Search This Blog

Saturday, June 1, 2013

UTATA KIFO CHA AFISA USALAMA KIJITONYAMA

Utata umeibuka kuhusiana na kifo cha Ofisa Usalama wa Taifa, Peter Tyenyi, ambaye mwili wake umekutwa ndani ya kisima cha maji kilichopo eneo la ofisi za idara zilizopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa njia ya simu, msemaji wa familia ambaye ni kaka wa marehemu, John Tyenyi alisema mwili wa Peter (53) ulikutwa juzi ukiwa ndani ya kisima cha maji kilicho ndani ya eneo la Ofisi za Usalama wa Taifa, Kijitonyama baada ya kutoweka tangu Jumatatu ya Mei 27, alipoaga kwenda kazini.
“Peter alitoweka tangu Jumatatu alipoaga kwenda kazini. Mimi nimepigiwa simu jana saa tano asubuhi nikiwa Mombasa nchini Kenya kwamba amepatikana akiwa ndani ya shimo la maji,” alisema John.
Baadhi ya ndugu zake waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina wakiwa msibani Kigamboni jijini Dar es Salaam, walisema kuwa baada ya ndugu yao kutoweka mkewe Joyce Mwakilama aliwataarifu na kuwasiliana na ofisi yake, lakini aliambiwa kuwa hata huko hayupo.
“Tuliwajulisha Usalama wa Taifa wakasema hata wao hawajui. Lakini jana (juzi) wakatupigia simu kuwa amekutwa kwenye kisima cha maji baada ya kutokea shida ya maji,” alisema mmoja wa wanafamilia kwa sharti la kutotajwa jina na kuongeza:
“Walisema kuwa kisima hicho huwa kinalindwa, lakini tunashangaa ndugu yetu aliingiaje humo.”
Ndugu mwingine alisema: “Awali tuliambiwa kuwa ndugu yetu yuko Muhimbili, tukaenda kuulizia tukamkosa. Baadaye tukaambiwa yuko hospitali ya Lugalo, huko tukamkuta ameshaandaliwa kwa mazishi. Tulipouliza tukaambiwa kibali cha kuzika kiko tayari na usafiri wa ndege uko tayari tujiandae kusafirisha.”
Hata hivyo, msemaji wa familia John Tyeni alisema kuwa ndugu hao walipinga kuusafirisha mwili huo, hadi ufanyiwe uchunguzi (post mortem).
Mkurugenzi Usalama wa Taifa katikakati
“Tulipokwenda hospitali tukakuta maofisa usalama wamemchukua OCD wa Wilaya ya Kinondoni Wilbrod Mutangungwa na askari wawili na kwenda kufanya post mortem. Yaani kulikuwa na ujanja ujanja unafanyika. Sisi tukamchukua Ofisa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, RCO Kimola na askari wawili na wapigapicha ndiyo tukafanya post mortem,” alisema John.
Akizungumzia matokeo ya uchunguzi huo, John alisema kuwa watapewa matokeo hayo baada ya kutoka kwenye mazishi yatakayofanyika Musoma mjini mkoani Mara, baada ya kusafirishwa leo.
Hata hivyo alisema kuwa macho yake yalikuwa yametoka nje kwa sababu ya kujaa maji.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walidai kuwa mwili wake ulikutwa ukiwa umetumbuliwa macho huku nguo na viatu vikiwa bado mwilini.
Akizungumzia kifo hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alikiri kutokea tukio hilo na kusema kuwa bado uchunguzi unaendelea.
“Ni kweli kuna ofisa usalama amefariki ndani ya kisima, lakini bado tunachunguza. Kwa sababu itabidi tupate taarifa ya daktari ndiyo tuunganishe na uchunguzi wetu,” alisema Kenyela.
SOURCE: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kifo-cha-Ofisa-Usalama-chazua-utata/-/1597578/1868848/-/ahqc99/-/index.html

No comments:

Post a Comment