Vijana. Katika Hotuba yake juu ya mapitio ya
utekelezaji kwa mwaka 2012/2013 na makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka
2013/2014 ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Mheshimiwa
Freeman Mbowe alihoji ni lini Serikali itawasilisha bungeni miswada binafsi ya
wabunge ukiwemo muswada huo.
Mheshimiwa Spika;
kwa mujibu wa Kitabu cha hoja za wabunge na majibu ya Serikali kuhusu Hotuba ya
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2013/2014 juu
ya muswada huo “Ofisi ya Katibu wa Bunge imemwandikia Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kupata ufafanuzi kama Muswada unaohusu uanzishwaji wa Baraza la Vijana
la Taifa hautakuwa na athari zozote za kiwango cha matumizi ya fedha kutoka
Mfuko Mkuu wa Hazina kama ilivyoanishwa katika Kanuni ya 95 ya Kanuni za Kudumu
za Bunge toleo la mwaka 2007”.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inayo taarifa kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ametoa ushauri kuwa muswada huo hauwezi kuchapishwa katika gazeti la Serikali
kwa kuwa umekiuka masharti ya ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi. Kambi Rasmi ya
Upinzani ina taarifa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri huo kwa
kuwa muswada unalenga pamoja na mambo mengine kupitia kifungu cha 31 kipengele
cha kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa madhumuni ya kugharamia
shughuli za baraza la vijana la taifa, mipango ya baraza na kutekeleza miradi
ya vijana kwa ajili ya maendeleo ya vijana.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza iwapo katika kutoa ushauri
huo ilizingatia kwamba kifungu cha 31 kipengele cha pili cha muswada huo
kinataja vyanzo mbalimbali vya fedha za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko zitatokana na fedha
zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya Baraza kwa mujibu wa Ibara ya
135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.
Mheshimiwa Spika;
Ibara ya 135 (2) ya Katiba ya Nchi inatamka
kuwa “fedha ambazo hazitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali
ni zile zote ambazo zimetajwa na sheria ya kwamba zitumike kwa shughuli maalum
au ziwekwe kwenye mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka ufafanuzi kutoka kwa Serikali ni kwanini haikutoa
ushauri wa kufanya ibara hiyo ya Katiba ya Nchi kutumika kuwezesha kuanzishwa
kwa Baraza la Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana bila kufungwa na Ibara ya
99 ya Katiba kifungu cha kwanza ambacho kimeweka masharti kuwa “Bunge
halitashughulikia jambo lolote kati ya mambo yanayohusika na ibara hii
isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na
pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na Rais.”
Mheshimiwa
Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua
kuwa Kifungu cha pili kinataja mambo yanayohusika na ibara hiyo ya 99 ni pamoja
na muswada wa sheria kwa ajili ya “kuagiza kwamba malipo au matumizi ya fedha
yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko mwingine wowote
au kubadilisha kiwango hicho kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kupunguza”. Hata
hivyo, kwa zaidi ya miaka 17 maraisi na mawaziri wenye dhamana wamekuwa
wakiacha kutumia madaraka hayo ya kikatiba kuleta muswada bungeni wa kuwezesha
kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa; hivyo kitendo cha Serikali kupitia kwa
Mwanasheria Mkuu kuendeleza vikwazo hata kwa muswada binafsi wa mbunge kuhusu suala
hilo kunaashiria ukosefu wa nia njema kwa upande wa Serikali katika mchakato wa
kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa.
Mheshimiwa
Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa
mwito kwa Serikali na Uongozi wa Bunge kuwezesha muswada wa Baraza la Taifa la
Vijana kuwasilishwa kwenye mkutano huu wa kumi na moja wa Bunge unaoendelea iwe
ni kupitia muswada binafsi, muswada wa kamati au muswada wa Serikali kwa kuwa
tayari maoni yameshakusanywa kwa miaka mingi kinachohitajika sasa ni
utekelezaji wa Sera na ahadi.
Kambi rasmi ya upinzani, Tunataka kujua msimamo wa Serikali katika
bunge hili, ituambie muda mahsusi (time frame) lini hasa mchakato wa uundwaji
wa baraza hilo utakamilika na hatimaye kuanza kufanya kazi kwa Baraza la Vijana
la Taifa kwa ajili ya maslahi ya vijana wa nchi hii. Iwapo
Serikali ya CCM itaendelea kupiga dana dana muswada wa sheria wa kuundwa kwa
chombo hiki muhimu kwa maendeleo ya vijana; Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni
inayoongozwa na CHADEMA itawahamasisha vijana nchi nzima kuelekeza nguvu na uwingi
wao katika kuishinikiza Serikali sikivu ya CCM, kufanya mabadiliko yenye
kuwezesha matakwa ya vijana kutekelezwa kwa wakati.
4.2 Sekta ya maendeleo ya vijana
Mathalani katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka
jana, kazi pekee ambazo zimekuwa zikipewa kipaumbele na sekta hii ni kukimbiza
mbio za mwenge na kuratibu maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa.
Aidha kwa mwaka jana, sekta hii, kwa mujibu wa
maelezo ya wizara, ilifanya uratibu wa mafunzo ya kuwawezesha vijana kuwa na
mawazo ya kimkakati ya ubunifu na ujasiriamali katika mikoa ya Mbeya, Mwanza,
Mara, Morogoro, Geita, Njombe, Kigoma na Arusha!
Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka wizara
kulieleza bunge lako hili kwa takwimu na maelezo ya kina ni kiasi gani mbio za
Mwenge ambazo zimekuwa zikitumia mabilioni ya fedha ‘kuingiza’ mamilioni ya
fedha, zimeweza kuwasaidia vijana wa Tanzania kupambana na tatizo kubwa
linalowakabili la ukosefu wa ajira na ujira wenye staha.
Je, wizara inaweza kutoa takwimu hapa kuonesha
namna ambavyo mabilioni ya fedha waliyotengewa mwaka jana kwa ajili ya uratibu
wa mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali, wameweza kufundisha vijana wangapi na
katika maeneo yapi hasa ya utaalamu na taaluma, kwa kiwango gani ili kuweza
kuwajengea uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri kwa ajili ya kupata ujira wenye
staha.
4.3 Mikataba, mipango, sera na utekelezaji
Mheshimiwa Spika, Mwaka mzima baada ya serikali kusimama hapa bungeni na kulipatia
bunge lako matumaini na kutoa ahadi kemkem wakati wa kupitisha Azimio la
Mkataba wa Kimataifa wa Vijana wa Afrika, hadi sasa wizara hii imeendelea
kusuasua na kuzidi kutoa ahadi juu ya ahadi kuhusu kuweka utaratibu wa kisheria
wa utekelezaji wa mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Baada ya bunge hili katika mkutano wake wa mwezi Februari mwaka jana
kupitisha azimio hilo, katika hotuba ya bajeti mwaka jana, wizara hii ilisema
kuwa, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza
kuchukua hatua za kuandaa muswada wa sheria ya utekelezaji wa mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Lakini katika kuonesha kuwa serikali hii haikuwa wala haina nia ya
dhati kuweka utaratibu wa kisheria ili kusaidia utekelezaji wa azimio hilo,
katika malengo yake ya utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha
2013/14, imeshindwa kabisa kuzungumza chochote juu ya suala hilo.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaona kuwa huu ni mwendelezo tu wa serikali hii ya CCM kuendelea na
utamaduni wake wa kuwatelekeza,kuwapuuza na kuwadharau vijana wa nchi hii.Aidha
, tunataka kujua ni lini wizara italeta mswada huo hapa Bungeni kwa ajili ya
kupitishwa na Bunge na kuwa sheria.
4.4 Mbio za Mwenge wa Uhuru
Mheshimiwa Spika,mara kadhaa sasa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihoji
maswali anuai kuhusu jambo hili lakini bahati mbaya yamekuwa yakitolea majibu
yasiyokidhi haja. Nasi kwa ajili ya kutimiza wajibu wetu wa kuwasemea
Watanzania wasiokuwa na sauti ndani ya mhimili huu, tutaendelea kukumbushia na
kuhoji hadi majibu mujarabu yakakapotolewa.
Mathalani, katika moja ya malengo ya utekelezaji
wa mpango wa bajeti wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni
ukimbizaji wa Mwenge wa Uhuru. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, si tu kwamba
imekuwa ikihoji maana nzima ya kuendelea kutumia mabilioni ya walipa kodi
maskini kwenye mbio za mwenge, badala ya kuuweka makumbusho na kuufanya kuwa
moja ya vivutio vya kiutamaduni.
Mheshimiwa Spika, mtu yeyote makini hawezi kuona mantiki ya mbio za mwenge ambazo
zimekuwa zikitumia mabilioni ya fedha kuzunguka nchi nzima kuzindua miradi ya
mamilioni ya watu binafsi! Kama vile bar, nyumba za kulala wageni na mingineyo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha tumeendelea kutenga fedha kwa ajili ya
kukimbiza mwenge, randama ya wizara inaonyesha kuwa ,kijifungu 210319 zinaombwa shilingi 3,000,000 ‘kwa ajili ya kulipa matibabu na bima kwa
wakimbiza Mwenge wa uhuru’,kijifungu 210315 zinaombwa
shilingi 64,200,000 ‘kwa ajili ya kulipa posho za kujikimu kwa wakimbiza mwenge wa uhuru, kijifungu 220302
zinaombwa shilingi 57,750,000 ‘kwa ajili ya kununulia dizeli ya magari mawili yatakayotumika kwenye
sherehe za uzinduzi na kilele cha mbio za mwenge wa uhuru’,.
Aidha, kijifungu 220604 sare, wizara inaomba kiasi cha shilingi 8,886,000 ‘kwa ajili ya sare za wakimbiza Mwenge kitaifa’, kijifungu 220708
zinaombwa shilingi 25,000,000 ‘kwa ajili ya kukodi ndege kwa shughuli za mbio za Mwenge wa uhuru’, kijifungu 220709
,zinaombwa jumla ya shilingi 7,200,000
zinaombwa kwa ‘ajili ya ununuzi wa vifaa vya mkutano wa
tathimini ya mbio za mwenge wa uhuru’,kijifungu 221005 zinaombwa shilingi 78,500,000 ‘kwa ajili ya posho ya safari za kikazi ndani ya
nchi kwa wakimbiza mwenge kitaifa’ ,kijifungu 221406
zinaombwa shilingi 15,000,000 kwa
ajili ya ‘...kuandaa tuzo ...wakati wa mbio za mwenge’,
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kutengwa kwa fedha zote hizi kiasi cha shilingi 259,536,000
pesa ambazo zingewekezwa kwenye mfuko wa kuwakopesha vijana zingeweza
kuwakwamua kwenye tatizo la ajira, serikali inaomba fedha hata kwa ajili ya
kukodi ndege kwa ajili ya kukimbiza mwenge , mwaka huu tutashuhudia mwenge
ukikimbizwa angani! bado mwenge umeendelea kupoteza mwelekeo
Mheshimiwa Spika, katika kuthibitisha kuwa Mwenge umepoteza mwelekeo katika mwaka huu
wa fedha katika kijifungu 230600 ‘matengenezo ya mashine’ katika
kijifungu 230605 ‘mikataba ya
matengenezo kutoka nje’ randama uk.86 inasema ‘mwaka 2013/2014 sh.366,000 zinaombwa kwa ajili
ya kupata wataalamu nje ya wizara kwa ajili ya kutoa huduma ya matengenezo ya
chombo cha Mwenge wa uhuru’. Unaweza kuona kuwa chombo hiki kinatafutiwa mtaalamu kutoka nje ya
wizara na malipo ya mtaalamu huyo ni shilingi laki tatu! Hii ni dalili ya wazi
kuwa chombo hiki yafaa kikawekwa kwenye jumba letu la makumbusho.
