Saratani imeendelea kuwa tishio hapa nchini huku hofu ikiendelea
kuikumba jamii kutokana na wataalamu wa afya kushindwa kufahamu tiba
halisi ya maradhi hayo hatari.
Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road
zinaonyesha ongezeko la saratani ya mdomo na koo kwa kiasi kikubwa
kutoka kesi 167 mwaka 2006 hadi 277 mwaka 2012.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Ocean road, Julius
Mwaiselage anaeleza kuwa watanzania wasipende kuiga mambo ambayo si
sahihi bila kujua madhara yake kama kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo.
“Saratani ya mdomo ipo, na nyingine zinasababishwa na zinaa “ anasema Dk
Mwaiselage
|
Mdomo ukliwa umeathiriwa na bakteria kufuatia kutumiwa kama njia ya kufanya mapenzi
|
Tafiti mbalimbali zimewahi kufanyika nchini na
kubaini kuwepo kwa ongezeko la saratani ya mdomo.Utafiti uliofanywa na
Dk Innocent Mosha wa Kitengo cha Patholojia cha Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH), umebaini aina za saratani 1,594, kati ya hizo 509
zikiwa ni za midomo kwa mwaka 2003 pekee.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kati ya saratani 509
za mdomo, saratani 242 zilisababishwa na Virusi vya Human Papiloma
ambavyo hutokana na zinaa.
“Ninachojua mimi ni kuwa Virusi vya HPV
husababishwa na magonjwa ya zinaa, hivyo mtu anayeugua saratani ya aina
hiyo, imetokana na zinaa,” anasema Dk Mosha.
Takwimu hizo ni zile zilizopatikana kwa watu waliokwenda kufanyiwa uchunguzi katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Dk Mosha anasema kuwa wanaume ndiyo huathiriwa
zaidi na saratani ya mdomo ambapo kwa hapa nchini, asilimia 53 ya
wanaume waliofika MNH kwa ajili ya vipimo, walibainika kuugua saratani
hiyo, huku wanawake wakiwa ni asilimia 47.
Utafiti kama huo ulifanywa pia na Dk Amos
Mwakigonja, mkuu wa Idara ya Patholojia katika Chuo Kikuu cha Tiba cha
Muhimbili (MUHAS).
Dk Mwakigonja alifanya utafiti wa saratani ya
mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma ambapo wagonjwa 78 walibainika na
saratani hiyo kuanzia mwaka 1990 hadi 2003. “Saratani za mdomo zipo za
aina nyingi na zimetofautiana kulingana na visababishi vyake,” anasema
Dk Mwakigonja.
Katika utafiti wake Dk Mwakigonja alibaini kuwa
wanawake wengi walikuwa na saratani ya mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma
kuliko wanaume.
Hata hivyo, utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia
50 ya wanaume walikuwa na saratani ya mdomo hatari zaidi (systemic)
kuliko wanawake ambao ni asilimia 37.
Mapenzi kwa mdomo husababisha maradhi
Dk Mwakigonja anasema kuwa mapenzi yoyote kwa njia ya mdomo lazima yasababishe maradhi ya zinaa iwapo mmoja ameambukizwa.
Pia anasema kwamba sampuli nyingi za wanaume
wanaojihusisha na mapenzi na wanaume wenzao (mashoga) zilibainika na
saratani ya mdomo.
Utafiti huo ni sehemu ya utafiti wa Shahada ya
Uzamivu ambao ulionyesha kuwa wagonjwa wengi wa saratani ya mdomo
walikuwa ni wanaume wenye umri wa miaka kati ya 38 na kuendelea na
wanawake ni 31.
Ufatiti wa WHO Tanzania
Shirika la Afya Duniani (WHO) pia lilifanya
utafiti mwaka 2010 nchini kwa kushirikiana na Kituo cha Taarifa za HPV,
ambapo ilibainika kuwa asilimia 20 ya saratani za koo na mdomo nchini
zinasababishwa na ufanyaji wa mapenzi kwa njia ya mdomo.
