Search This Blog

Wednesday, March 13, 2013

Sasa ni Papa Francis I !

Papa Francis ahutubu mara ya kwanza
Kadinali Jorge Mario Bergoglio wa Argentina amechaguliwa kuwa Papa mpya wa Kanisa Katoliki.
Kadinali Bergoglio anakuwa mtu wa kwanza kutoka Amerika kusini kuchaguliwa kuwa Papa.
Mara tu baada ya kuchaguliwa alichagua jina la Papa Francis I.
Awali moshi mweupe ulishuhudiwa ukifuka kutoka bomba la kutolea moshi katika kanisa la Sistine Chapel na kufuatiwa na kengele kupigwa. Hii ilikuwa ni ishara kwa walimwengu kuwa makadinali ambao walianza mchakato wa kumchagua Papa mpya hatimae walikuwa wamefaulu katika kazi yao.
Kadinali Bergoglio anachukuwa mahali pa Papa Benedict XVI, ambaye alijiuzulu mwezi uliopita akisema hana nguvu na uwezo wa kuendelea kuliongoza Kanisa Katoliki.
Makadinali 115 wamekuwa faraghani tangu siku ya Jumanne alasiri na wakaanza mchakato wao kwa kupiga kura mara nne kwa siku.
Ilikuwa inahitajika kuwa angalau Makadinali 77 yaani theluthi-mbili wangeliweza kumpigia kura mmoja wao ili aweze kutangazwa kuwa Papa mpya.
Na kabla ya mchakato huo kuanza kulikuwa hakuna dalili za kuonyesha nani angelichaguliwa.
Moshi mweupe
Maelfu ya watu kutoka sehemu mbali mbali duniani walikwa wamekusanyika katika ukumbi wa Kanisa la St Peter tangu siku ya Jumanne.
Muda mfupi kabla ya Kadinali Bergoglio kujitokeza , maelfu ya watu walionekana wakikimbia kuelekea ukumbi wa St Peters ili kuweza kumshuhudia Papa mpya akitangazwa .

 Papa Francis I ni nani?

Alizaliwa Mjini Buenos Aires huko Argentina mwaka1936.
Papa Francis 1 ni mtu wa kwanza katika kipindi cha miaka elfu moja (1,000) kwa mtu kutoka nje ya bara la Ulaya kutawazwa kuwa papa wa Kanisa Katoliki.
Papa Francis 1 ni mwana wa Mtaliano aliyekuwa akifanya kazi katika shirika la gari Moshi kabla ya kuhamia nchini Argentina miaka ya zamani.
Kama kadinali wa Jimbo la Buenos Aires, Kadinali Bergoglio amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Argentina.
Hata hivyo Kadinali Bergoglio anapendwa sana na wafuasi wa kanisa hilo huko Argentina na hasa watu maskini. Kadinali Jorge Bergoglio, mwenye umri wa mwaka 76, kwa karibu miaka yake yote kama Kasisi amehudumu nyumbani kwao Argentina.
Kadinali huyo wa Jimbo la Buenos Aires inasemekana aliibuka nambari mbili wakati Papa Benedict alipochaguliwa mwaka 2005.
Papa Francis akijitokeza
Anaaminika kuwa na ujuzi mkubwa ambao wengi wanasema utamsaidia sana katika uongozi wake.
Katika maisha yake ya huduma kwa Kanisa Katoliki huko Amerika Kusini ambapo Kanisa Katoliki lina waumini wengi zaidi duniani, Kadinali Bergoglio ameibuka kuwa mtu anayependa sana udhabiti wa kisiasa katika nchi zilizo katika bara la Amerika Kusini.
Bergoglio anasifiwa kwa kuleta mageuzi makubwa katika Kanisa la Argentina huku katika eneo hilo la Amerika Kusini Kanisa bado linashikilia itikadi za kale.

Thursday, March 7, 2013

Wateswe au wauawe wangapi ndipo tustuke?

Na Ndimara Tegambwage
Kibanda baada ya kushambuliwa
MWANDISHI wa habari Absalom Kibanda, amevamiwa. Akapigwa. Akachokonolewa jicho. Akachomolewa kucha. Akakatwa kidole. Akang’olewa meno. Akaachwa kufa nje ya lango la nyumba yake iliyoko mtaa wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
 
Ni usiku wa kuamkia jana, Jumatano. Hivi sasa Kibanda, mhariri mkuu mtendaji wa New Habari Media Group – kampuni inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai na The African, yuko taabani kitandani.
 
Aliyofanyiwa Kibanda ni yaleyale aliyofanyiwa Dk. Steven Ulimboka, kiongozi wa madaktari katika mgomo mkuu wa mwaka jana wa kushinikiza serikali kuweka mazingira bora ya kazi katika hospitali zake kwa kununua vifaa, dawa na kutoa mishahara inayostahili.
 
Katulanda akionyesha majeraha ya kushambuliwa kwake
Akang’olewa meno na kucha; akatupwa kwenye msitu wa Mabwepande, kilometa 45 nje ya jiji la Dar es Salaam. Aliponea chupuchupu.Dk. Ulimboka aliburutwa kwenye lami. Akakunjwakunjwa kama godoro na kuingizwa kwenye gari dogo. Akapigwa mara kwa mara kwa fimbo, makofi na mateke.
 
Kwahiyo, mbinu zilizotumika kumtesa Kibanda siyo mpya. Zimewahi kutumiwa. Unaweza kusema haraka kuwa waliomtesa mwandishi, ama wamesomea chuo kimoja au ni walewale waliomtesa Dk. Ulimboka.
 
Je, baada ya Kibanda, nani? Lakini kabla ya Kibanda, nani? Mwaka 2008, watu watatu wakiwa na panga, chupa yenye tindikali na gongo la mti, walivamia chumba cha habari cha gazeti la MwanaHALISI tulimokuwa tumebaki wawili.
 
Walifanikiwa kummwagia tindikali machoni, mwandishi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayochapisha gazeti hilo, Saed Kubenea. Hakupofuka kabisa lakini lazima aende India kila baada ya miezi minne kuchunguzwa macho.
 
Nakumbuka kunyukana na vijana wawili – mmoja mwenye panga na mwingine mwenye gongo – hadi panga lililolenga katikati ya kichwa lilipokoseshwa shabaha, kutua kwenye kisogo kulia na kudondokea nyuma yangu. Nilishonwa nyuzi 15. Nani alikuwa amewatuma?
 
Desemba 2009, mwandishi Frederick  Katulanda wa Mwanza, alivamiwa nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza sauti na kudai kuwa ana nyaraka za akaunti za benki za halmashauri ya jiji la Mwanza.
 
Walikuwa na mapanga. Walikuwa wakichagizana kwa kusema, “Kata kichwa! Kata kichwa!” Waliondoka na mafaili. Walimwachia kilema mguuni na makovu mikononi.
 
Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi wa jiji la Mwanza, walikusanywa na kufanya maandamano makubwa kwa walichoita “kupinga mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo” na kudai kwamba alikuwa Mkenya na “siyo raia wa Tanzania.”  
 
Hii ilikuwa baada ya filamu iitwayo “Darwin’s Nightmare” kuonyesha jinsi wananchi wakazi wa jiji wanavyokula mapanki badala ya samaki.
 
Mgamba alidaiwa kuwabeba watengeneza filamu na kuwaonyesha maeneo ambako kweli kunguru na binadamu walikuwa wanagombea mabaki (mifupa) ya samaki baada ya viwanda kunyofoa minofu ya kuuza Ulaya. Mgamba alilazimika kuwa “mkimbizi” jijini Dar es Salaam.
 
Sept 2010 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, katika eneo la Nyambiti, jimbo la Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, mwandishi Frederick Katulanda alivamiwa na kupigwa na watu wapatao 15 waliojiita “Green Guard” – wa “chama cha kijani.”
 
Katika “kumshughulikia,” Katulanda anasema, walikuwa wakionyesha kuwa na ujuzi mkubwa wa judo na karate huku wakidai kuwa anawaandika “vibaya” Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Mwaka 2011 mwandishi Richard Massatu alikutwa amekufa katika eneo la Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari viliripoti kuwa macho yake yalikuwa yametobolewa na kuwekwa gundi aina ya super glue; mguu wa kushoto na mbavu vilikuwa vimevunjika.
 
Vyombo vya habari viliripoti kuwa Massatu aliyekuwa mmiliki na mhariri mkuu wa gazeti la Kasi Mpya (sauti ya umma), alionekana mara ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa na maofisa wa polisi na usalama katika baa iitwayo Cross Park katika eneo la Igoma.
 
Daudi Mwangosi, mwandishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten aliuawa kwa kupigwa risasi katikati na mikononi mwa polisi na hasa mbele ya mkuu wa polisi wa mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
 
Hii ilikuwa tarehe 2 Septemba mwaka jana. Kesi bado iko mahakamani. Picha zinazoonyesha Mwangosi alivyolipuliwa, zinatia simanzi kwa kila anayethamini utu.
 
Mwaka huu, tarehe 3 Januari, maiti ya mwandishi Issa Ngumba iliokotwa katika pori la mlima Kajuruheta, kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko katika mkoa wa Kigoma.
 
Ngumba alikuwa mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Alikutwa amekufa baada ya kutoweka nyumbani kwa siku tatu.
 
Mwandishi wa habari Erick Kabendera anayeishi Dar es Salaam, anaishi kwa wasiwasi. Wazazi wake waishio Bukoba, wamehojiwa na “ofisa usalama” kwa kile kilichoitwa “uhalali wa uraia wao.”
 
Kabendera, ambaye ncha ya kalamu yake haipindwi kwa woga wala upendeleo, amekuwa akiripoti kupigiwa simu na kutishiwa kwamba “atarudishwa kwao.” Naye hajui kwao kwingine isipokuwa Tanzania.
 
Juzi, Jumanne, mwandishi Charles Misango wa TanzaniaDaima, alishindwa kurudi nyumbani kwake, Kimara nje kidogo ya Dar es Salaam.
 