Kambi Rasmi ya Upinzani, haikubaliani na serikali kutumia kiasi cha
shilingi 259,536,000 kwa ajili ya posho za kukimbiza mwenge, tunataka fedha
hizi ziingizwe kwenye programu za maendeleo ya vijana ili waweze kujiajiri na
mwenge uwekwe kwenye jumba la makumbusho, kwani umekuwa ni kero kwa wananchi
vijijini kuchangishwa fedha za mwenge bila hata kujua zinaenda kufanya nini.
5.0 USIMAMIZI WA MICHEZO NA MUSTAKABALI WAKE KWA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Pamoja na hazina ya wanamichezo nchini, lakini michezo mingi nchini
haipewi kipaumbele na serikali.Mara kadhaa vyombo vya habari vimekua vikiupa
kipaumbele mchezo wa soka kana kwamba michezo mingine haina tija kwa taifa. Leo
hii kuna michezo ambayo kama ikipewa uzito wa kutosha italeta taifa hili
heshima katika medani za kimataifa.
Mheshimiwa Spika,Labda kwa kuwa tumeshindwa kuwekeza kwenye michezo mingine kwa
vipaumbele ambavyo vinaweza kuiweka Tanzania katika ramani ya michezo, hii
imefanya michezo hiyo kufa na hazina ya taifa ya vipaji mbalimbali nayo kufa
bila kutumika. Mfano katika michezo ya 30 ya Olimpiki iliyofanyika jijini
London, Uingereza Julai mwaka 2012, Tanzania ilipeleka jumla ya wanamichezo 7
ambao hawakuambulia medani yoyote .
Mheshimiwa Spika,Wakati Afrika ya Kusini ilipeleka wanamichezo 125 kwa jumla ya michezo
17,sisi tulipeleka 7 tu. Kuna jambo kuu la kujifunza kutokana na jinsi ambavyo Serikali, sikivu , ya CCM
inaendesha nchi yetu. Jambo ambalo linastaajabisha na lenye maswali mengi
yasiyo na majibu, Je Wizara hii ina kazi gani? Ina mikakati gani ya jumla
katika kusimamia vyama vya michezo nchini ili viwe na tija? Je wizara hii ina
uchungu na fedha za kodi za wananchi hii kwa matumizi yasiyo na tija katika sekta
ya michezo? Je taifa hili limekosa kutumia michezo kama njia mojawapo ya
kutangaza jina la Tanzania na kuliweka katika ramani ya dunia kwa kuwa na
wanamichezo bora na si bora wanamichezo?
Kambi rasmi ya Upinzani, inapendekeza kwa msisitizo mkubwa kuwa katika
kipindi hiki ambacho taifa letu lipo katika mpasuko na mgawanyiko wa masuala
mbalimbali kuanzia udini,mchakato wa katiba nk , katika kipindi hiki ambacho
mshikamano na umoja wetu kama taifa upo katika hatari ya kusambaratika, jambo
ambalo linaweza kutuunganisha kama taifa moja lililobakia ni michezo .
Hivyo basi tuhakikishe kwamba timu ya taifa ya mpira wa miguu
inaandaliwa vya kutosha na tuweze kuingia kwenye fainali za kombe la dunia
ifikapo 2014, tuna kazi ndogo ya kuifunga Morocco kwao, tunatakiwa kuifunga
Ivory coast hapa kwetu, tunaamini inawezekana kama mipango madhubuti ikiwekwa
sasa.
5.1 Chama cha Riadha Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012, katika mashindano ya taifa
ya riadha kulikua na changamoto kubwa ya wanariadha kushiriki katika mashindano
ya taifa bila ya maandalizi ya kutosha, huku baadhi ya wanariadha wakishiriki
katika mashindano bila ya kuwa na viatu. Haya ni mashindano ya taifa, Chama cha
Riadha (RT)nchini, kimeyandaa bila ya kuwa na mikakati ya kitaifa ya kuhakikisha
kuwa vigezo na viwango vimefuatwa.
Aidha , chama hiki kimekuwa
kikilalamikiwa sana na wadau wake kutokana na hisia kwamba kunakuwa na
upendeleo katika kutuma wanariadha ambao wamekuwa wakiwakilisha taifa letu
katika michezo mbalimbali ya kimataifa.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua serikali imechukua
hatua gani dhidi ya viongozi wa chama hiki ambao badala ya kusimamia riadha
wamekuwa hawafanyi hivyo , aidha kuna mikakati na mipango gani ya kuinua
kiwango cha riadha hapa nchini ili kurudhisha heshima ya taifa kwenye mchezo
huu maarufu duniani kote?
5.2 Mapato ya viwanja vya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa randama uk
102 katika mapato kuna kifungu 140259 ambacho kinahusu mapato ya viwanja vya
michezo (uhuru na Taifa) makadirio yalikuwa kukusanya shilingi 400,000,000 kwa mwaka 2012/2013 ila
mapato halisi yaliyokusanywa kutokana na asilimia 15 ya mapato yote
yanayokusanywa kutokana na kutumika kwa kiwanja hicho mpaka februari 2013
yalikuwa 329,814,400 tu.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua mapato hayo yalikusanywa
kutokana na michezo mingapi na fedha hizo zilitumika katika kufanya kazi gani
za kuendeleza michezo hapa nchini.
5.3 Malipo kwa makocha wa kigeni.
Mheshimiwa spika, katika mwaka huu wa
fedha serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.230 katika kifungu
6004-280518 (Baraza la Michezo la Taifa –Makocha)(chanzo:randama, jedwali namba 8) kwa ajili ya matumizi
mengineyo (OC),Aidha kwenye fungu hilo hilo 6004 kwenye matumizi ya kawaida (chanzo randama ;jedwali namba
6) zimetengwa jumla ya shilingi milioni 586,079,000 kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo
zimetengwa shilingi 1,917,960,000
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa randama ya
wizara uk.93 kijifungu 270800 ‘ruzuku
kwa asasi na vituo’ zimetengwa jumla ya shilingi 1,564,382,000 na katika
kijifungu kidogo cha 270813 ‘Baraza la
Michezo la Taifa’ zimetengwa shilingi
1,524,382,000 kwa ajili ya ‘mishahara
ya Makocha wa Kigeni’ na matumizi ya Baraza la michezo la Taifa. Aidha
katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwenye kijifungu hiki zilitengwa jumla ya
shilingi 823,546,000 tu kwa ajili ya
mishahara kwa makocha wa kigeni.
Wakati kichwa cha habari
cha kasma hii na kijifungu hiki kikisema ni ‘ruzuku kwa asasi na vituo’ ,
ruzuku inayokwenda kutolewa ni kiasi cha shilingi
milioni 40 tu kama ambavyo inaonekana kwenye kijifungu 270839 kituo cha
michezo Arusha shilingi milioni 20 na kijifungu 270840 kituo cha michezo Songea
shilingi milioni 20.
Kambi rasmi ya upinzani, inaona kuwa fedha hizi
ni nyingi sana kwa ajili ya mishahara na marupurupu ya makocha wa kigeni, hivyo
basi tunataka kujua yafuatayo;
i.
Ni makocha wangapi watalipwa na ni wa michezo
gani?
ii.
Wanapewa marupurupu gani kama stahili zao?
iii.
Kwanini serikali na wizara hii isiwapeleke
makocha wa kitanzania mafunzoni nje ya nchi ili waweze kutumikia taifa lao
pindi wakimaliza masomo yao?
6.0 BARAZA LA KISWAHILI TANZANIA
Mheshimiwa Spika,Wizara inao wajibu wa kuimarisha, kukuza na kuendeleza lugha yetu ya
Kiswahili kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano ikiwa ni pamoja na uratibu na
kuhakikisha ustawi na maendeleo ya utumiaji wa Kiswahili kwa kushirikiana na
asasi zile ambazo zinahusika na uendelezaji wa lugha hii hapa nchini. Baraza lina wajibu wa kuhakikisha kuwa
matumizi ya Kiswahili yanapewa kipaumbele katika maisha ya kila siku ya
mtanzania, ikiwemo katika shughuli za kitaifa na kimataifa ambazo viongozi wa
taifa letu wanahudhuria.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na nyimbo ambazo Serikali ya CCM imekua ikiziimba mara kwa mara
kuwa inataka kukuza lugha ya Kiswahili ili kuutangaza utamaduni wa Tanzania
katika jumuia ya kimataifa ni aibu kubwa kwa taifa letu pale ambapo viongozi
wake waandamizi wanapokuwa watumwa wa lugha za nchi za Magharibi!
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Serikali ya CCM imeamua kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia
na nchi ya China, ni kitendo cha kusikitisha na aibu kuona kuwa wakati wa ziara
yake nchini, Raisi wa China, alihutubia na kuzungumza kwa ufasaha lugha ya
taifa lake wakati Rais wa Tanzania na Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa
kimataifa wakitumia lugha ya Kiingereza. Swali la kujiuliza, kama Raisi wa nchi
pamoja na waziri wake wanaona ugumu kutumia lugha ya taifa wakati mgeni wao
ametumia lugha ya taifa lake wakati walengwa wa ujio ule na wageni wengi
waliokuwa katika uzinduzi wa Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere wengi
walikua ni watanzania, je itakuaje kwa mwananchi wa kawaida leo? Lugha ya
Kiswahili haiwezi kukua wala kupewa umuhimu na mataifa mengine ikiwa viongozi
wa Serikali wanaonesha hadharani utumwa wa utamaduni wa nchi za magharibi,
lazima kwa nguvu zote Bunge na taifa tukatae aina hii ya utumwa kwa maana kuwa
hata Serikali inayotakiwa kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili na
kukitangaza, wamekua mstari wa mbele kutumia lugha ya Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani
tunajiuliza hivi, Hata kama Serikali ya CCM imeshindwa kulinda tembo wetu basi
hata Kiswahili mshindwe kukilinda? Tunarudia tena, huu ni utumwa! Haukubaliki!
Tutumie na kukitangaza Kiswahili kwenye dhifa na hafla za kimataifa, kwa kuwa
Kiswahili ndiyo urithi wetu.
7.0 USIMAMIZI WA HAKI ZA WASANII NA USHIRIKI WA SERIKALI KATIKA
UTEKELEZAJI
Mheshimiwa Spika, Sheria ya hakimiliki inayotumika sasa katika kusimamia hakimiliki na
hakishiriki za wasanii , ni sheria iliyopitishwa na Bunge inayojulikana kama
Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki namba 7 ya 1999. Hii iliiondoa sheria ya
awali Sheria ya Hakimiliki namba 61 ya 1966. Sheria hii imeendelea kutumika
baada ya kutungwa kanuni mbalimbali mwaka 2000 na kuanza kutumika zikiwemo
sheria iliyounda COSOTA. COSOTA ilianza kwa kuwa na bodi iliyokuwa mchanganyiko
wa wajumbe waliochaguliwa na wasanii na wajumbe walioteuliwa na Waziri wa
Viwanda na Biashara. Na hali hii ya kuwa na wawakilishi wasanii katika COSOTA
iliendelea mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho 2007, ambapo Waziri
hakuweza kuteua Mwenyekiti wa bodi ya chombo hicho na hivyo kuzuia Bodi kuweko.
Mheshimiwa Spika,hata alipoulizwa na Mh. Martha Mlata kwenye bunge la bajeti 2008
aliahidi kushughulikia na hakufanya hivyo hata akaulizwa tena bunge la bajeti
2009. Hivyo hatimaye 2011 ikateuliwa
Bodi ambayo haikuwa na muwakilishi kutoka wasanii japokuwa COSOTA iliendelea
kukusanya mirabaha ‘kwa niaba ya wasanii’.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua ni kwanini bodi hii haina
mwakilishi wa wasanii kama sheria inavyotaka? Lini mwakilishi huyo atateuliwa
na wizara?
7.1 Kulinda kazi za wasanii
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2001, ilitengenezwa kamati iliyoitwa National Anti Piracy
Committee ikiongozwa na Mwenyekiti John Kitime, iliyokuwa chini ya COSOTA, kazi
yake kubwa ni kuwezesha kutengeneza sheria na kanuni za kuwezesha kazi za audio
na video kuwa na stika za mapato. Kazi hii ilifanyika na kukamilika na kanuni
hizo zilipita kwa usimamizi wa Waziri Mh. Juma Ngasongwa kabla tu ya uchaguzi
wa mwaka 2005, lengo likiwa ni kupata sapoti ya wasanii.
Mheshimiwa Spika, Baada ya jitihada za hapa na pale, Serikali kwa kupitia TRA wameleta
stika mpya, ambazo Tatizo moja tu hapa
ni kuwa TRA kazi yao ni kukusanya kodi tu na sio kulinda hakimiliki, hivyo
stika ya TRA ni stika ya kukusanya kodi na italeta mkanganyiko katika
utekelezaji wa taratibu za hakimiliki. Je, wizara imepanga mikakati gani
kuhakikisha kuwa kazi za sanaa hazidurufiwi, kuuzwa na kusambazwa bila ya
ridhaa za wasanii nchini? Kambi rasmi ya upinzani bungeni inarudia kuitaka
Serikali kuifumua COSOTA na kuunda chombo kipya kitachokuwa na uwezo wa
kusimamia kazi za sanaa.
7.2 Nyimbo za wasanii na Mapato kwao.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2003 zilipitishwa kanuni zilizoagiza wenye vyombo vya utangazaji
nchini ziwalipe wanamuziki kutokana na matumizi ya nyimbo zao mbalimbali ambazo
wanazitumia kwenye vipindi mbalimbali. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa
Serikali ya CCM inayojitapa kuwa na utawala wa sheria inashindwa kudhibiti
vyombo vya habari na utangazaji ambavyo vimeendelea kutumia kila aina ya ubabe
na njia za kiunyonyaji ili visilipe fedha hizi kwa wasanii. Leo hii wasanii
wanalazimishwa kuandika barua kuwa wametoa nyimbo zao kwa vyombo hivyo zipigwe
bila kulipia na kutokana na mazingira yaliyotengenezwa, wanamuziki wanajikuta
ni lazima wahonge! ili nyimbo zao zipigwe ili waweze kupata soko la kazi zao.
Mheshimiwa Spika,Wizara hii ambayo inasimamia TBC, televisheni na redio ya Taifa,
imeshindwa kuvichukulia hatua za kisheria vyombo vyake ambavyo vimekua moja wapo
ya wakiukaji wa sheria hii. Ni kejeli kwa taifa, ni kejeli kwa wasanii
wanaopata shida kujikwamua kimaisha. TBC leo inapiga na kucheza nyimbo za
wasanii bila kuwalipa, huku wizara inayotakiwa kusimamia vyombo hivi
inashuhudia sheria zilizopitishwa na bunge hili zinavunjwa.
Mbaya zaidi TBC inauza CD na kanda za nyimbo
zilizoko katika maktaba yake bila kutoa hata senti kwa wanamuziki waliorekodi
nyimbo hizo, iko wapi tofauti yao na maharamia wengine? Leo hii wizara inawezaje
kusema kuwa wao ni wasafi? Ni aibu kwa wizara, ni aibu kwa watendaji wake, ni
aibu kwa serikali , sikivu, ya CCM!
