Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano),
Stephen Wasira, ameitetea Idara ya Usalama wa Taifa dhidi ya tuhuma
zinazowahusu baadhi ya watendaji wake kuhusika katika matukio kadhaa ya utekaji
na utesaji wa raia.
Akizungumza bungeni jana jioni wakati wa kujibu hoja
mbalimbali zilizotolewa na wabunge waliochangia katika hotuba ya makadirio ya
bajeti ya mwaka 2013/14 ya Ofisi ya Rais, alisema haiwezekani kwa watumishi wa
idara hiyo kujihusisha na matukio hayo na kueleza mafanikio mbalimbali ambayo
idara hiyo imeliletea taifa.
Wasira akiwa ameuchapa usingizi Bungeni |
Alihoji sababu za kulihusisha tukio la kutekwa na kuteswa
kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda; na kuhoji
‘kwani yeye ni nani?.’
Wassira alisema haiwezekani idara hiyo ikahusika kwa kuwa
Kibanda hana umaarufu katika siasa za Tanzania na kusema kwamba labda wangekuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, na
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, angeelewa.
Kibanda alivamiwa na watu wasiojulikana wakati akirejea
nyumbani kwake, Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam Machi 5, mwaka huu.
Katika tukio hilo, watu hao walimng’oa meno, kumkata kidole
na kumharibu jicho la kushoto.
Hali hiyo ilisababisha Kibanda kulazwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH), baadaye katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), jijini
Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika
Kusini ambako anaendelea na matibabu zaidi hadi sasa.
Kibanda alifanyiwa unyama wa kutisha unaofanana na ule
aliofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, mwaka
jana.
Hata hivyo, pamoja na kwamba Inspekta Jenerali wa Polisi
(IGP), Said Mwema, ameunda timu ya makachero kuchunguza kutekwa kwa Kibanda,
hadi jana siku 45 tangu kutokea kwa unyama huo, hakuna taarifa za kukamatwa kwa
mtu yeyote.
Katika majumuisho ya jana, Wassira alitaja mafanikio ya
Usalama wa Taifa kwamba ni pamoja na kusaidia shughuli za ukombozi Kusini mwa
Afrika, kuzima njama za uhaini mapema miaka ya 80 na kutoa taarifa sahihi
zilizosaidia kukamatwa kwa watu waliohusika katika shambulio la kigaidi katika
ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998.
Pia alisema kuwa ni idara hiyo ilisaidia kufikiwa kwa kiini
cha ujambazi wa kupora mabenki nchini ambao ulikuwa umepamba moto sana nchini
miaka ya 2004-2006.
Wassira alisema Idara ya Usalama wa Taifa haiwezi kumfuata
na kumdhuru mtu yeyote isipokuwa anayepanga njama za uhaini dhidi ya
serikali. Akizungumzia udini, alisema
haujaleta athari kwa wananchi wa vijijini na mijini na kwamba bado waumini wa
madhehebu yote wanashirikiana katika mambo mbalimbali.
Hata hivyo, alisema katika baadhi ya matukio yaliyotokea
nchini katika miezi ya karibuni, serikali imechukua hatua kadhaa za kudhibiti
matukio hayo.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni kumkamata mtuhumiwa wa mauaji
ya Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili Zanzibar;
kuwakamata na kuwafungulia mashitaka watuhumiwa wa kuchoma makanisa Mbagala
mkoani Dar es Salaam pamoja na waliohusika katika vurugu za Geita na
kusababisha kifo cha mchungaji. Wassira
alisema kuwa hatua nyingine ni kukamata kanda za uchochezi katika baadhi ya
maeneo kama Dar es Salaam, Tanga, Simiyu na Mwanza na wahusika kukamatwa.
Alilitaka Bunge bila kujali itikadi za wabunge kukemea
vitendo vya uchochezi wa dini badala ya kuchochea.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment