Tumekubali masharti ya wakubwa wetu tena bila kuwauliza. Tumekubali masharti ya jinsi ya kuendesha siasa zetu na jinsi ya kuendesha uchumi wetu. Tumekubali mapendekezo ya nini tufanye kwenye sheria zetu na tumebadilisha sheria kukidhi matakwa yao. Tumekubali mapendekeo yao ya mfumo wa uchumi, sera za mambo ya fedha na uendeshaji wa uchumi huo.
Tumekubali jinsi ya kulibadilisha jeshi letu la polisi kama tulivyofanya kwenye JWTZ. Mambo ambayo yasingeweza kutokea kwenye majeshi hayo wakati wa utawala wa Nyerere leo yanatokea na yanatokea gizani na mchana. Zamani tulikuwa na ujasiri wa kuchagua marafiki zetu na maadui zetu lakini leo marafiki zetu wanatuchagulia maadui zetu. Tumekubali.
Tumekubali jinsi gani Bunge letu liwe ili kuongeza demokrasia. Bila ya shaka leo tunaweza kusema tunaona Bungeni demokrasia zaidi na mfumo wa uwazi wa kutosha sana. Tumekubali ufadhili wao wa jinsi ya kuboresha shughuli za Bunge na siyo ufadhili tumekubali na mafunzo mbalimbali ambayo wanatupatia katika mabunge yao na nchi zao kwa ajili ya viongozi wetu. Tumekubali ukubwa wao na sisi tumeendelea kuwafuata.
Tumewakubalia wakubwa wa demokrasia - au ndivyo tunavyowadhani - kiasi kwamba demokrasia yetu tunaipima kwa macho yao na mitazamo yao. Mfumo wetu wa kisiasa unafanana kwa lugha na muundo kwa kiasi kikubwa na mifumo yao na wao wenyewe wametufadhili hadi kwenye demokrasia. Wanakuja na kutuambia jinsi ya kuendesha uchaguzi wetu na tukafuata na pamaja na hilo jinsi ya kuendesha siasa zetu. Wametupa warsha, makongamano, semina na mikutano ya kila aina nasi tumewakubalia tena tukicheka huku tukiwashukuru kwa kimombo - thank you so very much! Tunacheka na kuwachekea, tukichekelea na kuchekeana.Tumewakubali wageni watuambie nini cha kulima katika ardhi yetu tukiwakubalia masharti ya kulima huko huku tukiwakubalia maeneo makubwa ya ardhi yetu ili walime kwa ajili ya masoko na walaji wa kwao. Tumewakubalia hata kuwafukuza (wenyewe tunaita kuwahamisha) wananchi wetu ili wakubwa hawa waje na makampuni yao makubwa kulima, kuchimba na kufukua na kicha kuchukua wanachokitaka. Na hata tulipowaambia kuwa wananchi wetu wanaanza kukasirika wakatukubalia nini cha kupunguza na tukapunguza kwa masharti yao!
Tumewakubalia masharti yao ya uwekezaji na mikataba ya uwekezaji. Kuanzia kwenye madini, nishati na sasa kwenye gesi tumewakubalia. Wametutishia na kutuambia mikataba hiyo ni siri na kuwa tukiiweka hadharani wananchi wetu wakajua basi wao wataondoka na watawala wetu kama kasuku wenye njaa wanarudia maneno hao hayo hata bila kuyafikiria. Hivyo, tumekubali kuwaficha wananchi wetu tunayoyafanya kwa jina lao japo wao ndio wanalipa gharama ya kufanya kwa sababu hatuamini wanahitaji kujua. Hivyo, tumewakubalia wawekezaji wa kigeni mambo ambayo tunajua hatuwezi kuwakubalia wawekezaji wetu wa ndani na wenyewe tunaona furaha; bila haya, soni, wala hiyana tunawaambia wananchi wetu kuwa bila hawa wawekezaji watakufa njaa!