7.2 Harakati za kudai haki za wasanii.
Mheshimiwa Spika, sanaa imeendelea kufanywa mtaji wa biashara na watu wachache ambao
wanatumia nguvu waliyo nayo katika jamii na uwezo wao wa kifedha katika
kukandamiza maslahi ya wasanii hapa nchini. Katika harakati za kutafuta haki za
wasanii hapa nchini, mimi binafsi pamoja na wasanii wengine wachache,
tulianzisha harakati za kudai haki kwa
kupitia programu maarufu iliyojulikana kama
'Anti Virus' chini ya 'Vinega'
ikiwa na lengo na juhudi za kudai haki za wasanii dhidi ya ukandamizaji
unaofanywa na wajanja wachache kwenye muziki, ambao wametumia nafasi kama njia
ya kutumia mitaji yao ya fedha kuwaendesha wasanii jinsi wanavyotaka wao.
Mheshimiwa Spika, Kama ilivyo kawaida, wasanii wengi walidharau jitihada zetu na
kutotuunga mkono. Leo hii katika tasnia ya muziki, kuna mgogoro mkubwa uliofuka
moto kati ya msanii maarufu Lady Jaydee dhidi ya wamiliki wa radio ya Clouds FM
hatua iliyosababisha nyimbo za
wanamuziki wa kizazi kipya maarufu kama 'Bongo
Flavour' kutopigwa kwa siku moja katika kituo hicho. Sasa, ukiangalia kilio
cha Lady Jaydee ni kilio kilekile kilichopelekea VINEGA kuingia vitani.
Mheshimiwa Spika, kama msemaji mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, na mwenye dhamana na uchungu
na tasnia ya sanaa nchini, niweke wazi kwa umma wa watanzania kuwa, tumefikia
hapa tulipo si kwa kuwa na sheria kandamizi tu bali pia kwa kukosekana kwa
umoja wa wasanii nchini. Wakati tukiwa na juhudi za kutetea maslahi ya
watanzania kupitia Anti Virus, ni
wasanii wachache ambao walituunga mkono na wengi wao wakibeza jitihada zetu,
wakiwemo hawa ambao leo wanalalamika kuwa wananyonywa haki zao. Wengine
walifikia hatua ya kusema kuwa tumepewa fedha ili kuzima harakati
tulizozianzisha.
Mheshimiwa Spika, Umoja wa wasanii hasa wa muziki wa kizazi kipya nchini, unasimamiwa na
chombo halali kinachojulikana TUMA-‘Tanzania Urban Music Association’, lakini
kutokana na ujanja wa watu wachache, waliudhoofisha umoja huu kwa kuanzisha
kampuni iliyosajiliwa kama TFU- ‘Tanzania Flavour Unit’ iliyowalaghai wasanii
kuwa ni muungano wa wanamuziki wa Bongo Fleva na kuhodhi majukumu ya TUMA
ambacho ni chama halali cha kusimamia wanamuziki wa Bongo Fleva. Mpaka
tunapoongea leo hii, hata Studio iliyotolewa na Mheshimiwa Raisi, bado ipo
katika mikono ya TFU pamoja na Serikali kuamuru irudishwe katika mikono ya
Serikali ili ikabidhiwe kwa wasanii wote chini ya chama halali cha TUMA. Sasa
tunataka wasanii wote nchini waache uoga na unafiki na wajiunge na vyama vyao
halali ili viwatete haki zao.
Mheshimiwa Spika,Kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa utetezi wa haki za wasanii kwa kuwa wanaotuhumiwa
kunyonya haki za wasanii wameweza kutajirika na kuneemeka kwa kupitia jasho na
mgongo wa wasanii. Hawa hawa wanaotuhumiwa kuhujumu wasanii ndio wanatumia
nafasi yao kuupotosha ukweli wa tuhuma dhidi yao. Wanatumia fedha na rasilimali
walizo nazo katika kunyanyasa wasanii, kuwakandamiza, kuwapokonya haki zao na
kuwadhalilisha kuwa bila wao, wasanii wasingekua kitu.
Mheshimiwa Spika, Leo hii wasanii wanaishi kwenye hali ngumu, umasikini mkubwa lakini
bado wanatolewa maneno ya kashfa na dharau na Serikali imeendelea kukaa kimya.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kuacha siasa kwenye kutatua
migogoro ya taifa hili. Siasa zimetumika sana katika kuzima jitihada za
wanyonge kwenye taifa hili, leo hii wananchi hawana imani na Serikali kwa kuwa
imeonesha wazi imeshindwa! Kushindwa kwa Serikali katika kutatua migogoro ya
wasanii kwa kutotekeleza makubaliano mbalimbali yanayoafikiwa kati yake na
wasanii, yameshusha hadhi yake kwa wasanii. Swali kubwa kwa Serikali sikivu ya
CCM, Je mnasubiri migogoro mingapi ili mjue kuwa wasanii hawatendewi haki? Je
mnasubiri vikao vingapi vya upatanishi
na usuluhihishi ili mjue kuna tatizo? Ama mnataka wasanii wagombane,
wapigane, wauane ili mjue kuwa kuna tatizo?
Mheshimiwa Spika,Leo hii, Serikali bila ya kukaa na wadau wa muziki wa dansi, taarabu,
bongo fleva, hip hop, mnanda na mahadhi mengine na kuwasikiliza kwa makini
wamejikuta wanajihusisha na mambo ambayo hawajui. Watendaji wa Serikali
wameendelea kuwaingiza mkenge viongozi wa Serikali katika masuala ya sanaa
nchini. Hivi karibuni,hapa Dodoma, bila ya kuwa na taarifa muhimu juu ya
unyonyaji wa haki za wasanii, waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda, alishiriki katika
tamasha la kudai haki za wasanii ambalo liliandaliwa na baadhi ya watu ambao
kwa muda mrefu wamekua wakituhumiwa kuwa ni wanyonyaji wa kazi za wasanii.
