Search This Blog

Friday, April 19, 2013

Darasa la saba sasa kujiunga vyuo vikuu

Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), imepanga kuanza kuwadahili wanafunzi wa kujiunga na masomo ya vyuo vikuu kwa kutumia uzoefu wao.
Udahili huo utakaoanza mwaka huu wa masomo 2013/14, utakuwa ukiwahusisha wale ambao elimu yao imeishia darasa la saba na kuendelea, lakini walikosa sifa ya kuendelea na masomo kwa ngazi ya chuo kikuu.
Kupitia utaratibu huo mpya, mtahiniwa atajiunga na Chuo Kikuu kulingana na fani atakayoiomba na atatakiwa kufanya mitihani mitatu na kufaulu kwa wastani wa daraja B.
Mkurugenzi wa Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu kutoka TCU, Dk Savinus Maronga aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kuona kuna watu wengi wanaopenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu, lakini wameshindwa kutokana na kutokuwa na vigezo, TCU imeamua kuanzisha mitihani hiyo maalumu.
Alisema kuwa mfumo huo unaojulikana kama ‘Recognition of Prior Learning’ (RPL), utamwezesha mwombaji kudahiliwa vyuoni kupitia tume hiyo kama wanavyofanya watahiniwa wengine.
Sifa zinazotakiwa
Kuhusu sifa za kujiunga, Dk Maronga alisema kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na umri kuanzia miaka 25 na kuendelea, sambamba na kuwa na elimu isiyopungua darasa la saba.
“Mwombaji anatakiwa kuwa na nia ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu na uzoefu wa kile ambacho anakusudia kukisoma.
Awe na uwezo wa kuandika na kusoma Lugha ya Kiingereza, ambayo ndiyo inayotumika kufundishia vyuoni,”alisema Dk Maronga na kuongeza:
“Kuna watu wameishia darasa la saba, lakini wamefanya kazi katika eneo moja, mfano karani wa mahakama, mwandishi wa habari kwa muda mrefu. Hivyo mfumo huu utawawezesha kuendelea na masomo bila tatizo.”
Vigezo
Mkurugenzi huyo alisema, kutakuwa na mitihani ya masomo matatu, ambayo mtahiniwa ili apate nafasi ya kuendelea na masomo ni lazima afaulu kwa wastani wa daraja B.
Alisema daraja la kwanza linaloanza na alama A ni 75-100, daraja B+ ni 60-75, B ni 50-59, C ni 40-49, D ni 35-39 na daraja E ni 0-34.
“Katika mitihani mitatu atakayoifanya, atatakiwa kupata wastani wa daraja ‘B’ na somo husika la fani yake atatakiwa kupata alama B ili kuwa na vigezo vya kupata cheti kitakachomwezesha kuendelea na masomo yake,”alisema Dk Maronga.

Alibainisha kuwa mitihani itakayokuwa ikitumika kudahili watahiniwa itakuwa ni wa somo la Kiingereza na Hisabati utakaokuwa na alama 30.
Mtihani wa Pili utakuwa na alama 30 ambao ni mtihani wa Maarifa na wa tatu utakuwa na alama 40, utakaokuwa ukitokana na fani husika ya mwombaji.
“Mfano mtahimiwa anataka kusomea sheria au uandishi wa habari, atatakiwa kufaulu kwa asilimia 50 somo husika, hivyo endapo atakosa kupata asilimia 50 ya somo lake hatapata cheti kitakachomwezesha kuendelea na elimu ya juu,”alisema Dk Marango na kuongeza:
“Cheti tutakachompatia mtahiniwa kitakuwa halali kwa kipindi cha miaka mitatu na baada ya hapo mwombaji atatakiwa kufanya upya mitihani hiyo.”
Viambatanisho
Kutokana na maelezo ya TCU, mwombaji anatakiwa kuambatanisha cheti cha kuzaliwa au hati ya kusafiria,wasifu wake pamoja na vyeti vya ushiriki mzuri kutoka sehemu anayofanyia kazi.
Vingine ni nakala za vyeti vya taaluma, picha ndogo ‘passport size, nakala za vyeti vya taaluma za masomo ya hapo awali, ripoti ya tathmini ya utendaji kazi wake kazini kwa walioajiriwa kutoka kwa mwajiri na nakala ya kozi za awali alizokwishafanya.
Vituo vya Mitihani
Mkurugenzi huyo alisema mitihani itafanyika kati ya Mei na Juni mwaka huu katika vituo vinne vilivyoandaliwa katika vyuo.
Alisema kuwa chini ya mfumo huo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kitahusika na masuala ya Elimu huku Chuo Kikuu Tumaini Makumira cha Dar es Salaam (TUMADARCo) kikihusika na Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma.
Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), kitahusika na Kilimo na Wanyamapori wakati Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU) kitahusika na masuala ya usimamizi na utawala,uhasibu, sheria na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).
“Kwa kuwa ndiyo tunaanza, tumeamua kutenga vituo vinne, lakini mwakani tunatarajia kuongeza viwe vingi ili kukidhi mahitaji ya wananchi walio wengi,”anasema Dk Maronga.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/1753450/-/item/0/-/u5m88u/-/index.html

No comments:

Post a Comment