Taarifa hizo za WHO zinaeleza kuwa wanaume 747
hugundulika na saratani ya mdomo kila mwaka wakati wanawake 472
hubainika na saratani hiyo pia.
Wakati huohuo, wanaume wanaopoteza maisha kutokana na saratani hiyo ni 444, kwa mwaka na wanawake ni 270, kwa mwaka.
Utafiti wa WHO umebaini kuwa saratani ya mdomo
inashika nafasi ya sita katika aina 24 za saratani 24 zinazoisumbua
zaidi Tanzania.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wanaume wanaoathirika
zaidi ni wenye umri wa kati ya miaka 15 na 55, ambao tayari wameshaanza
kujihusisha na ngono.
Kama maradhi mengine ya kuambukiza, Virusi vya HPV
huambukizwa kwa urahisi zaidi kutoka kwa wanawake kwenda kwa wanaume
kuliko kutoka kwa wanaume kwenda kwa wanawake.
Utafiti huo uliodhaminiwa na mfuko wa Bill na
Melinda Gates na Kituo cha Saratani na Mpango wa Utafiti wa Taasisi ya
ICO unaeleza kuwa mitandao ya kijamii na picha za ngono ndiyo chanzo cha
watu wengi kuiga ufanyaji wa mapenzi ya aina hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, tafiti zimefanyika
na kubaini kuwa asilimia 70 ya wagonjwa wanaobainika na saratani ya koo
na mdomo duniani, husababishwa na Virusi vya Human Pappiloma
vinavyotokana na magonjwa ya zinaa.
Tafiti hizo zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi
wanaogundulika na saratani hiyo ni wanaume wenye umri wa kati, wenye
uwezo wa kifedha, wasiovuta sigara wala siyo walevi waliokubuhu.
Utafiti huo ulibaini kuwa wanaume wapo hatarini zaidi kupata saratani ya koo inayosababishwa na Virusi vya HPV.
Miaka ya 80, idadi ndogo ya watu waliougua saratani ya koo walihusishwa na maambukizi ya Virusi vya HPV. Kihistoria, watu waliobainika na ugonjwa huo, ni
wenye umri wa miaka 70 kwenda juu ambao walikuwa ni wale walevi
waliokubuhu na wavuta sigara.
Ilielezwa kuwa Virusi vya HPV vipo kwa wingi kiasi
ambacho watu wazima wanaojihusisha na ngono ya aina yeyote ile, huweza
kupata maambukizi ya zinaa hata kama siyo saratani.
Hata hivyo ilibainishwa kuwa saratani
isababishwayo na virusi vya HPV ni rahisi kuitibu kuliko saratani ya koo
isababishwayo na tumbaku au pombe kali.
Virusi vya HPV ni nini?
Kwa jina la jumla, saratani ya koo au mdomo huitwa saratani ya kichwa na shingo. (Neck and Head Cancer)
HPV ni miongoni mwa virusi hatari zaidi duniani
visababishwavyo na magonjwa ya zinaa na vinaweza kuathiri sehemu
mbalimbali za mwili.
Zipo aina zaidi ya 120 za HPV, baadhi huweza
kuzalisha usugu (warts) ambazo si saratani katika sehemu za siri,
mikononi na miguuni.
Maambukizi ya HPV hufanyika kwa urahisi, hata kwa kugusana ngozi au majimaji, huku maambukizi mengine yakisababishwa na ngono.
Virusi hatari na vinavyosababisha saratani ni HPV-16, HPV-18, HPV-31 na HPV 45.
Aina hii ya Virusi vya HPV husababisha saratani
ambapo uvimbe waweza kujitokeza kwa ndani na unaweza usionekane
ukilinganisha na vivimbe vingine vya saratani.
Wataalamu wanasema HPV-16 na HPV-18 inahusishwa
zaidi na saratani ya shingo ya kizazi na endapo mapenzi kwa njia ya
mdomo yatafanywa na mtu mwenye uambukizo huu ni rahisi kuambukizwa.
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Ngono-kwa-njia-ya-mdomo-husababisha-saratani/-/1597578/1876252/-/y3laqcz/-/index.html