Viongozi wetu wamegeuzwa makuwadi wa mataifa ya nje wakiuza taifa lao kwa bei ya chee na kuuza hata vile visivyouzwa wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo watazidi kupendwa huko nje; na kupendwa wanapendwa. Hawakosi mialiko ya ulaji, na nafasi lukuki za kuonekana na wakubwa na wao wenyewe wanapokuja kwetu wanatuambia jinsi wanavyokubalika na hao wamiliki wa mawazo yao. Wanatuambia - watawala hao - kuwa hao wawekezaji ndio wanaotutakia mema na hivyo tusifanye mambo tusije tukawaudhi.
Hivyo tumewakubalia kama wazee ambao wanaletewa posa ya binti yao na japo mioyoni mwao wanasita kwa sababu wanajua vya kutosha juu ya huyo mchumba mshenga hata hivyo anasisitiza kuwa mchumba amejaa kichizi na atawajengea nyumba, kuwawekea mashine ya kusaga n.k Wanakubali japo wanajua huyo "mchumba" ameshaoa kwenye vijiji vya jirani na ahadi zote alizotoa huko hazijatimia na zile zilizotimizwa hazilinganishwi na gharama ya watoto wao walioolewa; wengi walishaachwa wakiwa na watoto, majeraha, na wakiwa! Tumewakubalia japo tunajua nini kitatokea huyo mchumba akishamaliza na taifa letu! Tunajua; tumekubali hata hivyo kwa sababu ndiye mtu anayeonesha kutupenda mno!
Hivyo, katika kukubali kwetu tulitarajiwa tuwe na furaha; tuwe na umoja tufurahie mema yote yanayotokana na kukubali kwetu. Katika kukubali kwetu tulirajiwa tuanze kuishi katika nchi imiminikayo maziwa na asali; kwamba baada ya kuwakubalia yote ambayo wakati wa Nyerere tuliwakatalia basi taifa letu litakuwa limeinuka na watu wetu wakiishi maisha ya utu zaidi na umaskini, magonjwa na ujinga vikifutika! Tumekubali masharti yao lakini matokeo yake tumekuwa ombaomba zaidi, tunawategemea zaidi, na kila kukicha tunawafikiria wao kama suluhisho la matatizo yetu. Na wao hawajachoka; wanakuja na masharti mengi zaidi, mbinu nyingi zaidi na matakwa mengi zaidi. Na wale waliokwisha kukubali awali hawawezi tena kukataa! Wakatae kwa msingi upi? Wenyewe wanalalamika pembeni lakini wakikaa nao mezani hutikisa vichwa kama waliopagawa wakikubali kwa kuitikia vichwa, mikono na midomo!
Furaha yetu iko wapi,
Umoja wetu uko wapi,
Mema waliliyotuahidia yako wapi,
Wanatuambia "hamyaoni"? Wanatuonesha vitu ambavyo wakubwa hao wametupatia wanasema "mbona hamvioni". Wanatuonesha mashule, ndege, barabara, hospitali, madaraja, nguo, tv, intaneti, radio na mitumba wanasema "hamuoni"?
Tunawauliza mbona hatuna furaha.
Wanasema na nyinyi hamkubali? Wanasema sisi ni wabishi na wachochezi, wanatukaripia na kutuapia kuwa watatushughulikia kwa nguvu ya mkono wa sheria. Wanasema hatuna shukrani kwa mema yote ambayo wao wametupatia kutoka kwa wakubwa zao! Wanatuona wasumbufu. Na kati yetu wapo ambao nao wanatuambia kwanini tunawasumbua wakubwa walioko serikalini; wanasema ati tunawapinga sana!
Najiuliza, mbona tulishakubali? Mbona wao walishasema tumekubali na wakafanya yote waliyoyafanya. Wamekuwa kama wacheza ngoma ambao wameahidiwa kutuzwa. Wanacheza, wanakatika, wanarembua na kujichekelesha, wanafuata kila aina mdungo, wanatingisha mabega, wanachezesha vichwa, wanapiga miluzi na filimbi. Kama wanaocheza lizombe wanatikisa lingwamba, huku wakicheza "jamani sepetula, sepetu!" Lakini wanapomaliza tunawauliza.
Mbona hatuna furaha!?
Wapo wenye furaha? Kwanini?
M. M. Mwanakijiji
Search This Blog
Friday, February 1, 2013
Tumefanya yote waliyotaka na ziada - mbona hatuna furaha, tunagombana na kukamiana...?
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment