Search This Blog
Wednesday, August 7, 2013
Tendwa: Nilifanya kazi vyema kwa mujibu wa sheria
Siku moja baada ya kutangazwa rasmi kwamba aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amestaafu kwa mujibu wa sheria, amejitokeza na kueleza yaliyo moyoni mwake.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Harare jana, Tendwa alisema amepokea kwa mikono miwili kustaafu kutoka katika nafasi hiyo nyeti katika siasa za Tanzania, huku akisema anajiona mwenye bahati kufanya kazi na marais wawili katika nafasi yake.
John Tendwa
Tendwa amefanya kazi chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na baadaye Rais Jakaya Kikwete. Nafasi ya Tendwa, imechukuliwa na Jaji Francis Mutungi ambaye alikuwa jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Akizungumzia kuhusu viongozi wa vyama vya upinzani kupokea kwa nderemo kustaafu kwake, Tendwa alisema wala hashangai kuyasikia hayo kwani inaonyesha kwamba kazi yake alikuwa akiifanya vyema na mujibu wa sheria.
“Unajua unapokuwa msajili na ukaona wadau wote wanakushangilia hapo ujue kuna tatizo kubwa, nimekuwa ninafanya kazi yangu vizuri sana kwa kuzingatia misingi ya sheria ambayo imewekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni,”alisema Tendwa.
Alisema kwamba, “Unajua kuvilea vyama ni kazi kubwa sana ndugu yangu, maana kuna wakati hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wanasema ninaegemea na kuvipendelea sana vyama vya upinzani. Leo nimestaafu nasikia vyama vya upinzani vinasema kwamba nilikuwa nawapendelea CCM, hiyo inaonyesha kwamba nilikuwa ninafanya kazi yangu sawa sawa.”
Kitu gani ambacho Tendwa hatakisahau?
Alisema kwamba katika miaka yake 13 ambayo amekuwa msajili hatomsahau waziri mmoja wa CCM.
Hata hivyo, Mwananchi lilimbana kumtaja waziri huyo, lakini agoma kwa madai kwamba hapendi kuendeleza malumbano naye baada ya kustafu kwake utumishi wa umma.
Tendwa alisema katika utumishi wake, waziri huyo alikuwa akimpatia wakati mgumu sana kwa kumpakazia kwamba yeye ni mpinzani.
“Katika miaka yangu 13 ofisini sitaweza kumsahau huyo waziri maana alikuwa ananipakazia kwamba mimi ni mfuasi wa vyama vya upinzani. Ninamshukuru Mungu kwamba baadaye alikuja kuniomba msamaha, lakini ilikuwa imenisumbua sana katika kazi zangu,” alisema huku akionyesha masikitiko
Kwa nini vyama vinashuka?
Kuhusu kushuka na kupanda kwa vyama vya siasa hasa vile vya upinzani nchini baada ya uchaguzi kumalizika, Tendwa alisema katika kipindi chake cha uongozi aligundua kuwa migogoro ndani ya vyama hivyo ndio chanzo kikubwa cha kupoteza mvuto kwa wananchi.
“Tatizo la vyama vingi vya upinzani Tanzania vinadhani kuwapata wabunge basi ndio vinakuwa vimechukua Serikali, vinasahau kujizatiti na kujipambanua mbele ya macho ya wapigakura kuwa vinasimamia kitu gani, badala yake nimekuwa vikiishia kwenye migogoro isiyo ya lazima,” alisema Tendwa.
Tendwa alielezea jinsi ambavyo NCCR-Mageuzi ilivyokuwa na nguvu sana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, lakini baada ya kuingia kwenye migogoro chama hicho kikapoteza mvuto.
“Badala ya kujiingiza kwenye migogoro vinatakiwa kujipanga kisayansi, lazima wajue kwamba siasa ni sanyasi,” alisema.
Alisema hata CUF kilianza kupoteza mvuto kwa jamii baada ya kupata wabunge na kuanza kuibuka migogoro ya ndani.
Jambo la kujivunia
Tendwa alisema anajivunia kitengeneza muundo wa ofisi ambayo inazingatia maadili.
Alisema wakati anakabidhiwa ofisi alikuwa peke yake ndiye mwanasheria mwenye kiwango cha shahada ya chuo kikuu, lakini hivi sasa msajili mteule atakuta zaidi ya wanasheria 16 katika ofisi zote tano za kanda pamoja na makao makuu.
Pia alisema aliweza kuleta nidhamu ya matumizi ya fedha pamoja na kuleta weledi katika kujenga misingi imara ya ofisi hiyo ambayo imekabidhiwa jukumu kuvisimamia na kuvilea vyama vya siasa nchini.
Ushauri kwa mrithi wake
Tendwa alisema hawezi kumfundisha kazi Jaji Mutungi kwani anaamini atafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na taratibu kama ambavyo miongozo inavyotaka.
“Mutungi atafanya kazi kwa mujibu wa sheria, siku zote atafuata sheria na kutafsiri sheria maana yeye ni Jaji. Ninawaomba wadau wampatie ushirikiano maana sasa anakuja kufanya kazi na wanasiasa,” alisema Tendwa.
Alisema endapo Jaji Mutungi ataanza kubezwa na wanasiasa anatakiwa kujua ndani ya moyo wake kwamba anafanya kazi yake sawasawa.
“Ila kama ataona wanasiasa wanamsifia basi atakuwa kuna sehemu ambazo hatekelezi vyema majukumu yake. Kufanya kazi na wanasiasa kunahitaji busara na sio kufuata vitabu vya sheria vinasemaje,” alimshauri Jaji Mutungi.
Alisema baada ya kustaafu ana mpango wa kufanya kazi za ushauri katika siasa za kimataifa na sio siasa za maji taka.
“Nahitaji muda kidogo kufikiri nitafanya nini ila napenda sana kuwa ‘international consultant’ kwenye masuala ya siasa, lakini pia ikumbukwe kwamba mimi ni mwanasheria ambaye nimekuwa katika masuala ya uwakili kwa takriban miaka 23. Muda utaongea nifanye nini, ngoja kwanza nikabidhi ofisi,” alisema Tendwa.
Source: Mwananchi
Tuesday, August 6, 2013
Breaking News: Moto wateketeza uwanja wa ndege Kenya
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta
umefungwa baada ya moto mkubwa kutokea katika uwanja huo mjini Nairobi.
Kwa sasa moto huo umeweza kudhibitiwa
Rais Uhuru Kenyatta amewasili katika uwanja huo
na anatarjiwa kuhutibia waandishi wa habari baadaye. Hadi kufikia sasa
hakuna ripoti zozote za majeruhi .Mwandishi wa BBC katika uwanja huo amesema kuwa kulikuwa na moshi mkubwa uliotoka katika eneo la kuondokea na kuingilia wageni.
Mamlaka ya uwanja huo imesema kuwa tayari watu waliokuwa katika eneo hilo wameondolewa.
Imesema kuwa baadhi ya operesheni za uwanja huo zimekatizwa huku ndege zinazoingia katika uwanja huo zikielekezwa kutua katika viwanja vingine ndege kama vile Entebe, Dar es Salam ,Kigali, Mombasa na kwingineko nchini Kenya.
Baadhi ya safari za ndege kutoka uwanja huo pia zime-ahirishwa.
Mwishoni mwa wiki jana baadhi ya wenye maduka ya Duty Free katika uwanja huo walifurushwa baada ya serikali kusema kuwa leseni za wenye maduka zilikuwa zimepitwa na muda.
Hata hivyo chanzo cha moto bado hakijabainika.
Source: BBC
Afutiwa kesi ya kumteka Dk. Ulimboka lakini ashtakiwa kwa kudanganya kumteka
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia mashtaka raia wa
Kenya, Joshua Mulundi kuhusu kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka na sasa atakabiliwa na
mashtaka ya kuidanganya polisi kuhusika kumteka daktari huyo.
Hakimu Warialwande Lema aliyekuwa akisikiliza kesi
hiyo, alifikia hatua hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma
(DPP), kuwasilisha hati ya kumfutia mashtaka hayo.
Hati hiyo ya DPP iliwasilishwa mahakamani hapo na
Wakili wa Serikali, Beatha Kitau kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya
kuangalia kama upelelezi umekamilika.
![]() |
| Mtuhumiwa Joshua Mulundi |
Akiwasilisha hati hiyo mahakamani, Wakili Kitau
alisema DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa, chini
ya Kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka. Kutokana na
uamuzi huo wa DPP, Hakimu Lema alimfutia mashtaka Mulundi na kumwachia
huru.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye, alikamatwa na kufunguliwa kesi nyingine ya kutoa taarifa za uongo kwa Jeshi la Polisi.
Katika kesi hiyo mpya inayosikilizwa na Hakimu
Mkazi Aloyce Katemana, Wakili wa Serikali Mwandamizi Tumaini Kweka,
alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai, 2012, katika Kituo
cha Polisi Oysterbay.
Wakili Kweka alidai kuwa siku hiyo mshtakiwa akiwa
kituoni hapo alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa polisi kuwa yeye na
wenzake ndiyo waliokodiwa ili kumteka na kumdhuru Dk Ulimboka wakati
akijua kuwa si kweli.
Mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo.
Wakili Kweka alisema upelelezi wa kesi hiyo
umeshakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili waweze kuandaa
maelezo ya awali ya kesi hiyo. Pia aliweka pingamizi la dhamana dhidi ya
mshtakiwa akidai hana makazi ya kudumu kwa kuwa si raia pia kwa ajili
ya usalama wake kulingana na mazingira ya tukio hilo.
Kauli hiyo ya Wakili Kweka ilimfanya mshtakiwa
huyo alipuke na kudai kuwa wanamfungulia kesi za uongo ambazo hahusiki
na kudai kwamba wamepanga kumpoteza.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba unisamehe, kwa kile
nitakachokifanya, kwani nikirudi mahabusu mimi itaniumiza,” alidai
mshtakiwa huyo na kusisitiza kuwa hahusiki na kwamba bado ni kijana
mdogo.
Baada ya mshtakiwa huyo kulalamika hivyo, Hakimu
Katemana aliutaka upande wa mashtaka uwasilishe hati ya kuzuia dhamana
ambayo hata hivyo, hawakuwa nayo licha ya kuwaongezea saa mbili kuandaa.
Baada ya kushindwa, Hakimu Katemana alimpa mshtakiwa masharti ya
dhamana, ambayo hata hivyo, naye hakuweza kuyatekeleza hivyo kurudishwa
mahabusu, hadi Agosti 20, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.
Masharti hayo ya dhamana yalikuwa ni kuwa na
wadhamini wawili, mmoja akitoka katika taasisi inayofahamika, ambao wote
na yeye, watasaini hati ya Sh5 milioni kila mmoja na kuwasilisha
mahakamani hati zake za kusafiria.
Mulundi alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza
Julai 14, 2012 na kusomewa mashtaka mawili ya kumteka na kutaka kumuua
Dk Ulimboka.
Katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Hakimu Mkazi,
Agnes Mchome, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya alidai
kuwa Mulundi ambaye ni mkazi wa Murang’a, Kenya, alimteka Dk Ulimboka
Juni 26, 2012 akiwa eneo la Leaders Club, Kinondoni.
Katika shtaka la pili, Wakili Komanya alidai kuwa
tarehe hiyohiyo, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande Tegeta, Dar es
Salaam kinyume na sheria, mshitakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo
Dk Ulimboka.
Dk Ulimboka aliokotwa na msamaria mwema Juni 27,
2012 akiwa hajitambui katika msitu huo wa Mabwepande huku akiwa na
majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mshtakiwa alifikishwa polisi, baada ya kwenda
katika Kanisa la Ufufuo na Uzima Kawe la Josephat Gwajima, ambako alidai
kuwa anataka kutubu kwa kuwa yeye na wenzake ndiyo waliomteka Dk
Ulimboka.
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Afutiwa-kesi-ya-kumteka-Ulimboka-lakini-ashtakiwa/-/1597296/1939696/-/uhpb5j/-/index.html
Source: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Afutiwa-kesi-ya-kumteka-Ulimboka-lakini-ashtakiwa/-/1597296/1939696/-/uhpb5j/-/index.html
TAMKO LA CHADEMA DHIDI YA ALIYEKUWA MSAJILI WA VYAMA SIASA JOHN TENDWA
John Tendwa alipaswa kuwa ameondoka kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, tangu mwaka 2008, alipofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Aliendelea kufanya kazi zake hata baada ya muda wa mkataba wake alioongezewa kuwa umefikia mwisho, hivyo alikuwa anakalia ofisi hiyo ya umma, kinyume cha sheria.
![]() |
| John Tendwa |
Ametumia muda huo wa miezi kadhaa, aliokuwa anakalia ofisi ya umma kinyume cha sheria, kuropoka na kuharibu demokrasia, kwa manufaa ya mamlaka iliyomteua na CCM. Kutokana na mwenendo (maneno na matendo) wake mbovu, CHADEMA ilitangaza kutokumpatia ushirikiano wowote, yeye kama Tendwa. Ikamtangaza kuwa adui wa demokrasia nchini.
Kwa muda wote huo, CHADEMA ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Badala ya kuifuta CHADEMA na kufanikisha dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye.
Kuondoka kwa Tendwa hakuzuii kutekelezwa kwa mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, iliyomkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa, hivyo akasababisha kutokea kwa mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Nyololo, Iringa.
Hivyo CHADEMA, kupitia Kurugenzi ya Habari na Uenezi, inataka kauli ya Rais Jakaya Kikwete juu ya utekelezaji wa mapendekezo hayo kwa Tendwa watu wengine, akiwemo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na wote waliotajwa katika ripoti hiyo ya chombo cha serikali, kuwa walivunja sheria za nchi na kusababisha mauaji ya mwandishi, raia asiyekuwa na hatia.
Tunamkaribisha 'with benefit of doubt', msajili mpya, Jaji Francis Mutungi, kwenye kazi na majukumu yake mapya. Wapenda demokrasia na maendeleo nchini, wanamtarajia atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia haki, sheria na utawala bora, asije akapita njia ya Tendwa.
Kupitia mchakato wa Katiba Mpya unaojadiliwa sasa hivi, CHADEMA tunapendekeza Ofisi ya Msajili ipewe uhuru zaidi na uteuzi wake, usiwe suala la Rais kuamka tu na kuamua kuteua bila wahusika kuomba, kuchujwa na kuthibitishwa na mamlaka nyingine tofauti na iliyoteua.
Tunatambua kuwa msajili mpya aliwahi kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani, kwa muda mfupi, kisha akateuliwa kuwa Jaji na akateuliwa pia nafasi zingine. Na sasa mwaka mmoja baada ya kutumikia nafasi hizo, ameteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Jaji Mutungi, anapaswa kuonesha kwa maneno na vitendo kwamba hatakuwa kama Tendwa, kwa kuanza kushughulikia matendo ya kiharamia yaliyofanywa na Green Guards wa CCM kwenye chaguzi za madiwani, zilizomalizika karibuni, ambazo si tu yalikuwa kinyume na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambayo Jeshi la Polisi wanatakiwa kuchukua hatua, bali pia yalikuwa kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa. Hivyo yako kwenye mamlaka yake.
Jaji Mutungi, amshauri Rais Jakaya Kikwete kushughulikia mapendekezo ya Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, juu ya uvunjifu wa sheria wa wazi uliofanywa na askari polisi na John Tendwa, hivyo kusababisha mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012, huko Nyololo, Iringa.
Aidha, Jaji Mutungi anapaswa kumshauri Rais Kikwete kujibu na kufanyia kazi barua mbili alizoandikiwa na CHADEMA juu ya kuunda Tume Huru ya Kimahakama/Kijaji, kuchunguza mauaji yaliyofanyika kwenye shughuli halali za kisiasa za CHADEMA.
Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mauaji mfululizo mkoani Morogoro na Iringa, CHADEMA ilimwandikia barua Rais Kikwete kumtaka aunde Tume ya Kimahakama kuchunguza utata wa vifo hivyo na vingine kadhaa vilivyotokea kwenye shughuli halali za kisiasa, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ili ukweli ujulikane, haki itendeke na wahusika wachukuliwe hatua, hadi sasa rais hajafanya hivyo.
Itakumbukwa pia kuwa baada ya mlipuko wa bomu la Arusha, kwenye mkutano wa kampeni, CHADEMA pia ilimtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake kuunda Tume Huru ya Kimahakama, ili ushahidi juu ya tukio hilo uwasilishwe, hadi sasa pia rais yuko kimya. Hivyo kwa nafasi yake, msajili mpya atoe ushauri kwa rais kuchukua hatua hizo, ili vyama vitimize wajibu wa kikatiba kufanya kazi zake kwa haki, uhuru na sheria za nchi zinazosimamia shughuli za vyama vya siasa nchini.Imetolewa leo, Jumatatu, 5 Agosti, 2013 na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari, CHADEMA
Monday, August 5, 2013
KWA HERI JOHN TENDWA KARIBU JAJI MTUNGI MSAJILI MPYA WA VYAMA VYA SIASA
Jaji Francis S.K.Mutungi ateuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, baada ya John Tendwa kustaafu utumishi wa umma
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARIRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji Francis S.K.Mutungi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
![]() |
| John Tendwa |
Taarifa iliyotolewa Dar Es Salaam leo, Jumatatu, Agosti 5, 2013, na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza Ijumaa iliyopita Agosti 2, 2013.
Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. John Tendwa ambaye amestaafu Utumishi wa Umma kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Saturday, August 3, 2013
Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, kwa Wananchi, Julai 31, 2013
Utangulizi
Ndugu wananchi;
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha
kwa mara nyingine tena kutekeleza utaratibu wetu huu mzuri tuliojiwekea wa Rais
kuzungumza na taifa kila mwisho wa
mwezi.
Ndugu Wananchi;
Mwezi Julai, 2013 ulikuwa wa neema
kubwa ya wageni kwa nchi yetu wakiwemo watu na viongozi mashuhuri duniani.
Natoa shukrani nyingi kwa Watanzania wenzangu kwa jinsi tulivyowapokea wageni
wetu zaidi ya 1,700. Wamefurahi kuwepo
kwao nchini na wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu.
Wageni wetu wamekuwa wa manufaa makubwa kwa
nchi yetu. Wamesaidia kuitangaza
Tanzania duniani na kuendeleza fursa za kukuza utalii, biashara na uwekezaji
nchini na kwingineko katika Afrika.
Mkutano
wa Smart Partnership
Ndugu wananchi;
Wageni wetu wa kwanza ni wale
waliokuja kuhudhuria Mkutano wa Global
2013 Smart Partnership Dialogue
uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni hadi 1 Julai, 2013.
Mkutano huo
ulihudhuriwa
na watu zaidi ya 800 kutoka mabara
yote duniani wakiwemo Watanzania. Miongoni
mwa waliohudhuria ni pamoja na wakuu wa nchi na Serikali, viongozi wastaafu,
wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika na taasisi za kimataifa, makampuni ya
ndani na nje, wafanyabiashara, wasomi, asasi za kijamii na watu wa makundi
mbalimbali katika jamii.
Makampuni yetu 21 nayo yaliungana na makampuni mengine
28 kutoka nje ya nchi kushiriki
kwenye maonesho ya matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika sambamba na
mkutano huo.
Ndugu Wananchi;
Agenda kuu ya majadiliano ya mwaka huu
ilikuwa ni “Matumizi ya teknolojia kama
nyenzo ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi Barani Afrika (Leveraging Technology for Africa’s
Social-Economic Transformation: The Smart Partnership Way). Tuliichagua mada hii kwa kuwa ni ukweli ulio
wazi kuwa matumizi ya sayansi na teknolojia
ndiyo chachu kubwa iliyoleta mageuzi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika
nchi.
Ndiyo siri ya mafanikio katika nchi zilizoendelea na zinazopiga kasi kubwa
ya maendeleo duniani.
Bahati
mbaya sana kumekuwa na maendeleo na matumizi madogo ya sayansi na teknolojia katika
Afrika. Ndiyo maana nchi za Afrika ziko
nyuma kimaendeleo ukilinganisha na zile zilizoendelea. Katika mkutano huo umuhimu wa kuendeleza na
kuongeza matumizi ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya maendeleo Barani Afrika
ulitambuliwa na kusisitizwa.
Mkutano
ulihimiza na kusisitiza kuwa sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya nchi za
Afrika zitoe kipaumbele kwa kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia. Nchi zetu zimehimizwa kuwekeza katika elimu
ya sayansi na teknolojia pamoja na kujenga uwezo wetu wa ndani wa uvumbuzi,
ubunifu, umiliki na uendelezaji wa sayansi na teknolojia. Aidha, imesisitizwa
kwa nchi zetu ziongeze kasi ya kutumia sayansi
na teknolojia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kuongeza
ufanisi na kasi ya maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Jambo la kutia
faraja kwetu nchini ni kwamba mambo yote hayo tunayafanya. Tunachotakiwa sasa ni kufanya vizuri zaidi
na kuongeza uwekezaji na kasi ya kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia
katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Tutaendelea kuboresha sera, kuboresha
mazingira ya uwekezaji na kwa ajili ya maendeleo ya sayansi na teknolojia
nchini.
Ziara ya Rais wa Marekani Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Mgeni wetu wa pili alikuwa Rais wa
Marekani, Mheshimiwa Barack Obama, aliyefanya ziara nchini kwetu kati ya tarehe
1 - 2 Julai, 2013. Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha
uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Marekani na Tanzania.
Kama mjuavyo, nchi zetu mbili zina uhusiano
wa kibalozi tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 na Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar mwaka 1964.
Uhusiano wetu umepita katika vipindi
mbalimbali na kwamba hivi sasa umekuwa mzuri zaidi kuliko wakati mwingine wowote
katika historia ya nchi zetu mbili.
Kumekuwepo na ongezeko kubwa la misaada ya maendeleo kutoka Marekani na
uwekezaji wa vitega uchumi na biashara navyo vinakua. Pia ziara za kiserikali za viongozi wa nchi
zetu kutembeleana zimeongezeka. Kama mtakavyokumbuka, mwaka 2008 aliyekuwa Rais
wa Marekani Mheshimiwa George W. Bush alifanya ziara ya siku nne nchini.
Pia Mawaziri mbalimbali wa Serikali ya
Marekani wametembelea Tanzania akiwemo Mheshimiwa Hilary Clinton akiwa Waziri
wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyekuja mwaka 2011.
Ndugu Wananchi;
Nchi ya Marekani imekuwa mshirika wetu
muhimu wa maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wa afya kwa mfano, tunapata msaada mkubwa katika mapambano
dhidi ya malaria na UKIMWI. Katika
maendeleo ya elimu, nako wanatusaidia katika mafunzo ya wataalamu mbalimbali
pamoja na upatikanaji wa vitabu vya sayansi na hisabati kwa ajili ya shule za sekondari.
Kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia,
Marekani inatusaidia katika kuimarisha miundomuinu ya barabara, umeme na
maji. Ujenzi wa barabara za Tanga –
Horohoro, Namtumbo – Songea – Mbinga; Tunduma – Sumbawanga na baadhi ya
barabara za Pemba, ujenzi wa njia ya pili ya kupeleka umeme Unguja kutoka Dar
es Salaam, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na usambazaji wa umeme katika
Mikoa 10 ya Tanzania bara ni miongoni mwa matunda ya msaada wa Mfuko huo. Pamoja na hayo, ipo miradi ya kuongeza maji
katika jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Morogoro ambayo inaendelea
kutekelezwa.
Ndugu Wananchi;
Wakati wa ziara yake, Rais Obama
alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali yake ya kuimarisha zaidi
uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu. Alielezea kuridhika na hatua tuliyofikia ya kukuza
demokrasia nchini, utawala bora na kuwekeza katika maendeleo ya watu wetu. Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi
zetu.
Katika hili ameahidi kuongeza
misaada ya maendeleo na kiufundi katika sekta za afya, elimu, kilimo, barabara,
nishati na maendeleo ya vijana. Pia,
alithibitisha kwamba nchi yetu itaendelea kunufaika na ufadhili wa Awamu ya
Pili ya Mfuko wa Changamoto za Millenia.
Katika awamu hii, maeneo yatakayopewa kipaumbele hapa kwetu ni umeme na
barabara za vijijini. Mazungumzo ya
miradi itakayotekelezwa katika awamu hiyo yanaendelea vizuri.
Power
Africa
Ndugu Wananchi;
Rais Obama alitumia fursa ya ziara
yake nchini kuzindua mpango wa Serikali yake wa kusaidia maendeleo ya sekta ya
umeme katika Bara la Afrika. Mpango huu
unaoitwa “Power Africa Initiative” umetengewa kiasi cha dola za Marekani bilioni 7 na Serikali ya Marekani na
makampuni binafsi ya nchi hiyo yameahidi kuwekeza dola bilioni 9 katika mpango huo.
Kwa kuanzia, nchi sita za
Afrika (Ethiopia, Ghana, Nigeria, Tanzania, Liberia na Kenya) ikiwemo Tanzania
zitahusishwa.
Bila ya shaka Mpango huo ukikamilika utasaidia
sana kuimarisha upatikanaji wa umeme barani Afrika ambayo ni nyenzo muhimu
katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ni ukweli ulio wazi kuwa ukosefu wa umeme wa kutosha na wa uhakika ni
sababu kubwa inayokwamisha maendeleo ya haraka katika nchi za Afrika.
Hivyo basi, msaada huu ni muhimu sana kwetu. Kwa ajili hiyo nimeagiza Wizara ya Nishati
na Madini iandae mkakati madhubuti wa namna Tanzania itakavyoshiriki na
kufaidika na mpango huo. Nataka mpango
huo utakapoanza kutekelezwa utukute sisi tupo tayari kutumia fursa zake.
Vile vile, ndugu wananchi, katika
ziara hiyo Rais Obama alielezea nia ya Serikali yake kutaka kuwepo mpango wa kukuza
ushirikiano wa biashara na uwekezaji baina ya nchi yake na nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Nimeelekeza Wizara
husika yaani Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda,
Biashara na Masoko nao watengeneze mkakati utakaoonesha jinsi tulivyojipanga
kufaidika na mpango huo. Lazima
tujiandae vyema na mapema tunufaike saiwa na mpango huo.
Ziara
ya Rais Mstaafu wa Marekani Nchini
Ndugu Wananchi;
Sambamba na ziara ya Rais Obama, nchi
yetu ilipata bahati ya kutembelewa tena na Rais Mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa
George W. Bush na mkewe Laura Bush, tarehe 1 hadi 3 Julai, 2013. Kwa udhamini wa asasi ya George W. Bush
Foundation waliandaa Mkutano wa Wake wa Marais wa Afrika uliofanyika hapa Dar
es Salaam, tarehe 2 na 3 Julai, 2013. Mama
Michelle Obama naye alishiriki mkutano huo uliozungumzia kuimarisha maendeleo
na afya ya wanawake Barani Afrika.
Katika mkutano huo, pia, Mheshimiwa
George W. Bush alizindua mpango wa kuimarisha mapambano dhidi ya kansa ya
shingo ya kizazi na matiti barani Afrika.
Kufuatia Mpango huo, Serikali ya Marekani imetoa dola milioni 3 na mashine 16 za Cryo Therapy zinazotumia baridi
kali kuua chembechembe za kansa. Msaada
huo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa kila mwaka hapa nchini zaidi ya Watanzania
21,000 wanapata maradhi ya kansa.
Kati
ya hao asilimia 29.4 ni wanawake wanaopata magonjwa ya kansa ya
shingo ya uzazi na asilimia 6.2
wanapata kansa ya matiti. Naamini Mpango huu utatusaidia sana katika kuimarisha
mapambano dhidi ya maradhi haya yanayowasumbua na kuua kina mama wengi
nchini. Nimeitaka Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kuweka utaratibu mzuri ili msaada huo utumike ipasavyo na kuwanufaisha
walengwa.
Ziara ya
Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 23 mwezi Julai, 2013 pia
tulitembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Mheshimiwa Tony Blair. Katika mazungumzo yetu Mheshimiwa Blair
aliahidi kuisaidia nchi yetu kupitia taasisi yake ya Africa Governance
Initiative kusaidia kusambaza umeme wa jua katika shule zetu za sekondari
vijijini, maboresho ya shirika letu la umeme (TANESCO) na kusaidia uanzishaji
na uimarishaji wa Kitengo cha Rais cha Ufuatiliaji Utekelezaji wa Programu za
Maendeleo (Presidential Delivery Bureau - PDB).
Tunamshukuru kwa ahadi yake hiyo itakayochangia katika jitihada za
kujiletea maendeleo.
Ziara
ya Waziri Mkuu wa Thailand Nchini
Ndugu Wananchi;
Tarehe 30 Julai, 2013 tulimpokea Mheshimiwa
Yingluck Shinawatra, Waziri Mkuu wa Thailand aliyefanya ziara ya siku tatu
nchini. Lengo la ziara yake ni
kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Thailand na Tanzania. Katika ziara
hiyo, tumezindua Jukwaa la Wafanyabiashara wa Thailand na Tanzania (Thai-Tanzania
Business Forum) ili kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu.
Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra alitumia
fursa hiyo kufafanua sera ya Thailand kwa Afrika inayosisitiza kukuza
ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na kibiashara. Pia amepata nafasi ya kutembelea Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti kujionea mwenyewe jinsi nchi yetu ilivyobarikiwa kwa kuwa na
kivutio hicho cha aina yake. Alipokuwa
kule nchi zetu zilitiliana saini maelewano ya ushirikiano katika kulinda na
kuhifadhi wanyama pori.
Katika mazungumzo yangu na yeye, tumekubaliana
kuchukua hatua thabiti kukuza ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Tumetiliana saini mikataba mitano ya
ushirikiano kwa mambo yafuatayo: Kukuza
na kulinda vitega uchumi; kubadilishana wafungwa; ushirikiano wa kiufundi; na
ushirikiano kwa masuala ya madini.
Aidha, Waziri Mkuu huyo ameahidi kuwahimiza
wawekezaji wa nchini mwake kuja Tanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali za
uchumi ikiwemo kilimo, utalii, viwanda nakadhalika.
Pia, Waziri Mkuu wa Thailand ameahidi kuwa Serikali yake
itatoa ufadhili kwa vijana 10 kusoma
Shahada ya Uzamili nchini humo. Vile
vile, nchi hiyo itaanza kuleta wataalamu wa afya wa kujitolea kuja kushirikiana
na wataalam wetu kuimarisha huduma ya afya nchini.
Ziara hizi zinaonesha utayari wa dunia
kuunga mkono jitihada zetu za kujiletea maendeleo. Naomba Watanzania wenzangu tutumie vizuri
utayari huo wa dunia kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Tusijikwaze wenyewe.
Ziara
ya Kagera
Ndugu wananchi;
Kuanzia tarehe 24 hadi 29 Julai, 2013,
nilifanya ziara Mkoani Kagera. Nilishiriki
kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa na kuzindua jengo jipya la Mahakama Kuu.
Pia niliweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba na
kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara za Kigoma –
Lusahunga na Kyaka – Kayanga – Bugene.
Vile vile nilizindua Wilaya mpya ya Kyerwa na kukagua shughuli za
maendeleo pamoja na kuona na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili
wananchi ili kuzitafutia majawabu.
Sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa
zilifana sana. Niliwapongeza viongozi
wa Jeshi na wa Mkoa kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizo. Pia nilirudia kumpongeza Mkuu wa Majeshi,
Jenerali Davis Mwamunyange, kwa uamuzi wake wa busara wa kufanya sherehe za
kumbukumbu za mashujaa wetu pale Kaboya badala ya kufanyikia Dar es Salaam tu
kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Ni
uamuzi muafaka na wa busara kwani pale Kaboya ndipo walipolala mashujaa wetu waliopoteza maisha yao kutetea
mipaka na uhuru wa nchi yetu dhidi ya Nduli Iddi Amin.
Hali kadhalika, kule Naliendele, Mtwara
ambapo sherehe za mashujaa zilifanyika mwaka wa juzi, ndipo walipozikwa
mashujaa wetu waliopoteza maisha kuisaidia nchi jirani na rafiki ya Msumbuji
kutetea Uhuru wake dhidi ya wakoloni, makaburu na vibaraka wao wa ndani ya
Msumbiji.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu pale Kaboya
niliwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba katika kuwakumbuka mashujaa wetu wale
na sisi tulio hai, hatuna budi kutambua wajibu wetu wa kuwa tayari kujitolea
muhanga kwa ajili ya kulinda uhuru wa mipaka ya nchi yetu. Nilisisitiza utayari wa nchi yetu kulinda
mipaka yake na kwamba mfano wa mashujaa waliolala pale ni fundisho kwa mtu ye
yote anayetamani kumega kipande cho chote cha ardhi ya nchi yetu. Atakiona cha mtema kuni kilichomkuta Nduli
Iddi Amini au hata zaidi.
Nimesikia kuwa kauli yangu ile imetafsiriwa
visivyo na kupotoshwa na baadhi vyombo vya habari na hata majirani zetu. Tafsiri hizo ni potofu. Sikumtaja mtu ye yote au nchi yo yote. Nilikuwa nazungumzia wajibu wa majeshi yetu
na raia wa nchi yetu wa kulinda uhuru na mipaka yetu na kwamba hatutamruhusu
mtu au nchi yo yote kutupokonya wala kuichezea haki yetu hiyo ya msingi. Tuko tayari kuitetea hata kama gharama yake
ni maisha yetu kama walivyofanya mashujaa waliolala Kaboya.
Mahakama
Kuu
Ndugu Wananchi;
Katika ufunguzi wa Mahakama Kuu ya
Bukoba nilisisitiza dhamira na utayari wa Serikali yetu kuiwezesha Mahakama ya
Tanzania kuwa na Mahakama Kuu katika kila Mkoa.
Baada ya kukamilika kwa Mahakama Kuu ya Bukoba bado kuna Mikoa 14 hainazo. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14
tumetenga fedha za kujenga Mahakama Kuu katika Mikoa 7 na nilirudia ahadi yangu
kuwa katika mwaka ujao wa fedha tutatoa fedha za kumalizia Mikoa 7
iliyosalia.
Niliamua tuongeze kasi ya
kujenga Mahakama Kuu hizo ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kutimiza ipasavyo
wajibu wake wa kutoa haki nchini.
Maendeleo
ya Mkoa wa Kagera
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa Kagera nilifurahishwa na
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Taarifa za Mkoa na Wilaya zimefafanua kwa
kina mambo mazuri yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika Mkoani. Wameelezea furaha yao kwa mafanikio
yaliyopatikana ambayo baadhi nimeyashuhudia au hata kushiriki kuyazindua na
kuweka mawe ya msingi.
Taarifa hizo pia
zimelezea mambo mengi zaidi wanayotaka yafanyike na matatizo mapya na hata ya
zamani ambayo wanataka yapatiwe ufumbuzi.
Katika mazungumzo yangu na viongozi na
wananchi, yapo mambo ambayo yako kwenye uwezo wao kijijini, Wilayani na Mkoani
kuyapatia ufumbuzi. Tulikubaliana na
kuelekezana nini kifanyike. Yapo mengine
mengine ambayo yanahitaji nguvu ya taifa tumeyachukua kuja kuyafanyia
kazi. Kuna baadhi yaliwahusu Mawaziri
ambao nilikuwa nao ziarani waliyasemea na kuyafanyia kazi palepale
yalipojitokeza.
Ulinzi
na Usalama
Ndugu Wananchi;
Kuna mambo matatu yahusuyo usalama
ambayo yalizungumzwa na wananchi kwa uchungu mkubwa ambayo niliamua
tuyashughulikie kitaifa. Mambo hayo ni
ujambazi wa kutumia silaha kuteka magari, kupora mali na watu kuuawa. Jambo la pili ni wahamiaji kutoka nchi jirani
wanaoingia, kuishi na kufanya shughuli nchini kinyume cha sheria. Na tatu, mifugo kuingizwa kwa wingi nchini
bila kufuata taratibu husika na mingine kuingizwa katika hifadhi za wanyama.
Ndugu wananchi;
Nilitoa maagizo kwa wakuu wa vyombo
vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Uhamiaji
watengeneze mpango kabambe wa kuyashughulikia matatizo hayo.
Watayarishe na kutekeleza operesheni maalum
itakayo au zitakazokomesha ujambazi, kuondoa wahamiaji wasiokuwa halali na
kuondoa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume na utaratibu na ile iliyoko kwenye
maeneo yasiyo stahili.
Aidha, niliwataka majambazi
wajisalimishe na wasalimishe silaha zao ndani ya wiki mbili na siku hizo
zinaanzia tarehe 29 Julai, 2013 nilipomaliza ziara yangu Mkoani humo.
Kwa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha
sheria nimewataka watumie muda huo kuondoka nchini au kuhalalisha ukaazi
wao. Hivyo hivyo kwa mifugo iliyoingizwa
nchini kinyume na sheria au ile iliyoko kwenye maeneo yasiyostahili. Ndani ya muda huo watu wote waondoe mifugo
yao au wajitokeze kufuata taratibu zilizopo.
Ndugu Wananchi;
Nilisema nilipokuwa Mkoani Kagera na
narudia tena leo kuwa baada ya siku 14 kupita, vyombo vya ulinzi na usalama
vitaendesha operesheni maalum ya kushughulikia matatizo hayo.
Nilisema kuwa operesheni hiyo itafanyika
katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja. Napenda kuwahakikishia kuwa hapatakuwa na
mahali pa kukimbilia wala kujificha.
Nawashauri wale wote wanaohusika na ujambazi, uhamiaji haramu na
uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua muafaka sasa. Wasisubiri operesheni iwakute, wala
wasifikirie kuwa hili ni jambo la kupita.