Kwa siku nzima familia yake ilishinda ikiripoti watu tofauti waliokuwa wakifika nyumbani kwake wakimuulizia na wengine kuzengea nyumba tu.
 
“Nilipomwambia mhariri wangu juu ya hali hiyo, aliniambia ‘usiwe mjinga; nenda ukalale hotelini.’ Nilikwenda kwa rafiki yangu mwenye ua mkubwa, nikaegesha gari na kulala katika gari langu kwa kuwa alikuwa na wageni wengi,” anasimulia Misango.
 
Misango ni mmoja wa wahariri wanaokabiliwa na tuhuma za “kuandika uongo.” Kesi yao iko mahakamani jijini Dar es Salaam.
 
Kuna orodha ndefu ya waandishi wa habari waliotishwa na wanaoendelea kutishwa; waliopigwa na polisi na askari magereza (Ukonga, Dar es Salaama) kwa tuhuma mbalimbali; waliotishiwa maisha kwa simu na hata kwa kufuatiliwa na watu wasiowafahamu.
 
Miezi mitatu iliyopita, ilivumishwa kuwa Ansbert Ngurumo, mhariri mtendaji wa sasa wa TanzaniaDaima amefariki. Taarifa hii ilipelekwa pia kwenye mtandao mpana na unaoheshimika wa Jamii Forum (JF).
 
Hakuna ajuaye kama hakukuwa na nia ya kuua au kudhuru Ngurumo. Livumalo lipo na Ngurumo alipewa ushauri wa “kuwa makini” kwani kila uvumi una shina lake.
 
Ngurumo amekuwa muwazi siku zote kuelezea jinsi baadhi ya walioko madarakani walivyoshindwa kumshawishi kuwapenda, kuwanyenyekea na hata kufanyakazi nao. 
 
Tatizo lililopo ni kwamba kila janga lilipotokea, baadhi ya waandishi walijitenga na kusema, “Shauri yao, nao wamezidi.” Nani amezidi wapi? Kumekuwa na tabia ya kujitenga na kubaguana.
 
Huko tuendako, baada ya kujikata kutoka shina kuu la wanataaluma, tunakuwa kama vifaranga vya kuku visivyo na ulinzi wa mbawa wala kelele za mama. Tunajianika mmojammoja kwa mwewe kututafuna mmoja baada ya mwingine. Tutaisha!
 
Nani atalinda maisha ya waandishi wa habari Tanzania? Tayari mmoja yuko kariku kufa kwa woga. Aliwaambia wenzake jana kwenye viwanja vya hospitali ya Muhimbili (MOI), “Labda tutafute makazi nje hadi mwisho wa utawala wa awamu hii nne…”
 
Huu ni woga, labda ni upumbavu pia. Kwamba kumekuwa na taarifa za madai ya kuua waandishi wawili maarufu wa habari na wanasiasa wawili mashuhuri; siyo sababu ya kukimbia nchi.
 
Kuwa na umoja katika taaluma, kuandika zaidi na hasa kuandika ukweli; kuchunguza, chambua na kufafanua zaidi – kuweka jamii wazi juu ya kinachoendelea – hivi vinaweza kuwa ngao kuu kwetu sasa na huko tuendako.
 
Bali tujenge mashaka juu ya mfanano wa mbinu za kutesa na kuua. Watesaji na wauaji waweza kuwa watu walewale. Wako wapi? Tuwasake na kuwaanika. Tunaweza katika umoja wetu.

Source:http://ndimara.blogspot.com/2013/03/kutekwa-na-kuteswa-kwa-absalom-kibanda.html

Wednesday, March 6, 2013

ABSALOM KIBANDA AVAMIA NA KUSHAMBULIWA VIBAYA

TASWIRA ZA ABSALOM KIBANDA AKIWA HOSPITALINI MUHIMBILI BAADA YA KUVAMIWA NA KUUMIZWA VIBAYA

Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi, akimjulia hali Absalom Kibanda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Magazeti ya Habari Corporation, Hussein Bashe, akimpa pole Kibanda.
Kibanda akiwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).
 Wanahabari wakimjulia hali Kibanda pamoja na kupata machache kutoka kwake.
Kibanda akiendelea kupata matibabu ICU.
Dk. Reginald Mengi (kushoto) akibadilishana mawazo na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Waziri wa Afya Dk. Hussein Mwinyi akibadilishana mawazo na Prof. Lawrence Maseru wa MOI.
Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi (kulia) akimpa pole, Afisa Mtendaji Mkuu wa Magazeti ya Habari Corporation, Hussein Bashe.Baadhi ya majeraha aliyoyapata Kibanda.
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Habari Corporation, Absalom Kibanda, usiku wa kuamkia leo amevamiwa na watu wasiojulikana wakati akivuka geti kuingia nyumbani kwake na gari yake aina ya Nissan.
Wavamizi hao walivunja kioo cha gari lake na kumchomoa ambapo walimpiga mapanga na kumjeruhi vibaya jicho la kushoto. Baada ya kufanyiwa unyama huo Kibanda alikimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi ‘ICU’.
(PICHA ZOTE : RICHARD BUKOS NA HARUNI SANCHAWA / GPL)