Na
Ndimara Tegambwage
|
Kibanda baada ya kushambuliwa |
MWANDISHI wa habari Absalom Kibanda, amevamiwa.
Akapigwa. Akachokonolewa jicho. Akachomolewa kucha. Akakatwa kidole.
Akang’olewa meno. Akaachwa kufa nje ya lango la nyumba yake iliyoko mtaa wa
Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Ni usiku wa kuamkia jana, Jumatano. Hivi sasa
Kibanda, mhariri mkuu mtendaji wa New Habari Media Group – kampuni
inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai na The African, yuko taabani
kitandani.
Aliyofanyiwa Kibanda ni yaleyale aliyofanyiwa Dk.
Steven Ulimboka, kiongozi wa madaktari katika mgomo mkuu wa mwaka jana wa kushinikiza
serikali kuweka mazingira bora ya kazi katika hospitali zake kwa kununua vifaa,
dawa na kutoa mishahara inayostahili.
|
Katulanda akionyesha majeraha ya kushambuliwa kwake |
Akang’olewa meno na kucha; akatupwa kwenye
msitu wa Mabwepande, kilometa 45 nje ya jiji la Dar es Salaam. Aliponea
chupuchupu.Dk. Ulimboka aliburutwa kwenye lami.
Akakunjwakunjwa kama godoro na kuingizwa kwenye gari dogo. Akapigwa mara kwa
mara kwa fimbo, makofi na mateke.
Kwahiyo, mbinu zilizotumika kumtesa Kibanda siyo
mpya. Zimewahi kutumiwa. Unaweza kusema haraka kuwa waliomtesa mwandishi, ama
wamesomea chuo kimoja au ni walewale waliomtesa Dk. Ulimboka.
Je, baada ya Kibanda, nani? Lakini kabla ya
Kibanda, nani? Mwaka 2008, watu watatu wakiwa na panga, chupa yenye tindikali
na gongo la mti, walivamia chumba cha habari cha gazeti la MwanaHALISI tulimokuwa
tumebaki wawili.
Walifanikiwa kummwagia tindikali machoni,
mwandishi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayochapisha gazeti hilo, Saed
Kubenea. Hakupofuka kabisa lakini lazima aende India kila baada ya miezi minne kuchunguzwa
macho.
Nakumbuka kunyukana na vijana wawili – mmoja
mwenye panga na mwingine mwenye gongo – hadi panga lililolenga katikati ya
kichwa lilipokoseshwa shabaha, kutua kwenye kisogo kulia na kudondokea nyuma
yangu. Nilishonwa nyuzi 15. Nani alikuwa amewatuma?
Desemba 2009, mwandishi Frederick Katulanda wa Mwanza, alivamiwa nyumbani.
Wavamizi walikuwa wakipaza sauti na kudai kuwa ana nyaraka za akaunti za benki
za halmashauri ya jiji la Mwanza.
Walikuwa na mapanga. Walikuwa wakichagizana kwa
kusema, “Kata kichwa! Kata kichwa!” Waliondoka na mafaili. Walimwachia kilema
mguuni na makovu mikononi.
Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi wa jiji la
Mwanza, walikusanywa na kufanya maandamano makubwa kwa walichoita “kupinga
mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo” na kudai kwamba alikuwa Mkenya na
“siyo raia wa Tanzania.”
Hii ilikuwa baada ya filamu iitwayo “Darwin’s
Nightmare” kuonyesha jinsi wananchi wakazi wa jiji wanavyokula mapanki badala
ya samaki.
Mgamba alidaiwa kuwabeba watengeneza filamu na
kuwaonyesha maeneo ambako kweli kunguru na binadamu walikuwa wanagombea mabaki
(mifupa) ya samaki baada ya viwanda kunyofoa minofu ya kuuza Ulaya. Mgamba alilazimika
kuwa “mkimbizi” jijini Dar es Salaam.
Sept 2010 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu,
katika eneo la Nyambiti, jimbo la Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza,
mwandishi Frederick Katulanda alivamiwa na kupigwa na watu wapatao 15
waliojiita “Green Guard” – wa “chama cha kijani.”
Katika “kumshughulikia,” Katulanda anasema, walikuwa
wakionyesha kuwa na ujuzi mkubwa wa judo na karate huku wakidai kuwa
anawaandika “vibaya” Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwaka 2011 mwandishi Richard Massatu alikutwa
amekufa katika eneo la Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari viliripoti kuwa
macho yake yalikuwa yametobolewa na kuwekwa gundi aina ya super glue; mguu wa
kushoto na mbavu vilikuwa vimevunjika.
Vyombo vya habari viliripoti kuwa Massatu aliyekuwa
mmiliki na mhariri mkuu wa gazeti la Kasi
Mpya (sauti ya umma), alionekana mara ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa
na maofisa wa polisi na usalama katika baa iitwayo Cross Park katika eneo la
Igoma.
Daudi Mwangosi, mwandishi wa kituo cha televisheni
cha Channel Ten aliuawa kwa kupigwa
risasi katikati na mikononi mwa polisi na hasa mbele ya mkuu wa polisi wa mkoa
wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Hii ilikuwa tarehe 2 Septemba mwaka jana. Kesi
bado iko mahakamani. Picha zinazoonyesha Mwangosi alivyolipuliwa, zinatia
simanzi kwa kila anayethamini utu.
Mwaka huu, tarehe 3 Januari, maiti ya mwandishi
Issa Ngumba iliokotwa katika pori la mlima Kajuruheta, kijiji cha Mhange,
wilayani Kakonko katika mkoa wa Kigoma.
Ngumba alikuwa mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Alikutwa amekufa baada ya
kutoweka nyumbani kwa siku tatu.
Mwandishi wa habari Erick Kabendera anayeishi Dar
es Salaam, anaishi kwa wasiwasi. Wazazi wake waishio Bukoba, wamehojiwa na
“ofisa usalama” kwa kile kilichoitwa “uhalali wa uraia wao.”
Kabendera, ambaye ncha ya kalamu yake haipindwi
kwa woga wala upendeleo, amekuwa akiripoti kupigiwa simu na kutishiwa kwamba
“atarudishwa kwao.” Naye hajui kwao kwingine isipokuwa Tanzania.
Juzi, Jumanne, mwandishi Charles Misango wa TanzaniaDaima, alishindwa kurudi
nyumbani kwake, Kimara nje kidogo ya Dar es Salaam.
Kwa siku nzima familia yake ilishinda ikiripoti
watu tofauti waliokuwa wakifika nyumbani kwake wakimuulizia na wengine kuzengea
nyumba tu.
“Nilipomwambia mhariri wangu juu ya hali hiyo,
aliniambia ‘usiwe mjinga; nenda ukalale hotelini.’ Nilikwenda kwa rafiki yangu
mwenye ua mkubwa, nikaegesha gari na kulala katika gari langu kwa kuwa alikuwa
na wageni wengi,” anasimulia Misango.
Misango ni mmoja wa wahariri wanaokabiliwa na
tuhuma za “kuandika uongo.” Kesi yao iko mahakamani jijini Dar es Salaam.
Kuna orodha ndefu ya waandishi wa habari waliotishwa
na wanaoendelea kutishwa; waliopigwa na polisi na askari magereza (Ukonga, Dar
es Salaama) kwa tuhuma mbalimbali; waliotishiwa maisha kwa simu na hata kwa
kufuatiliwa na watu wasiowafahamu.
Miezi mitatu iliyopita, ilivumishwa kuwa Ansbert
Ngurumo, mhariri mtendaji wa sasa wa TanzaniaDaima
amefariki. Taarifa hii ilipelekwa pia kwenye mtandao mpana na unaoheshimika wa Jamii Forum (JF).
Hakuna ajuaye kama hakukuwa na nia ya kuua au
kudhuru Ngurumo. Livumalo lipo na Ngurumo alipewa ushauri wa “kuwa makini”
kwani kila uvumi una shina lake.
Ngurumo amekuwa muwazi siku zote kuelezea jinsi
baadhi ya walioko madarakani walivyoshindwa kumshawishi kuwapenda,
kuwanyenyekea na hata kufanyakazi nao.
Tatizo lililopo ni kwamba kila janga lilipotokea,
baadhi ya waandishi walijitenga na kusema, “Shauri yao, nao wamezidi.” Nani
amezidi wapi? Kumekuwa na tabia ya kujitenga na kubaguana.
Huko tuendako, baada ya kujikata kutoka shina kuu
la wanataaluma, tunakuwa kama vifaranga vya kuku visivyo na ulinzi wa mbawa
wala kelele za mama. Tunajianika mmojammoja kwa mwewe kututafuna mmoja baada ya
mwingine. Tutaisha!
Nani atalinda maisha ya waandishi wa habari
Tanzania? Tayari mmoja yuko kariku kufa kwa woga. Aliwaambia wenzake jana
kwenye viwanja vya hospitali ya Muhimbili (MOI), “Labda tutafute makazi nje hadi
mwisho wa utawala wa awamu hii nne…”
Huu ni woga, labda ni upumbavu pia. Kwamba
kumekuwa na taarifa za madai ya kuua waandishi wawili maarufu wa habari na
wanasiasa wawili mashuhuri; siyo sababu ya kukimbia nchi.
Kuwa na umoja katika taaluma, kuandika zaidi na
hasa kuandika ukweli; kuchunguza, chambua na kufafanua zaidi – kuweka jamii wazi
juu ya kinachoendelea – hivi vinaweza kuwa ngao kuu kwetu sasa na huko
tuendako.
Bali tujenge mashaka juu ya mfanano wa mbinu za kutesa
na kuua. Watesaji na wauaji waweza kuwa watu walewale. Wako wapi? Tuwasake na
kuwaanika. Tunaweza katika umoja wetu.
Source:http://ndimara.blogspot.com/2013/03/kutekwa-na-kuteswa-kwa-absalom-kibanda.html