Kiongozi mkuu wa Serikali, unashiriki katika kupiga mihuri na kuhalalisha
mikakati ya kimafia ya kuua umoja wa wasanii bila ya kuwa na taarifa sahihi.
Je, waziri mkuu ana taarifa kuwa walioandaa tamasha la kudai haki za wasanii
ndio walalamikiwa namba moja nchini dhidi ya haki za wasanii hasa wa muziki?
Tuinataka Serikali na wanasiasa wote kuacha kutumia wasanii kwa faida zao binafsi bali wasaidie kutatua
matatizo halisi ya wasanii ili waondokane na umasikini.
8.0 UTAMADUNI NA MALIKALE NCHINI
Mheshimiwa Spika,Zipo njia mbalimbali ambazo zinatambulisha utamaduni wa mtanzania kwa
mataifa mengine. Utamaduni wetu unatambuliwa kwa kupitia lugha, mavazi,
vyakula, sanaa, maadili na malikale za taifa letu. Leo hii ukiangalia
makumbusho ya taifa, haina vitu vya msingi vya kufanya makumbusho kuwa chanzo
cha kuliingizia taifa fedha za kigeni kwa njia ya utalii. Sehemu nyingi nchini
ambazo zinaelezea utamaduni wetu na asili ya taifa letu, kama Bagamoyo, Kilwa
Masoko, Kilwa Kivinje, Isimila, Zanzibar haziwekwi katika mazingira ya
kuyatunza kwa ajili ya kuelezea asili ya taifa letu.
Leo hii , Serikali ya CCM ikijitetea kuhusu
kuboresha ama kutunza malikale za taifa letu ikiwemo majengo ya kale,
itajigamba kuwa imeyapaka rangi. Lakini ni maajabu kuona majengo yale,
yamepakwa rangi nyeupe, chokaa hali inayoyafanya majengo haya kuwa na rangi za
kijani zenye ukungu inapokuja suala la ukarabati wake. Ukiangalia marekebisho
ya majengo hayo, yamefanyika na kuondoa uasilia wa majengo hayo kama yalivyokua
zamani,.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaiuliza Serikali je,imeshindwa kutafuta wataalamu wa majengo wenye
kuweza kurekebisha na kuyatunza majengo katika hali ilokuwa bila ya kuyaharibu zaidi? Ni mikakati ipi
ambayo Serikali imejiwekea kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014 katika kuyatunza
na kuyatengeneza majengo ya kale ili
kutunza utamaduni wa taifa letu?
10.0 UCHONGAJI WA VINYAGO NA THAMANI YAKE KWA TAIFA
Mheshimiwa Spika,Kama kawaida Serikali ya CCM imeendelea kutawala huku kukiwa hakuna
utaratibu mzuri wa kusimamia maslahi ya wachongaji wa vinyago hapa nchini.
Wachongaji wa vinyago ambao wamesaidia kwa kiasi kikubwa kutangaza utamaduni wa
taifa letu kwa kutumia kazi zao za sanaa hapa nchini hasa katika kutangaza
utalii.
Kwa taarifa tulizonazo kutoka kwa wachongaji
vinyago ni malalamiko ya kazi zao za sanaa kununuliwa na kisha kusafirishwa
kuelekea nchi za nje ambapo huko hupigwa mihuri kuwa imetoka katika nchi za
jirani. Hii imeua soko la vinyago hapo nchini na kukandamiza maslahi ya
wachongaji hawa ambao ni hazina kwa taifa letu. Wachongaji vinyago wana umuhimu
mkubwa katika kulinda utamaduni wa nchi yetu kwa kuwa ni urithi tuliopewa na ni
lazima Serikali iweke mikakati ya kuhakikisha kuwa soko la vinyago ndani na nje
ya nchi linamufaisha mchongaji kimapato.
Kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka Serikali kutoa kauli hapa bungeni ina
mkakati gani uliowekwa kwa mwaka huu wa fedha katika kuhakikisha kuwa
wachongaji vinyago wananufaika kwa kazi zao hasa ukizingatia kuwa, soko la
ndani la vinyago halina faida ya kutosha na usimamizi wa kina. Vinyago ambavyo
vinachongwa Tanzania vimeendelea kuuzwa nje ya nchi na kuzipatia nchi hizo
mapato makubwa na baadhi ya kazi hizo hazitambuliwi kuwa zinatoka nchini.
11.0 USIMAMIZI WA HAKI ZA WASANII KATIKA UUZAJI WA MIITO YA SIMU
Mheshimiwa Spika,Biashara ya miito ya simu, inayofanywa na makampuni ya simu nchini ni
biashara ya siri ya kimafia inayohitaji kuwekwa wazi kwani kuna ukwepaji mkubwa
wa kodi na haki za wasanii, ambapo pamoja na waliojiunga kihalali kutopata haki
yao wako wale wanaokuta nyimbo zao zinatumika bila kujua zimepelekwa huko na
nani na kwa mikataba ipi. Leo vyombo vyote vya Serikali vinavyotakiwa kusimamia
sheria na kanuni za hakimiliki zinakaa kimya huku wasanii wakipokwa haki zao,
taifa likipoteza mapato na kuubariki wizi huu wazi wazi.
Mheshimiwa Spika,Hivi karibuni tumeshuhudia Serikali ya CCM kupitia wizara yake yenye
dhamana ya kufuatilia biashara ya miito ya simu, wizara ya mawasiliano, sayansi
na teknolojia imeshindwa kutoa majibu ya ufuatiliaji wa tozo na mapato ya miito
ya simu, Mmeshindwa kutimiza wajibu wenu kwa wananchi lakini pia mmeshindwa
kutimiza wajibu wenu katika kutekeleza matakwa ya katiba ya nchi hii, kuulinda
uhuru na haki za wananchi wake kama ambavyo muasisi wa taifa hili alijitahidi
kufanya.