Safari hii itakuwa endelevu.
Ndugu Zangu;
Hatuwezi kukubali hali hii niliyoikuta
Mkoani Kagera ikaachwa kuendelea. Italeta
madhara makubwa zaidi siku za usoni. Haiwezekani
raia katika nchi yake, akose uhuru na usalama wa kutembea peke yake mpaka
asindikizwe na Polisi. Na, baya zaidi
hata Polisi nao wanashambuliwa na kuuawa watakavyo majambazi. Uhalifu huu lazima ukomeshwe, uishe na
usijirudie tena.
Pia, haiwezekani hali ya watu kutoka
nchi jirani kuingia nchini, kuishi na kufanya shughuli na kutoka watakavyo. Hatuzuii watu kuingia na kuishi Tanzania
lakini wafuate sheria na taratibu za kuhamia na kuishi katika nchi yetu.
Nchi yetu ina sifa na ukarimu huo. Hakuna
uthibitisho mkubwa zaidi ya ule wa mwaka 1982, Rais Julius Nyerere wakati ule
alipowaruhusu wakimbizi wanaopenda kuwa raia wa Tanzania wafanye hivyo.
Wakimbizi 30,000 tu waliitumia fursa hiyo.
Mwaka 2010 tuliwapa uraia wakimbizi 160,000
wa kutoka Burundi. Kwa sababu
hiyo hatuoni sababu ya watu kufanya wanayoyafanya sasa kule Mkoani Kagera. Hatuwezi kuacha hali hiyo iendelee ilivyo.
Ndugu Wananchi;
Nilipokuwa Mkoani Kagera nilielezea
kusikitishwa kwangu na vitendo vya baadhi ya watendaji na viongozi wa vijiji na
wananchi kuwaruhusu watu kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria. Nimewataka waache mtindo huo. Nimeagiza na wao wajumuishwe katika
operesheni ijayo.
Watakaobainika
kujihusisha na vitendo hivyo haramu wachukuliwe hatua zipasazo kisheria. Aidha, niliwataka Maafisa wa Uhamiaji
watimize ipasavyo wajibu wao. Ukweli ni
kwamba, mambo haya kuendelea kwa muda mrefu kiasi hiki ni kwa sababu ya udhaifu
wa mamlaka husika.
Vile vile, nimewataka
TAKUKURU nao watimize wajibu wao. Hapa
kuna uthibitisho tosha wa kuwepo kwa vitendo vya rushwa vinavyohusisha
wahamiaji hao na maofisa wa vijiji na idara husika za Serikali. Mimi naamini kama TAKUKURU ikiwabana na
Uhamiaji wakichemka vya kutosha tatizo hili lingepungua sana au hata kutokuwepo
kabisa.
Uhusiano
na Nchi ya Rwanda
Ndugu wananchi;
Katika kipindi cha miezi miwili sasa hususan
tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi yetu na Rwanda
unapitia katika wakati mgumu.
Kauli za
viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu ni ushahidi wa kuwepo hali
hiyo. Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu
na ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania
tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo
kwa nchi zote jirani. Kama majirani kila
mmoja anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano
mzuri.
Napenda kusisitiza kuwa mimi na
Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya
dhidi ya Rwanda au nchi yo yote jirani au yo yote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo
ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.
Ndugu Wananchi;
Ukweli ni kwamba wakati wote tumekuwa
tunajihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo
ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi zetu.
Hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya
Nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu na nchi ya Rwanda kabla
na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa.
Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda
kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na
ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo
lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye
vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu.
Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la
hasha. Sijafanya hivyo kwa sababu sioni
faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna
mgogoro wa aina yo yote. Busara
inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo.
Waingereza wanasema “two wrongs do
not make a right”.
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo uhusiano wetu na Rwanda
umekuwa mzuri kwa miaka mingi.
Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa
na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika Umoja
wa Afrika na hata kimataifa.
Uhusiano
unaelekea kupata mtikisiko baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda
kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri ule
niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza
kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa
Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda.
Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli
yangu. Rais wa Rwanda hakusema cho chote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza
kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.
Kwa kweli nimestaajabu sana na jinsi
walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely out of proportion and out of context. Mimi nilifanya
vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda
wetu.
Tumekuwa tunakutana katika mikutano
na vikao mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za
kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea. Wakati wote tumeyachukulia kuwa ni mambo
yanayotuhusu sote hivyo kupeana ushauri ni wajibu wetu wote.
Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana
kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo
mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri
si amri. Una hiyari ya kuukubali au
kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri wako”. Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno
yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia kusema kuwa mimi
binafsi na Serikali yetu ya Tanzania hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya na
Rwanda. Tunapenda tuendelee kuwa na
uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu
wanalo lao jambo dhidi yetu ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa
na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu. Hatupendi kuyaamini moja kwa moja
tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza, naomba kutumia
nafasi hii pia kuwatakia Waislamu wote nchini heri na baraka tele katika
kukamilisha ibada muhimu ya kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Naomba tuendelee kuwatakia heri ili wamalize
salama na tuweze kusherehekea kwa furaha na bashasha tele siku kuu ya Idd el
Fitr pindi itakapowadia.
Mwisho kabisa, nawaomba Watanzania
wenzangu wote tuendelee kushirikiana na kuishi kwa upendo, umoja na mshikamano
kama ilivyo kawaida yetu.
Mungu Ibariki
Tanzania!
Mungu Ibariki
Afrika!
Asanteni Sana
Kwa Kunisikiliza.
Subscribe to:
Posts (Atom)