12.0 TASNIA YA
FILAMU NA MCHANGO WAKE KATIKA KUKUZA UCHUMI NCHINI
Mheshimiwa Spika,Tasnia
ya filamu nchini imeendelea kukua kila siku huku kukiwa na usimamizi mdogo wa
Serikali katika kuhakikisha kuwa sekta hii inatumika vizuri kama chanzo cha
kukuza ajira nchini lakini pia kama moja ya njia ya kuwaongezea wananchi kipato
na Serikali kukuza uchumi kwa kupitia kodi mbalimbali. Leo hii, soko la filamu
nchini Nigeria limeweza kuingiza takribani kiasi cha dola 250 milioni kwa mwaka
kama mapato ya filamu zinazotengenezwa kwa soko lao la Nollywood, je Serikali
kupitia wizara hii imefanya tathmini gani kwa kupitia mamlaka za mapato na
kujua soko la filamu kwa mwaka linaingiza kiasi gani hapa nchini? Kambi rasmi
ya Upinzani, inaitaka Serikali ya CCM kuacha kufanya kazi kwa mazoea sasa na
badala yake ivisimamie vyombo husika kuhakikisha kuwa sekta ya filamu inapewa kipaumbele
pia na thamani ili kuweza kukusanya kodi na kupunguza umasikini nchini. Tasnia
ya filamu si tu inaweza kuliingizia soko hili fedha bali pia ikipewa thamani
inauwezo mkubwa kwa kutatua tatizo la ajira hapa nchini. Kwa kuwa mpaka sasa,
Tanzania imeshatoa filamu nyingi na soko lake kupanuka katika nchi za Afrika
Mashariki na kati, je tasnia hii mpaka sasa imeweza kuzalisha ajira ngapi?
Kambi rasmi ya upinzani, inaitaka wizara kuja na takwimu rasmi za ajira
zilizotokana na tasnia hii kufikia mwezi Machi mwaka huu.
Mheshimiwa Spika,Tanzania
ambayo imebarikiwa kwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Mlima
Kilimanjaro, mbuga za wanyama za Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Mikumi pamoja
na hifadhi za wanyama kama Selous, Tarangire, maziwa makubwa ya Victoria,
Tanganyika na Nyasa, sehemu zenye asili ya utumwa kama Bagamoyo, Zanzibar,
Kilwa Masoko, misitu mikubwa, mito na vivutio mbalimbali; ina nafasi kubwa ya
kutumika kama moja ya 'film destinations' duniani kama ambavyo nchi nyengine
imewekeza.
Mheshimiwa Spika,Nchi
mbalimbali zimeweza kujiingizia fedha za kigeni kila mwaka kutokana na kutumia
vivutio walivyo navyo na mandhari ya nchi zao kupitia tasnia ya filamu. Nchini
Afrika Kusini, tasnia ya filamu ina thamani ya kiasi cha takribani randi 12 bilioni
sawa na shilingi trilioni 2.17 za kitanzania huku ikichangia kiasi cha shilingi
1.4 bilioni kwenye uchumi wa taifa na ongezeko la kiasi cha shilingi milioni
400 kwa mwaka katika kipindi cha miaka minne toka mwaka 2008 walipoamua kufanya
mabadiliko ya tasnia ya filamu. Zaidi , tasnia ya filamu imeweza kuongeza soko
la ajira kwa kutoa karibu ajira 30,000.[1]Afrika
kusini imeweza kutumia sekta hii kwa kwa kutumia mandhari waliyo nayo ambayo
inafanana na mandhari za takribani nchi 57 ulimwenguni na kutumika kutengeneza
filamu zenye mafanikio Hollywood. Ipo haja ya wizara hii kwa kushirikiana na
wizara ya maliasili na utalii kufanya tathmini ya kina na kutengeneza mazingira
ya kutumia vivutio tulivyo navyo ili kuifanya Tanzania sehemu bora zaidi Afrika
kwa ajili ya kutengeneza filamu kwa kupitia mandhari zake. Lazima Serikali
itengeneze mkakati endelevu wa kuendeleza sekta ya filamu nchini kwa kuitangaza
Tanzania katika anga za kimataifa kama 'film destination' bora zaidi Afrika.
13.0 MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI 2013/2014
Mheshimiwa Spika, katika makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hii kwa mwaka wa
fedha 2013/14, jumla ya shilingi 21, 328,045,000, zimeombwa kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.
Aidha, kama ilivyo ada ya miaka yote kwa bajeti za
serikali hii ya CCM, katika wizara zote, fedha za matumizi ya kawaida ni nyingi
kuliko fedha ambazo zinatarajiwa kutumika katika miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Suala linaloweza kumuumiza mdau yeyote ambaye angependa kuona wizara
hii ikisonga mbele ni pale ambapo miradi ya maendeleo imetengewa sh.
600,000,000 pekee, wakati kuna kiasi cha takriban bilioni 10 zimetengwa kwa
ajili ya kitu kinachoitwa ‘matumizi mengineyo’.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inahoji hayo matumizi mengineyo yasiyojulikana
au kuelezwa hapa mbele ya bunge lako lakini yanatengewa karibu nusu yote ya
bajeti ya matumizi ya kawaida, ni nini na yapi?
Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba
kuwasilisha.
.......................................
Joseph Osmund Mbilinyi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Habari,Vijana,
Utamaduni na Michezo.
20.05.2013